Friday, 17 November 2017

TAA kusaka hati miliki za viwanja vya ndege




Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (aliyesimama mbele), akiongea na wafanyakazi wa Mamlaka hiyo katika mkutano uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Transit uliopo kwenye jengo la kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imesema itahakikisha inapata hati za viwanja vyake vya ndege ili kupunguza uvamizi kutoka kwa wananchi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela  alitoa kauli hiyo leo kwenye mkutano na wafanyakazi uliofanyika katika ukumbi ya Transit uliopo jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI), ikiwa ni moja ya mikakati ya mamlaka hadi kufikia Juni 2018.
Bw. Mayongela alisema tayari wameanza taratibu za kupata hati miliki kwa viwanja 13, vikiwemo vya JNIA na Mwanza zilizofutwa awali.
Hata hivyo, Wananchi wamekuwa na tabia za kuvamia maeneo ya viwanja vya ndege kwa kufanya makazi na mashamba, jambo ambalo ni hatarishi kiusalama.
Bw. Mayongela alisema mkakati mwingine ni kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya viwanja vya ndege 58 vinavyomilikiwa na serikali na ambavyo havipo chini ya serikali.

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kutoka Makao Makuu na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mkuu (hayupo pichani) aliyekuwa akiongelea mikakati na masuala mbalimbali yanayohusiana na maendeleo ya taasisi hiyo.
“Pia tutaanda kikosi kazi kitachosaidiana na wenzetu wa TANROADS katika usimamizi na uangalizi wa viwanja vya ndege  vinavyoendelea kujengwa maeneo mbalimbali nchini,” alisema Bw. Mayongela.
Katika hatua nyingine Bw. Mayongela alisema pia mamlaka inampango wa kuendeleza miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo ya abiria, Mizigo, ufungaji wa taa za kuongezea ndege na ufungaji kamera za usalama (CCTV) kwenye viwanja vya Arusha, Mwanza, JNIA na Dodoma.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Lawrence Thobias aliwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa uweledi na uwazi, ili kufikia malengo yaliyowekwa na hatakuwa tayari kumfukuza mtumishi kazi kwa masuala yasiyokuwa na msingi.
“Ninafungua milango kwa wafanyakazi mje ofisini kwangu kwani hii ni ofisi ya rasilimali watu na sio rasilimali mtu, naweka milango wazi mje tujadili masuala ya kazi ya kujenga na sio majungu,” alisisitiza Bw. Thobias.

Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Lawrence Thobias (aliyesimama mbele), akizungumza na Wafanyakazi katika mkutano uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Transit uliopo kwenye jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).

Tuesday, 14 November 2017

Italia Yashindwa Kufuzu Kombe la Dunia 2018

Wachezaji wa Italia wakifarijiana baada ya kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018. Timu hiyo ilitoka suluhu na Sweden katika mchezo uliofanyika San Siro, Italia baada ya kufungwa 1-0 katika mchezo wa kwanza nchini Sweden, hivyo imetolewa kwa kufungwa 1-0.

ROME, Italia

MABINGWA mara nne wa dunia Italia wameshindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1958 baada ya kushindwa katika mchezo wa mchujo dhidi ya Sweden.

Suluhu dhidi ya Sweden, haikuisaidia Italia kusonga mbele na badala yake wapinzani wao hao ndio wamefuzu kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006 walipofuzu kwa fainali hizo.

Hiyo ina maana kuwa timu ya taifa ya Italia inayojulikana kama Azzurri itakosa mashindano hayo kwa mara ya pili tangu yalipoanzishwa baada ya kushindwa kushiriki wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo mwaka 1930.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Sweden wiki iliyopita, Italia walipokea kichapo cha bao 1-0 kabla ya kutoka suluhu katika mchezo huo wa juzi uliofanyika kwenye Uwanja wa San Siro jijini Milan.

Pamoja na suluhu hiyo, lakini wenyeji ndio walitawala zaidi mchezo huo kwa asilimia 76, licha ya kushindwa kuzifumania nyavu.

