Saturday, 15 July 2017

Taifa Stars yajiweka pabaya Chan 2018 Nairobi



Na Mwandishi Wetu, Mwanza
KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Salum Mayanga amesema kuwa timu yake imeshindwa kuibuka na ushindi katika mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (Chan) kwa wachezaji wa nyumbani baada ya kufungwa bao la mapema na Rwanda kwenye Uwanja wa CCM Kirumba hapa.

Taifa Stars ilifungwa bao katika dakika ya 17 na kuwa na kibarua cha kutafuta bao la kusawazisha, ambalo walilipata kwa penalti.

Mayanga aliyasema hayo baada ya mchezo huo was are ya kufungana bao 1-1 na timu yake kujiweka katika nafasingumu ya kusonga mbele katika mashindano hayo. Bao la wageni lilipachikwa na Dominique Nshuti.

Kukosa utulivu ni jambo jingine ambalo limechangia Taifa Stars kushindwa kupata matokeo ya ushindi. Mayanga alisema kuwa wapinzani wao walitumia mbinu ya kupoteza muda ili kupata matokeo ya sare.


Naye kocha wa Rwanda alisema kuwa wanajipanga kqa ajili ya mchezo wa marudiano kwani mchezo huo bado haujamalizika lakini alisema timu ya Tanzania sio timu ya kuibeza kwani iko vizuri.

Matokeo hayo yanamaanisha Taifa Stars italazimika kwenda kushinda ugenini mjini Kigali Julai 22 ili kusonga mbele katika kuwania tiketi ya CHAN mwakani nchini Kenya, ambako itamenyana na mshindi kati ya Sudan Kusini na Uganda zilizotoa sare ya 0-0 pia jana mjini Juba.

Vijana wa Madola waondoka na matumaini kibao

Wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 pamoja na viongozi wa Kamati ya Olimpiki (TOC) kabla timu hiyo haijapanda ndege kwenda Bahamas leo jioni.
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 imeondoka leo nchini kwenda Nassau, Bahamas ikitamba kuwa itafanya vizuri katika michezo hiyo itakayoanza kutimua `vumbi' Jumatano Julai 19.

Tanzania katika michezo hiyo ya sita ya Jumuiya ya Madola kwa wachezaji wa umri chini ya miaka hiyo imepeleka wachezaji wanne tu, wawili wawili wa mchezo wa riadha, Mwinga Mwanjala  na kuogelea, Amir Twalib Abdullah, ambao walitamba timu zao kufanya vizuri katika michezo hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), makocha hao walisema kuwa timu zao zitafanya vizuri kwani wamejiandaa kwenda kushindana na sio kushiriki.

Mwanjala ambaye wachezaji wake ni Regina Mpigachai na Francis Damiano watakaoshiriki mbio za meta  800 na 3,000.wakati waogeleaji ni  Celina Itatiro na Colin Saiboki, ambao watashiriki katika michezo ya aina tofauti tofauti.

Wachezaji hai nao walisema watafanya vizuri katika michezo hiyo kwani wamefanya mazoezi kwa muda mrefu.

Timu hiyo imeondoka leo kwa ndege ya Emirates kupitia Dubai na wanatarajia kurudi nchini Julai 24 siku moja baada ya michezo hiyo kufungwa rasmi Julai 23.
Timu hiyo iliagwa rasmi juzi katika ofisi za Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na Rais wa TOC Giulam Rashid, ambapo walitakiwa kwenda kupambana ili kuliletea sifa taifa kwa kufanya vizuri mkatika michezo hiyo.

Makamu wa Rais wa TOC Henry Tandau aliwataka wachezaji hao kuondoa uoga na kwenda kushindana katika mashindano hayo na sio kuogopa chochote kwani wanatakiwa kujiamini.
Nahodha wa timu hiyo, Mpigachai alisema kuwa wamejiandaa vizuri na wanajiamini watafanya vizuri katika mashindano hayo, ambapo amewataka Watanzania kuwaombea.
Nahodha wa timu ya Tanzania, Regina Mpigachai akizungumza baada ya kukabidhiwa bendera katika ofisi za TOC jijini Dar es Salaam juzi.
Kwenye Uwanja wa Ndege, timu hiyo ilisindikizwa na Makamu wa Rais wa TOC, Henry Tandau, Katibu Mkuu Filbert Bayi, mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya TOC, Peter Mwita na Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday na mjumbe wa RT, Tullo Chambo na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali.
Kocha wa timu ya taifa ya riadha na Mkuu wa Msafara wa timu ya Jumuiya ya Madola ya Vijana, Mwinga Mwanjala akizungumza baada ya timu hiyo kukabidhiwa bendera.


