Friday 8 November 2019

Bombardier Nayo Kutua Kiwanja cha Arusha


Na Mwandishi Wetu
NDEGE aina ya Bombardier zitaweza kutua katika Kiwanja cha Ndege cha Arusha baada ya kukamilika mpango wa kuongezwa barabara ya kutua na kuruka ndege, imeelezwa.

Hayo yalisema bungeni mjini Dodoma juzi na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Issac Kamwelwe wakati akijibu swali la Mhe Husna Malima, Mbunge wa Kigoma Kusini aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Arusha ili ndege kubwa ziweze kutua.

Malima alisema kuwa kuongezwa kwa uwanja huo kutawawezesha wananchi wa mikoa ya Singida, Manyara, Simiyu, Mara na Dodoma kuamasika kutumia usafiri wa ndege, ambao unatosheleza kwa sasa?


Amesema mafaniko ya uwepo wa ndege nyingi za abiria nchini ni pamoja na ndege hizo kutumika kwa wananchi kuzipanda.

Kamwelwe amesema kurefushwa huko kutafanikisha ndege aina ya Bombardier ambayo inabeba abiria kuanzia 70 kutua na kuruka bila tatizo kwenye kiwanja hicho kilichopo Kisongo mkoani Arusha.


Amesema tayari bajeti imetengwa kwa ajili ya kazi hiyo, ambapo kiwanja hicho ni cha tatu nchini kwa kutua na kuruka ndege nyingi, ambapo hutua ndege zaidi ya 125 kwa siku.

“Tumeweka bajeti kuendeleza kiwanja cha ndege cha Arusha na tayari tenda imetangazwa, kiwanja hiki kinaongoza kwa kutua ndege nyingi zaidi kwa siku ni biashara kubwa na ndio maana tunataka ndege ya Bombardier itue hapo,” alisisitiza Mhe. Kamwelwe.

Amesema mikoa jirani na Arusha ya Manyara, Singida, Dodoma, Simiyu na Mara itafaidika na maboresho ya kiwanja hicho kwa kuwa wataweza kukitumia ipasavyo.

Naye Meneja wa Kiwanja hicho, Mhandisi Elipid Tesha amesema barabara ya kutua na kuruka ndege itaongezwa urefu kwa meta 200, ambapo sasa ina urefu wa meta 1600 na itakuwa 1800, na pia patajengwa eneo la kugeuza ndege.

Mhandisi Tesha amesema kwa sasa kazi inayoendelea ni ujenzi wa eneo la maegesho ya ndege (Apron), ambayo yakikamilika yatapunguza msongamano kwa asilimia 30; pia barabara ya kupita ndege kwenda katika maegesho (taxiway);  ujenzi wa maegesho ya magari yapatayo 350 kwa kiwango cha lami.

Pia ujenzi wa mfumo wa malipo ya maegesho hayo unaendelea sambamba na ule wa maegesho ya magari.

Pia amesema ujenzi huo wa maboresho ya kiwanja cha ndege cha Arusha utahusisha ujenzi wa eneo la kupumzika abiria, ofisi za waegesha ndege (mashellers), kibanda cha ulinzi na vyoo.

No comments:

Post a Comment