PIGO KWA KIPA

Mbali na kutolewa, Italia pia ilipata pigo jingine baada ya kipa wao na baadhi ya wachezaji wengine kuamua kustaafu baada ya timu yao kushindwa kufuzu kwa fainali za mwakani zitakazofanyika Urusi.

Nafasi safi ya Italia kupata bao ilitibuliwa na kipa wa Sweden Robin Olsen alipookoa mpira uliopigwa na mchezaji aliyetokea benchi Stephan El Shaarawy.

Mshambuliaji Ciro Immobile alikosa nafasi kibao na juhudi zake katika kipindi cha kwanza ziliokolewa katika mstari na beki wakati Andreas Granqvist.

Kipa Gianluigi Buffon alisema alikuwa na majonzi makubwa yeye pamoja na wadau wote wa soka wa Italia kwa nchi yao kushindwa kufuzu baada ya kufungwa na Sweden.

Mtu akisoma gazeti la michezo la Italia la "Gazetta dello Sport" huku ukurasa wa mbele ukisomeka "Mwisho" siku moja baada ya Italia kutolewa katika hatua ya kufuzu kwa Kombe la Dunia walipocheza dhidi ya Sweden juzi katika soko la vyakula jijini Rome, Italia.

Buffon, 39, alisema: "Ni aibu kwa mchezo wangu rasmi wa mwisho kwa kuumaliza kwa kushindwa kufuzu kwa Kombe la Dunia.

"Lawama zinagawanywa kwa kila mmoja. Hakuna mtu wa kutupiwa lawama hapa.”

Mchezaji mwenzake na Buffon wanayecheza pamoja na Juventus Andrea Barzagli na kiungo wa Roma Daniele de Rossi pia alimaliza kipindi chake cha kuichezea Italia, wakati Giorgio Chiellini anatarajia kujiunga nao. Wanne hao wamecheza mechi 461 miongoni mwao.


Kipa Buffon ameichezea timu hiyo mechi 175 katika kipindi cha miaka 20, ambapo alitwaa taji la Dunia 2006 – na anaamini kuwa bado timu hiyo inaweza kufanya vizuri mbeleni.

Maofisa AAKIA Wafurahishwa Ulinzi JNIA

Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Lugano Mwansasu (kulia), akitoa maelezo kwa Maafisa wa Idara mbalimbali kutoka kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA) waliofanya ziara ya mafunzo. Kushoto ni Msaidizi wa Mkuu wa kitengo cha Ulinzi na usalama JNIA, Bw. Hamis Mashaka.

Na Mwandishi Wetu

MAOFISA kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA), wamefurahishwa na namna ulinzi na usalama wa abiria na mali zao unavyofanywa kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), imeelezwa.

Maofisa hao kutoka Idara mbalimbali walitoa kauli hiyo jana katika ziara ya siku moja ya mafunzo JNIA, ambapo walitembelea maeneo mbalimbali na kupata maelezo ya kina kutoka kwa maofisa husika.

                    Maofisa wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA), Bw. Shaaban Kombo (kuanzia wa pili kulia), Bi. Zakhia Mohamed, Bw. Salehe Said na Bi. Fatma Yussuf wakimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Lugano Mwansasu (kulia) akiwaelekeza jambo wakati wa ziara yao ya mafunzo iliyofanyika leo.

Mkuu wa msafara wa maofisa hao, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha AAKIA, Bw. Shaaban Kombo alisema pamoja na kupata mambo mengi ya msingi ya uendeshaji wa viwanja vya ndege, pia wamejifunza namna abiria na mizigo anavyokaguliwa kwa kutumia mitambo ya kisasa kabla ya kupanda ndege.