Ziara ya Waziri Mbarawa Kiwanja cha ndege JNIA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (kulia) akifurahia jambo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Phillip Mpango (kushoto)  na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba na Katibu Mkuu  sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho (mwenye mkoba mweusi) leo walipokutana kwenye Jengo la Watu Mashuhuri la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
Katibu Mkuu wa Chama cha Madereva wa Taxi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Simon Mwampashi (kulia), akitoa maoni mbalimbali kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa alipofanya ziara JNIA.
  1. Mkuu wa Kitengo cha Idara ya Uhamiaji Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Bw. Flugence Andrew (kulia) akitoa maelezo ya utaratibu unaotumika kulipia viza kwa Mhe. Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano leo alipofanya ziara kwenye jengo la abiria la kiwanja hicho. 
Ofisa wa Benki ya NMB, Leah Rutayungurwa  (aliyendani ya dirisha) leo akimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof Makame Mbarawa aliyetaka kujua muda anaohudumiwa abiria mmoja wakati akilipia viza kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (TBII-JNIA).
Ofisa Forodha Msaidizi, Hezron Giso (kulia), akielezea shughuli anazozifanya ndani ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (TBII-JNIA), kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (mwenye miwani kifuani), wakati wa ziara ya Waziri iliyofanyika leo.
Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (TBII-JNIA), mwenye kizibao akielezea jambo katika meza ya ukaguzi wa tiketi za abiria wanaosafiri. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),  Salim Msangi.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akiwa katika mfumo wa kupokelea mizigo kwa abiria wanaowasili kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere alipofanya ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali. Mwenye kizibao ni Kaimu Mkurugenzi wa kiwanja hicho, Joseph Nyahende.

Hotuba ya mgeni rasmi Injinia Ndigilo wakati akifunga mafunzo ya makocha wa riadha

 
Wakufunzi wa Kimataifa, Tagara Tendai na Charles Mukiibi (waliofunikwa vitenge) katika picha ya pamoja baada ya kukabidhiwa zawadi na washiriki wa mafunzo ya ufundishaji riadha kwa watoto wenye umri chini ya miaka 16 yaliyofanyika katika Kituo cha Michezo cha Filbert Bayi Kibaha mkoani Pwani.
Rais, Kamati ya Olimpiki Tanzania,Ndugu Gulam Rashid,

Makamu wa Rais, Kamati ya Olimpiki Tanzania, Ndugu Henry Tandau

Katibu Mkuu, Kamati ya Olimpiki Tanzania, Ndugu Filbert Bayi,

Katibu Mkuu, Riadha Tanzania, Ndugu Wilhelm Gidabuday

Mwakilishi, Chama cha Riadha Zanzibar

Wakufunzi wa Kimataifa, Ndugu Tagara Tendai na Charles Mukiibi

Waratibu wa Mafunzo, Ndugu Irene Mwasanga (TOC) na Robert Kalyahe (RT)

Washiriki wa Mafunzo,

Wageni waalikwa,

Mabibi na Mabwana.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Injinia Evarist Ndigilo (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau.
Napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru ofisi ya TOC kwa kunipa heshima hii ya kuwa mgeni rasmi katika kufunga mafunzo haya ya walimu wa mchezo wa Riadha daraja la 1.

Nimefahamishwa kwamba mafunzo haya yalifunguliwa siku 11 zilizopita na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Harrison George Mwakyembe. Ni matumaini yangu kuwa mmepata dozi nzuri ya taaluma na mbinu mbalimbali ya kufundisha mchezo huu. TOC inauthamini sana  mchezo wa Riadha, kwani ni kati ya michezo ambayo imeiletea heshima Taifa Taifa letu katika Michezo ya Kimataifa kama Jumuiya ya Madola, Afrika.

Siwezi kuzungumzia Olimpiki kwani  nimefahamishwa tangu tuanze kushiriki Olimpiki mwaka 1964 mjini Tokyo, Tanzania imewahi kupata medali mbili za fedha kupitia Filbert  Bayi (        Mita 3000 kuruka Magongo) na Suleiman Nyambui (Mita 5000).
 
Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Pwani Everist Ndigilo (kushoto) akimkabidhi cheti mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ya takribani wiki mbili, Suleiman Ame ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Zanzibar (ZAAA) wakati wa hafla hiyo.
Sote tunakumbuka mwaka 2016 wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Rio, Mtanzania Alphonce Felix Simbu pamoja na kuwa mshindi wa 5 katika mbio za Marathon aliweza kuitoa Tanzania kimasomaso kwa nafasi ambayo kwa mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1992 mjini Barcelona wakati mkimbiaji wa Tanzania Kanali Mstaafu Juma Ikangaa alipokuwa wa sita (6) katika mbio za Marathon.

Kama nilivyofahamishwa haya  ni mafunzo ya nne kufanyika kwa walimu wetu hapa Tanzania. Mafunzo ya awali yalifanyika mjini Dar Es Salaam mwaka 1991, mjini Dodoma mwaka 2004 na mwaka 2010 mjini Dar Es Salaam na mwaka huu 2017 hapa Mkuza, Kibaha. Mafunzo yote yakifadhiliwa na Olimpiki Solidariti (OS) kupitia Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).

Pia naamini mmefaidika na elimu mliopata kutoka kwa wataalamu wa Kimataifa ambao wamekuwa wakiwaandalia masomo yote ya nadharia na vitendo kwa muda wote wa siku 11. Ni mategemeo yangu elimu mliyopata itawasaidia kuandaa timu zenu na kutambua vipaji vipya katika maeneo mnayotoka. Ni ukweli usiopingika kwamba mmejiongezea elimu ya kufundisha mchezo huu wa riadha kwa kiwango cha hali ya juu, mkilinganisha uwezo na elimu mliyokuwa nayo awali.

Wakati wote TOC imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza taaluma ya ufundishaji na mbinu za kisasa za kuboresha uwezo wa walimu wetu, ili wachezaji wetu waweze kufikia viwango vinavyotakiwa na timu zetu zinaposhindana katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa.

Hivi karibuni tumesikia wanariadha wetu wakifanya vizuri katika mashindano ya Kimataifa baada ya Alphonce Felix Simbu kufungua milango ya ufanisi kwa kuwa wa tano (5) kwenye mbio za masafa marefu (Marathon) wakati wa Olimpiki ya Rio 2016.

Baada ya mafanikio hayo ya Simbu, kumekuwa na misafara ya wanariadha wetu kushindana nchi mbalimbali duniani aidha kuongeza mapato au kufikia viwango vya kushiriki mashindano makubwa ya Dunia yanayofanyika Augusti, 2017.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Ndigilo akimkabidhi cheti, Meta Petro wa Karatu wakati wa hafla hiyo ya kukabidhi vyeti kwa washiriki hao Kibaha.
Mara kwa mara tumesikia katika mafunzo yaliyopita walimu wengi wanapohitimu wanakimbilia kufundisha tu michezo ya kukimbia  hususan mbio za masafa marefu (Marathon) na ndefu (5000/10000) na kusahau michezo mingine, riadha siyo kukimbia tu, kuna mbio fupi (sprints) kati, (middle distance) kuruka (kuruka chini, miruko mitatu, kuruka juu na upondo) na kurusha (mkuki, kisahani, tufe na nyundo).

Ningependa kusisitizia sana kwenu walimu mnaomaliza mafunzo haya, kwamba  mhakikishe mchezo huu wa riadha  unapiga hatua katika maeneo yote na kufikia viwango vya miaka ya 70.

Tanzania haina tofauti na jirani zetu Kenya ambao wamekuwa tishio katika mchezo wa riadha duniani.

Ningependa kuwasihi walimu mnaomaliza mafunzo haya leo kuupeleka mchezo huu mashuleni walipo vijana wengi wenye vipaji vingi ambao wanafundishika na rahisi kuelewa. Inahitajika mipango mahususi ya mazoezi na mashindano ambayo nina imani Chama cha Riadha Taifa inayo.

Nyie wachache mliohudhuria hapa muwe mabalozi wa kupeleka elimu hii kwa wale ambao nao wangependa kuwa hapa, lakini kutokana na nafasi ndogo ya washiriki kwa maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) hawakuweza kushiriki.

