Wednesday 25 September 2019

JAMAFEST, URITHI WETU WAPANDA MLIMA KILIMANJARO


Wawakilishi wa Matamasha ya JAMAFEST na URITHI FESTIVAL  kutoka Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro pamoja na wa Wizara ya Maliasili na Utalii kabla ya kuanza safari ya SIKU SITA kuelekea Kilele cha Uhuru Kama sehemu ya matukio ya Matamasha hayo yaliyozinduliwa na Makamu wa Rais ,Mama Samia Suluhu Hassan. (Na Mpigapicha Wetu).

Na Mwandishi Wetu, Moshi
WAWAKILISHI wanne kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika matamasha JAMAFEST na URITHI FESTIVAL wanaendelea na safari ya siku sita ya kupanda Mlima Kilimanjaro kuelekea kilele cha Uhuru ikiwa ni sehemu ya matamasha hayo yaliyozinduliwa Jumapili na Makamu wa Rais,  Samia Suluhu Hassan.
Wanaopanda Mlima Kilimanjaro kama sehemu ya matamasha hayo makubwa kwa nchi za Afrika Mashariki ni pamoja na Joel Acana kutoka nchini Uganda, Luca Waiganja kutoka nchini Kenya na Anita Brown wa Tanzania wakiwakilisha tamasha la JAMAFEST huku Jocktan Makeke akiwakilisha tamasha la Urithi Festival.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga washiriki hao, Mwakilishi wa Katibu Mkuu waWizara ya Maliasili na Utalii, William Mwita alisema chanzo cha tamasha la JAMAFEST ni utekelezaji wa maelekezo ya sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kutaka Malikale na Utamaduni kutumika kama vivutio vya Utalii.
 “Sekretarieti ilizielekeza nchi wanachama  wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2012 zihakikishe Malikale na utamaduni unatumika kama kivutio cha utalii ili uweze kutumika katika maendeleo ay nchi za afrika Mashariki,”alisema Mwita.
Alisema baada ya maelekezo hayo, sekretarieti ilianzisha tamasha la Sanaa na Utamaduni kwa nchi za Afrika Mashariki likiwa tayari limefanyika katika majiji matatu; Kigali (Rwanda), Nairobi (Kenya), Kampala (Uganda) na sasa linafanyika Dar es Salaam Tanzania.
Kwa Tanzania, tamasha la JAMAFEST lilizinduliwa Jumapili sambamba na tamasha la URITHI FESTIVAL, tamasha ambalo liko kwenye ngazi ya kitaifa likiwa na maudhui kama ya tamasha la JAMAFEST.
Wakati Jamafest inaunganisha wana Afrika Mashariki na kutumika kama kivutio cha Utalii au zao la utalii, Urithi festival linafanya mambo hayo hayo kwa Tanzania, kamba unaunganisha Watanzania na inatumika kama zao la Utalii.
Mapema mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Uhifadhi wa shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Victor Kitansi aliwakapongeza waratibu wa matamasha hayo kufanya uamuzi wa kutumia sehemu ya matukio kuwa ni kushiriki kupanda Mlima Kilimanjaro.
Tamasha la JAMAFEST ambalo hufanyika kila baada ya miaka miwili kuzunguka nchi wanachama linafanyika kwa muda wa siku nane huku Tamasha la Urithi Festiva likifanyika katika mikoa 12 ya Tanzania Bara kwa kila mkoa kuionesha kivutio ambacho kitatumika kama zao la Utalii.

No comments:

Post a Comment