Bw. Kombo alisema JNIA imekuwa darasa tosha, ambapo pia katika upande wa utoaji wa vitambulisho wamejifunza namna utoaji wa vitambulisho unavyofanyika, ambapo AAKIA hutoa vitambulisho vya kudumu mara utaratibu wa muombaji utakapokamilika, tofauti na JNIA muombaji anaweza kupewa kitambulisho cha muda na kuendelea kufanyakazi huku cha kudumu kikiwa katika matengenezo.

Msaidizi wa Mkuu wa kitengo cha Ulinzi na usalama wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Hamis Mashaka (kushoto), akitoa maelezo mbalimbali yanayohusiana na ulinzi na usalama kwa maofisa kutoka idara mbalimbali za Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA) cha Zanzibar walipofanya ziara ya mafunzo leo.

“Tumefaidika na mambo mengi ukiangalia sisi kwetu hii ya vitambulisho ni tofauti kabisa, ila kwetu kwa kipindi chote mteja anasubiri kitambulisho cha kudumu anakuwa hawezi kuendelea na kazi zake eneo la kiwanja hadi atakapopata cha kudumu, lakini hapa anakuwa na cha muda kinachomfanya aendelee na shughuli zake huku cha kudumu kikiwa katika matengenezo,” alisema Bw. Kombo.

Naye Mkuu wa kitengpo cha Ulinzi na Usalama cha JNIA, Bw. Lugano Mwansasu alisema ziara ya maofisa wa AAKIA imewafariji na kuanza ukurasa wa mahusiano katika ushirikiano, ambapo nao wamejifunza kulingana na maelezo ya uendeshaji wa AAKIA.

 Meneja Uendeshaji  cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Vedastus Fabian (kulia) akiwapa maelezo mbalimbali Maofisa kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA) walipofanya ziara ya mafunzo leo.

Bw. Lugano alitoa wito kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuiga mfano huo wa kupeleka maofisa wake kwenye viwanja mbalimbali vya nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza utendaji kwa lengo la kuboresha huduma za viwanja kwa ujumla. TAA inasimamia viwanja 58 vilivyopo chini ya serikali.

“Kila siku mambo ya uendeshaji yanabadilika, basi tunaiomba mamlaka yetu itusaidie na sisi kwenda kutembelea viwanja vya wenzetu tujifunze huko, zipo changamoto labda sisi hatujui zinatatuliwaje lakini kwa ziara za mafunzo tunaweza kupata mbinu kutoka kwa wenzetu,” alisema Bw. Lugano.

Ofisa Habari katika jengo la Watu Mashuhuri la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (VIP-JNIA), Bw. Kenny Kwenga (kushoto) akitoa maelezo ya namna watu mashuhuri wanavyohudumiwa na maofisa kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA), walipofanya ziara jana. Kulia ni Msimamizi wa VIP, Bi. Josephine Mwaisukule.

Katika hatua nyingine, Meneja Uendeshaji wa JNIA, Bw. Vedastus Fabian alisema faida ya ziara ya mafunzo ni kujijengea uwezo na mahusiano mazuri baina ya kiwanja kimoja na kingine.

Bw.Fabian alisema ziara hizo zinasaidia katika kutatua matatizo yanayovikumba viwanja vya ndege, ambapo kwa sasa kumekuwa na masuala ya ugaidi, uvushaji wa dawa za kulevia na nyara za serikali.

Saturday, 11 November 2017

Nyota Kibao Kushiriki Tamasha la Karatu 2017

Na Mwandishi Wetu

NYOTA kibao wa riadha wanatarajia kushiriki mbio za kilometa 10 na zile za kilometa tano za wanawake na wanaume zitakazofanyika Desemba 23 mjini Karatu.

Mbio hizo pamoja na michezo mingine kama ya baiskeli, mpira wa wavu, soka, ngoma na kwaya zitakuwa ni hitimisho la Tamasha la Michezo la Karatu 2017.

Kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo Meta Petro, mbio za mwaka huu zinatarajia kushirikisha wanariadha kibao nyota kutoka sehemu mbalimbali nchini.