Kumekwepo na mapungufu ya walimu wa michezo mbalimbali hasa riadha wakati wa maandalizi ya Umisseta na Umitashumta. Ninaowaomba kwa kuwa mmetoka karibu kila Mkoa wa nchi yetu (Tanzania Bara/Zanzibar) muwasaidie walimu hao kabla na mara maandalizi yanapoanza.

Napenda nichukue nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru Wataalamu wa Kimatafa kwa jitihada zao za kutoa mafunzo haya kwa ufanisi mkubwa, waratibu wa RT/ZAAA, TOC na Walimu washiriki kwani bila wao kuwepo hapa mafunzo haya yasingefanyika.

Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru Olimpiki Solidariti kwa kufadhili mafunzo haya, Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) kuwateua Wakufunzi wa kuendesha mafunzo, TOC na RT/ZAAA kwa maandalizi mazuri, mwisho wenyeji wenu katika Kituo hiki kwa mazingira mazuri na tulivu kwa mafunzo kama haya.

Mwisho kabisa nawashukuru wale wote waliohusika katika kufanikisha mafunzo haya kwa namna moja au nyingine.

Kwa haya machache sasa natamka kwamba mafunzo yenu ya ualimu wa mchezo wa Riadha ninayafunga rasmi na niko tayari kutoa vyeti mbalimbali.


Ahsanteni kwa kunisikiliza.



Tuesday, 4 July 2017

Taifa Stars v Zambia mubashara nusu fainali Cosafa

Na Mwandishi Wetu
KAMA ilivyo ada, King’amuzi cha DStv kitaonyesha mubashara mechi inayosubiriwa kwa hamu kubwa kati ya Tanzania na Zambia ikiwa ni nusu fainali ya michuano ya COSAFA 2017 itakayochezwa kesho Jumatano saa 12 jioni huko Afrika Kusini

Taifa stars imefuzu nusu fainali baada ya shughuli pevu ya kuwafunga wenyeji Africa Kusini (Bafana Bafana) na sasa itakumbana na moja ya miamba ya soka barani Afrika Zambia katika nusu fainali inayotarajiwa kuwa na upinzania mkali.

Meneja Masoko wa Multichoice Tanzania Alpha Mria amethibitisha kuwa mechi hiyo itarushwa mubashara kupitia DStv chaneli ya SuperSport4 ambayo inapatikana kwenye vifurushi vyote kikiwemo kile cha DStv Bomba ambacho hupatikana kwa Sh 19,975 tu.

“Kwanza kabisa tunawapongeza sana Taifa Stars, wamefanya kazi kubwa, wameleta matumaini makubwa, sasa kazi ni moja tu, kwenda fainiali na sisi DStv, tunawahakikishia wateja wetu na watanzania kwa ujumla kuwa mtanange huo watauona mubashara kupitia DStv” alisema Alpha.

Ameongeza kuwa enzi ya watanzania kusubiri matokeo ya michuano mikubwa kama hii ka saa kadhaa baada ya mechi kukamilika umepitwa na wakati, kwani kwa DStv, michuano hiyo huonyeshwa moja kwa moj. “Hakuna tena kwend amtandaoni kuangalia matokeo, wala kumuuliza mtu, ukiwa na DStv, unashuhudia mwenyewe” alisema.

Huduma za DStv zimekuwepo hapa Tanzania kwa miaka 20 sasa na maelfu kwa maelfu ya watanzania wameunganishiwa huduma za DStv na kuwafanya mamilioni ya watanzania katika kila pembe ya nchi kufurahia huduma zake. Mbali na kujikita Zaidi katika michezo na burudani, DStv pia ina chaneli mbalimbali za habari, Sanaa, Dini, Utafiri, Sayansi na Teknolojia, na pia utamaduni.


