Monday 4 November 2019

TAA Kufanikisha Mazingira Bora ya Kujisomea Wanafunzi 1560

Skauti wa shule ya Sekondari ya Ilala (kushoto) akimvisha skafu mgeni rasmi wa mahafali ya 13 ya shule hiyo, Bi. Harieth Nyalusi, Kaimu Meneja Biashara na Masoko wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu Mhandisi Julius Ndyamukama. Mahafali hayo yamefanyika hivi karibuni.



Na Bahati Mollel,TAA
WANAFUNZI 1560 wa shule ya sekondari ya Ilala ya Jijini Dar es Salaam, watasoma kwa furaha baada ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kukubali kufanya ukarabati wa jengo la maktaba, ambalo ni chakavu.


Ahadi hiyo imetolewa hivi karibuni na Kaimu Meneja Masoko na Biashara wa TAA, Harieth Nyalusi ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mahafali ya 11 ya shule hiyo, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama.

Nyalusi alisema kuwa Mamlaka inaunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli za kutoa elimu bure, ambapo sasa itaungana naye katika kukarabati chumba hicho cha maktaba, ili kuwezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora, yatakayochangia kufanya vyema katika masomo yao na katika  mitihani ya kidato cha pili na yake ya kuhitimu kidato cha nne.

     Mwanafunzi Diana Seth wa shule ya sekondari ya Ilala (kulia) akionesha moja ya majaribio katika maabara ya Biolojia, wakati wageni waalikwa pamoja na mgeni rasmi wa mahafali ya 13 ya shule hiyo, Bi. Harieth Nyalusi kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania  (wa pili kushoto), akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama walipotembelea maabara hiyo.


“Pamoja na kuunga juhudi za Mhe. Rais pia ni sera ya taasisi yetu kutoa kwa jamii katika kusaidia kutatua changamoto zinazozibabili jamii hizo, hivyo kama Mamlaka tutasaidia kufanya ukarabati wa ndani wa jengo hilo ambalo limekuwa chakavu, linalosababisha ari ya kusoma kushuka,” amesema.

Pia alisema Mamlaka inatambua jitihada kubwa inayofanywa kwa kushirikiana kwa Walimu, wazazi na wanafunzi katika kuhakikisha shule inaboresha utoaji wa elimu bora na ufaulu wa wanafunzi wa mitihani yao ijayo kuongezeka.

Hatahivyo, ametoa wito kwa wahitimu wa kidato cha Nne 2019 kuhakikisha wanaweka nia thabiti ya kujiendeleza zaidi kwa wale watakaobahatika kuchaguliwa  kwenda kidato cha Tano na vyuo mbalimbali, na ambao hawatabahatika waangalie nyanja mbalimbali za elimu ili kujitengenezea wigo mpana wa uwezo wa utambuzi wa kubadilisha changamoto zinazoizunguka jamii kuwa fursa.

  Kaimu Meneja wa Biashara na Masoko  wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bi. Harieth Nyalusi (aliyesimama), akiwakilisha salamu kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama wakati wa mahafali ya 13 ya shule ya sekondari ya Ilala ya Jijini Dar es Salaam, yaliyofanyika hivi karibuni.
“Ikumbukwe kuwa vijana ni hazina ya Taifa, hivyo napenda kuwasisitiza kuwa thamani yako kama kijana iko mikononi mwako, ishi kwa malengo, jitambue, jithamini, jilinde na ujitunze kwani wewe ni wathamani kuwa na Taifa linakutegemea,” amesema.

Akiizungumzia TAA, Nyalusi amesema imepewa jukumu la kusimamia na kuendeleza viwanja vya ndege 58 vilivyopo Tanzania Bara kati ya hivyo ni viwanja vya Kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA), ambavyo ndivyo milango mikuu ya kuingia nchini kwa kutokea nje ya nchi.

Amesema katika viwanja vya ndege kuna fursa mbalimbali za kibiashara, ajira rasmi na zisizo rasmi, ambapo amewataka vijana wanaohitimu kuzichangamkia ajira na fursa hizo pindi zitakapotangazwa.

Wanafunzi skauti wa shule ya sekondari ya Ilala wakionesha ukakamavu kwa kupasuliwa tofali kichwani katika sherehe za mahafali ya 13 ya shule hiyo yaliyofanyika hivi karibu.


Kwa upande wa risala ya wahitimu, imeeleza kuwa shule hiyo iliyoanzishwa miaka 13 iliyopita pamoja na kufanya vyema kwenye mitihani yao ya taifa ya kumaliza kidato cha nne kila mwaka, imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya upungufu wa vyoo vya wanafunzi, ambapo yapo matundu 18  kati ya 72 yanayohitajika; ukosefu wa maabara mbili za masomo ya Biolojia na Fizikia ambazo ujenzi wake haujakamilika.

Changamoto nyingine ni uchakavu wa majengo ya shule ikiwemo kuvuja kwa paa na ubovu wa sakafu madarasani; uchakavu wa rangi katika majengo yote ya shule; ukosefu wa chumba maalum cha watoto wa kike na wagonjwa pindi wapatapo matatizo wanapokuwa eneo la shule; ukosefu wa vifaa vya teknolojia na mawasiliano zikiwemo komputa, projeta, mashine za kurudufia na ‘printer’.

 Mmoja wa skauti wa shule ya sekondari ya Ilala ya Jijini Dar es Salaam akizuia pikipiki mbili kwa mikono na kichwa katika sherehe za mahafali ya 13 ya shule hiyo yaliyofanyika hivi karibuni.

Risala hiyo imeainisha pia changamoto za ukosefu wa jengo la ofisi za walimu, ambapo sasa wanatumia madarasa mawili kama ofisi jambo ambalo pia kumesababisha kuwe na upungufu wa madarasa; uchakavu wa maktaba na ukosefu wa vifaa muhimu ndani ya maktaba zikiwemo meza, viti, vitabu vya kiada na ziada, makabati; ukosefu wa kantini bora ya shule na ukosefu wa bwalo.
Mwanafunzi Salvatory Jeremia (kushoto), akipokea cheti cha kuhitimu kidato cha nne kutoka kwa mgeni rasmi Bi. Harieth Nyalusi, Kaimu Meneja Biashara na Masoko wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama.  (Picha zote na Bahati Mollel wa TAA).
Pamoja na changamoto hizo, wahitimu hao wameahidi kufanya vyema katika mitihani yao ya kuhitimu kidato cha nne, ambapo kila mwaka ufaulu umekuwa ukiongezeka ambapo sasa umefikia asilimia 70.

   
Wahitimu wa kidato cha Nne katika shule ya sekondari ya Ilala wakiimba wimbo wa kuwaaga wenzao pamoja na walimu katika mahafali yao yaliyofanyika hivi karibuni  jijini Dar es Salaam.


No comments:

Post a Comment