Alisema baadhi ya wanariadha hao watatoka katika taasisi za kijeshi, huku wengine wakitoka katika klabu za uraiani na sehemu mbalimbali katika mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Kilimanjaro na Dar es Salaam.

Filbert Bayi

Tamasha hilo ambalo linaendeshwa na Filbert Bayi Foundation (FBF) lilianza zaidi ya miaka 10 iliyopita na linafanyika Desemba ya kila mwaka.

Kwa mujibu wa Petro, tamasha hilo hasa mchezo wa mbio limekuwa na lengo la kuibua na kuuendeleza vipaji vya chipukizi ili kuwapata nyota wapya watakaochukua nafasi ya Bayi aliyewahi kuwa bingwa wa dunia wa mbio za meta 1500.

Mbali na meta 1500, Bayi pia aliwahi kutamba na kushikilia rekodi ya dunia ya mbio za maili moja na kutwaa medali ya fedha katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Moscow, Urusi mwaka 1980.

Bayi ni mwenyeji wa Karatu mkoani Arusha na aliamua kuanzisha mbio hizo ili kupata vipaji vipya vitakavyomrithi yeye katika mchezo huo.


Meta Petro

Mbali na mbio za kilometa 10 na zile za tano, pia kutakuwa na mbio za watoto ambazo zitakuwa za kilometa 2.5.

Friday, 10 November 2017

Chaneta Yaishusha Daraja Timu ya Simiyu

Na Mwandishi Wetu

WAKATI kinyang’anyiro cha netiboli za Ligi Daraja la Pili Taifa kikiendelea kutimua vumbi, timu ya Simiyu kutoka mkoani humo, imeshushwa daraja baada ya kushindwa kushiriki mashidano hayo.

Mashindano hayo ya kuwania kupanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza Taifa, yanaendelea kwenye viwanja vya Jakaya Kikwete Youth Park, ambapo timu saba zitapanda na kucheza Ligi Daraja la Kwanza Taifa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) Judith Ilunda amesema kuwa, timu ya Simiyu itashushwa daraja na kutakiwa kulipa sh 500,000 baada ya kuthibitisha kushiriki, lakini imeshindwa kutokea.

“Jana (juzi) tuliongea na kiongozi mmoja wa Simiyu alisema wako njiani wanakuja katika mashindano, lakini leo (jana) akathibitisha kuwa hawaji tena, watashushwa daraja na kutakiwa kulipa sh 500,000, “anasema Ilunda.

Anasema kuwa mashindano hayo yanaendelea vizuri na timu 11 kutoka mikoa sita Tanzania bara zinachuana kuwania nafasi saba za kupanda daraja.

Katika mechi za jana; timu ya Pamoja Youth iliichakaza Zimamoto kwa kuichapa mabao 55-27 wakati Magereza ya Morogoro iliibuka na ushindi wa magoli 53-28.

Katika mechi za juzi kwenye uwanja huo, Magereza Moro ilitamba kwa kuifunga Chem Chem kwa mabao 49-11, wakati Bandari Dar ikiichapa Sedico kwa mabao 49-30, Coca Cola waliilowesha Zima Moto kwa 43-31.


Hayo ni mashindano ya kwanza kufanyika chini ya uongozi mpya wa Chaneta ulioingia madarakani Septemba 30 mwaka huu mjini Dodoma.


DStv Kuonesha Tuzo za AFRIMA 2017

Na Mwandishi Wetu

WATEJA wa DStv wamepata nafasi ya kushuhudia Tuzo kubwa Afrika zinazotoa heshima na kutambua mchango wa wasanii kutoka Afrika,  kimataifa.

Ni Tuzo za AFRIMA (The All Africa Union Music Award Channel), ambazo zinatarajiwa kufanyika Jumapili hii na DStv imekuletea chaneli maalum kwa ajili ya kuonesha matukio yote muhimu na utoaji wa Tuzo hizi.