Monday, 3 July 2017

Serikali yavipa neno zito vyama vya michezo

Naibu waziri wa Habari, Utamaduni, sanaa na Michezo, Anastazia Wambura (katikati waliokaa) akiwa pamoja na washiriki na wakufunzi wa mafunzo ya ualimu wa Level 1 wa wachezaji wenye  umri aw miaka 16 iliyoanza leo katika Kituo cha Michezo cha Filbert Bayi Nkuza Kibaha.
Na Mwandishi Wetu, kibaha
SERIKALI imesema Tanzania inatakiwa kuanza mapema maandalizi ili kupata medali katika mashindano mbalimbali yajayo ya kimataifa.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Harrson Mwakyembe wakati akifungua mafunzo ya siku 13 ya makocha wa riadha ya hatua ya kwanza ya wachezaji wenye umri chini ya miaka 16 katika Kituo cha Michezo cha Filbert Bayi Mkuza, Kibaha mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura.
 Akizungumza kwa niaba ya Mwakyembe, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Anastazia Wambura alisema kuwa, vyama vya michezo lazima kuanza mapema maandalizi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ili kuiwezesha nchi kupata medali katika michezo ijayo.

Tanzania inatarajia kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Gold Coast, Australia 2018, ile ya Mataifa ya Afrika 2019 na Olimpiki itakayofanyika Tokyo, Japan 2020.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) akizunguza wakati wa mafunzo hayo.
Waziri alisema kuwa taifa lina vipaji vingi, lakini tatizo kubwa ni ufinyu wa maandalizii ya maana na kuhitaji makocha wenye uwezo mkubwa wenye uzoefu wa kimataifa ili kuwaandaa vizuri kisayansi wachezaji kwa ajili ya mashindano hayo.

Dk Mwakyembe alisema kuwa Tanzania inaweza kufanya maajabu katika mashindano ya kimataifa kutokana na vipaji vilivyopo katika michezo mbalimbali kama wachezaji wataandaliwa vizuri na mapema.
Makamu wa Rais wa TOC, Henry Tandau (kulia) na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura. Kulia kwa Waziri ni Makamu wa Pili wa Rais Riadha Tanzania (RT), Dk Hamad Ndee. 
 “Tunatakiwa kuwaandaa vizuri wanariadha wetu kwa ajili ya mashindano ya kimataifa kutoka kwa makocha wenye uzoefu mkubwa ambao watauwezesha kuupeleka mbele mchezo wetu huu wa riadha, “ alisema wakati akizungumza na washiriki kutoka zaidi ya mikoa 10 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

"Tuna mashindano makubwa mbele yetu, kama Jumuiya ya Madola 2018 Australia, Michezo ya Afrika 2019 Guinea ya Ikweta na ile ya Olimpiki mwaka 2020. “ alisema.

"Sasa tunatakiwa kuangalia mbele maandalizi ili kuweza kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, “alisema.
Mwakyembe alisema alibaini vipaji katika mashindano ya vijana ya wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 18 ya riadha iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam hivi karibuni wakati wanariadha chipukizi walipoonesha  uwezo wa hali ya juu.

Pia aliitaka Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kuratibu vizuri kozi hiyo kwa kushirikiana na vyama vya michezo vya Tanzania (RT) na kile cha Zanzibar (ZAAA) chini ya udhamini wa Mshikamano wa Olimpiki ((OS).

Mafunzo hayo yanashirikisha washiriki kutoka mikoa ya Mbeya, Singida, Mara, Kagera, Dar es Salaam, Zanzibar, Mwanza,Dodoma, Ruvuma, Arusha, Pwani, Simiyu, Iringa, Kilimanjaro, Njombe na Shinyanga.
Akizunumza mapewa mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo kutoka Uganda, Charles Mukiibi  alisema mafunzo hayo yanaleng katika kutoa ujuzi wa kufundisha watoto wenye umri chini ya miaka 16 na chini yake, wengi wao wakiwa ni wanafunzi wa shule za msingi, ambao wanalenga kuwa mabingwa wa baadae.

Makamu wa Rais wa Riadha Tanzania (RT), Dk Hamad Ndee alisema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwani yatasaidia kuongeza idadi ya makocha wa mchezo huo hapa nchini.
Aliwataka washiriki kutumia mafunzo hayo vizuri ili kuja kuwa makocha wazuri wa vijana.

"Tunaishukuru TOC kwa jitihada kubwa walizofanya hadi kutupatia mafunzo haya, ambayo yatatusaidia kuuendeleza mchezo huu hapa nchini, “alisema Katibu Mkuu wa ZAAA, Suleiman Ame wakati akitoa salama za shukrani kwa niaba ya washiriki wote.
Alisema kuwa mafunzo hayo yatasaidia mikoa kutoa wanariadha wengi chikupukizi ambao watafanya vizuri siku za usoni.