 Chaneli hii imeanza  kuanekana kuanzia Novemba 9 na inapatikana kwa wateja wote wa DStv kupitia namba 198 iliyopo kuanzia kifurushi Bomba cha sh.19,000 tu. Kwa kipindi cha siku tatu mfululizo,  wateja wa DStv watafurahia burudani kadha wa kadha kutoka kwa wasanii waliochaguliwa kwenye Tuzo hizi ikiwemo matamasha mbali mbali ya ndani na nje ya Bara  la Afrika kutoka kwa wasanii hawa.

Ni wakati wa watanzania  kushuhudia wasanii wetu wakipokea Tuzo zao za kimataifa  LIVE kupitia DStv pekee, Lipia Kifurushi chako cha DStv sasa kuanzia kifurushi Bomba kwa sh.19,000, ili usipitwe na Tuzo hizi.

 Majina ya wasanii kutoka Tanzania na vipengele walivyochaguliwa ni:

 Best Female Artist in Eastern Africa

Lady Jaydee – Sawa na Wao

Nandy- One Day

Feza Kessy - Walete

Vanessa Mdee- Cash Madame

 Best Male Artist in Eastern Africa

Ali Kiba – Aje

Diamond Platnumz – Eneka

 African Fans Favorite

Darassa- Muziki

 Best African Collaboration

Ali Kiba ft. MI – Aje

 Best Artiste/ Group in African Contemporary

Ali Kiba ft. MI – Aje

 Best Artist in African Pop

Diamond Platnumz- Eneka

 

Best Artist / Group in African R n B & Soul


Ali Kiba – Aje

Nchi Nane Zathibitisha Kushiriki Kili International Airport Marathon 2017, Usajili Kuanza Jumatatu

Mkurugenzi wa Kilimanjaro International Airport Marathon 2017, Amin Kimaro akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu

NCHI nane zimethibitisha kushiriki katika mbio za Kilimanjaro International Aiport Marathon zitakazofanyika Novemba 19 mwaka huu mjini Moshi.

Tayari zaidi ya wanariadha 2000 wamethibitisha kushiriki katika mbio hizo, ambazo ni za kwanza kufanyika nchini na zenye lengo la kuinua utalii wakati wa kipindi cha msimu wa watalii wachache.

Mkurugenzi wa mbio hizo, Amin Kimaro alizitaja nchi za India, Japan, Uholanzi, Sudan Kusini, Ufaransa, Canada, Taiwan na Kenya ndizo zilizothibitisha kushiriki katika mashindano hayo, huku akitarajia nzhi zaidi kujitokeza.

Kimaro anasema kuwa wanatarajia zaidi ya wanariadha 3,000 kushiriki mbio hizo zenye kauli mbinu ya ‘Utalii Unaanzi KIA’.

Anasema kuwa usajili wa katika mtandao ulianza Novemba Mosi wakati ule wa kawaida utaanza kufanyika Jumatatu Novemba 13 katika vituo vya Arusha, Moshi na Boma Ng’ombe.

Akifafanua kuhusu vituo hivyo, Kimaro anasema kuwa mkoa Arusha, usajili utafanyikia katika hoteli ya Mount Meru na Kibo Homes wakati Moshi katika Chuo cha Ushirika na Boma utakuwa Snow View Hotel, KIA na Meku Hotel.


Anasema kuwa wale wote waliofanya usajili mtandaoni, namba zao wanatakiwa kwenda kuzichukua kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) tayari kwa mbio hizo.

Washindi wa mbi hizo watapata zawadi kubwa kuwahi kutolewea hapa nchini katika mbio zote, ambapo mshindi wa kwanza wa kilometa 42 (Full Marathon) ataondoka na kitita cha sh milioni 5 wakati mshindi wa kwanza wa kilometa 21 au nusu marathon, atapata sh milioni 4.

Mbali na zawadi hizo pia takutakuwa na zawadu zingine kibao za fedha taslimu pamoja na medali, fulana na zawadi zingine kibao.