Naye katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi alisema kozi hiyo imeratbiwa na RT na ZAAA pamoja na TOC.

Bayi,ambaye ni gwiji wa zamani wa riadha Tanzania alisema kuwa vyana vya riadha vya mikoa haviko hai kutokana na ukosefu wa wanariadha chipukizi, ambao vipaji vyao haviendelezwi.
Alisema tayari TOC imeshatoa kozi 19 kwa viongozi wa vyama vya michezo vya kitaifa na makocha  katika harakati za kuendeleza michezo nchini.

Alisema ni jukumu la vyama vya michezo kuhakikisha mafunzo hayo yaliayoanza mwaka 2005, yatoa matunda.

Alisema kuwa TOC imekuwa ikifanya kazi bila kuchoka kuhakikisha Tanzania inatoa wakimbiaji watakaofanya vizuri katika mashindano mbalimbali.
Alisema kuwa Tanzania  inahitaji wanariadha chipukizi ikiwa nchi iliyopo katika 10 bora zilizoshiriki katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Rio de Janeiro 2016.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Makamu wa Rais wa TOC, Henry Tandau alisema ufinyu wa program za maendeleo kwa vyama vya michezo, masoko na udhamini ni miongoni mwa viti vinavyorudisha nyuma maendeleo ya michezo hapa nchini.


Vyama vya michezo vinatakiwa kuwa na program za uhakika na kuelekeza maandalizi yao katika mashindano makubwa badala ya kusubiri muda umekwisha ndio wafanye maandalizi ya zima moto.

Saturday, 1 July 2017

Mjomba Mpoto atangaza utalii wa ndani Saba Saba

Msanii mahiri wa mashairi, Mrisho Mpoto au Mjomba akizungumza katika banda la Hifadhi ya Ngorongoro katika Maonesho ya 41 ya Biashara ya Saba Saba jijini Dar es Salaam leo.
Na Mwandihsi Wetu
MRISHO Mpoto au Mjomba kama anavyojulikana sana na wapenzi wa sanaa nchini, leo alikuwa kivutio katika banda la Hifadhi ya Ngorongoro katika maonesho ya 41 ya Biashara ya Saba Saba jijini Dar es Salaam.

Mjomba anayetamba kwa uimbaji mashahiri alivuta watazamaji kibao katika banda hilo, ambalo ni sehemu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuvaa mfano wa mnyama tembo.
Mjomba akiwa na Stara Thomas katika banda la Hifadhi ya Ngorongoro leo.
`Sanamu’ hiyo aliyoivaa kuanzia shingoni ina mfano wa masikio makubwa na pembe kama za ndovu pamoja na mkonga wake, ambavyo vilikuwa kivutio kikubwa kwa watu wengi.

Mjomba pia alicheza ngoma za asili na baadae kuimba kibao chake cha Mjomba, akiongwa na bendi yake ya Mjomba iliyokuwa na wanamuziki kibao.

Wasanii wa Mjomba Band wakifanya vitu vyao leo.
Akizungumza katika viwanja hivyo, Mpoto alisema kuwa baadhi ya majukumu yake katika Ubalozi wa Ngorongoro ni kuelimisha na kuwahimiza Watanzania kufanya utalii wa ndani.

Alisema kila siku atakuwa katika banda hilo la Ngorongoro kutoa elimu na kuwashawishi watu kujua faida za utalii wa ndani na kutembelea vivutio.
Mjomba alivitaja baadhi ya vivutio hivyo katika Bonde la Ngorongoro ni pamoja na mchanga unaotembea, watu kuishi na wanyama wakali, nyayo za mtu anayesemekana ni wa zamani kabisa duniani.

Alisema ni aibu kubwa kuona watu kutoka nje ya Tanzania waijua Ngorongoro na vivutio vyake, kuliko Watanzania wenye nchi yao.
Naibu Muhifadhi wa Ngorongoro, Asangue Bangu (kushoto) akihojiwa na Mtangazaji Pascal Mayala katika banda hilo la Ngorongoro leo jijini Dar es Salaam.
Naye naibu mhifadhi wa Bonde la Ngorongoro, Asangue Bagu alisema Mpoto atawasaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utalii wa ndani.