Sunday, 5 November 2017

Arsenal yapokea kichapo cha 3-1 kutoka kwa City

Mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero (kushoto) akishangilia bao na mchezaji mwenzake baada yakufunga kwa penalti katika mchezo wa Ligi kuu ya England dhidi ya Arsenal leo kwenye Uwanja wa Etihad mjini Manchester, kaskazini magjaribi ya England. Man City imeshinda mabao 3-1. (Picha na AFP).


Wydad mabingwa wapya Ligi ya Mabingwa Afrika

CASABLANCA, Morocco

TIMU ya Wydad Casablanca (pichani) imetwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya kuifunga timu ngumu ya Al Ahly kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Stade Mohamed V Stadium mjini hapa.

Wydad imetwaa taji hilo baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 2-1 kufuatia timu hizo kutoka sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Misri wiki iliyopita.

Mchezo huo wa pili wa fainali ulimuliwa kwa bao la Walid El Karti katikati ya kipindi cha pili, wakati timu hiyo ya Morocco ikitwaa taji lake la pili la Afrika tangu mwaka 1992.

Al Ahly walionekana kuwa hatari zaidi katika dakika 20 za mwanzo na walipata nafasi nzuri ya kufunga mwanzoni mwa mchezo wakati Abdallah El-Said, alipomjaribu kipa wa Wydad Zouhair Laaroubi.

Wydad walipambana na kujaribu kuweka pamoja mashambulizi yao na katika dakika ya 30, mshambuliaji Abdeladim Khadrouf nusura afunge baada ya shuti lake mgonga beki na kugonga mwamba.


Ahly baada ya dakika kadhaa walikosa bao baada ya kufanya shambulizi la nguvu, ambapo Moemen Zakareya alipata nafasi nzuri lakini iliokolewa na Laaroubi.

Friday, 3 November 2017

Naibu Waziri aridhishwa na maendeleo ya ujenzi TB III

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imesema ukusanyaji wa mapato unaofanywa kwa sasa ni muhimu kwani unaweza kuifanikisha Tanzania kuwa na uwezo wa kujenga miradi mikubwa kwa kutumia fedha za ndani.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya Ujenzi), Elias Kwandikwa wakati alipotembea leo mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria au Terminal III la Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Alisema serikali inajenga awamu ya pili ya mradi huo kwa kutumia fedha za ndani, ishara ambayo ni nzuri, kwani inaonesha kuwa katika siku za mbele serikali itakuwa na uwezo wa kujenga miradi kwa kutumia fedha zake.

“Tunajenga mradi huu kwa fedha zetu za ndani, lakini pia kwa kushirikiana na wdau wengine, hii ni ishara nzuri kwamba sasa tunakokwenda tunao uwezo katika siku za usoni kuwa na miradi kama hii kwa fedha zetu,” alisema Kwandikwa.

Alisema kwa sasa hatua ya ujenzi wa mradi huo imefikia asilimia 66 na kwamba utakamilika Septemba mwakani na kwamba baada ya ujenzi huo kukamilika itakuwa ni picha ya kuelekea kwenye Tanzania mpya.

Kwandikwa alisema mkandarasi wa mradi huo, kampuni ya Bam International imelipwa fedha zake na kwamba wizara inahakikisha mkandarasi huyo anapata haki yake kwa wakati.

“Nilitembelea kule KIA (Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro), nikaona maendeleo ya ujenzi kule na nikaridhishwa, nikatamani nije hapa, lakini nimefika hapa pia nimeridhishwa na kasi ya ujenzi unaoendelea,” alisema.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi huo, Barton Komba alisema, mkandarasi wa ujenzi huo ameshalipwa fedha zake zote, hivyo kwa sasa hadai serikali na anafanya kazi yake vizuri.


“Mpaka mwezi wa tisa mwakani utakuwa umekamilika, lakini pia uwanja huu umezingatia watu wote hata ndugu zetu wenye mahitaji maalumu, n uwanja uliozingatia viwango vya kimataifa,” alisema Komba.