Friday 15 November 2019

Mchezo Mpya wa Teq Ball Wazinduliwa Rasmi Nchini

Makamu wa Rais na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau (kushoto) na Filbert Bayi (kulia) wakiwa na Mkuu wa Uhusiano wa Kimataifa FITEQ, Marius Vizer Jr kabla ya uzinduzi wa mchezo huo Kibaha jana.

Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MCHEZO mpya ujulikanao kama Teq Ball umetambulishwa rasmi Tanzania, ikiwa ni nchi ya kwanza katika Kanda ya Tano ya Afrika, imeelezwa.

Mchezo huo ulitambulishwa rasmi juzi katika Kituo cha Michezo cha Filbert kilichopo Mkuza Kibaha mkoani Pwani na wawakilishi wa Shirikisho la Kimataifa la Teq Ball (FITEQ), viongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), na viongozi wa kituo hicho pamoja na wanafunzi.

FITEQ imetoa meza tatu na mipira 12, ambapo mbili zitakuwa katika Kituo cha Olimpafrica, ambacho kinatumia vifaa vilivyopo katika Kituo cha Michezo cha Filbert Bayi mjini hapa.
Kwa Tanzania, meza mbili, moja ya TOC zitakuwa katika Kituo cha muda cha Olimpafrica kilichoko FBS Mkuza, nyingine Dole Zanzibar. Meza ya Zanzibar ilitarajia kukabidhiwa jana kisiwani humo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Uhusiano wa Kimataifa FITEQ, Marius Vizer Jr, alisema shirikisho hilo makao yake makuu yako Hungary na sasa wako kwenye mikakati ya kuusambaza zaidi Duniani, baada ya kupata usajili wa kimataifa mwaka 2017.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule za Filbert Bayi, Fibert Bayi akizungumza wakati wa uzinduzi wa mchezo wa Teq Ball uliofanyika Mkuza, Kibaha jana.
Vizer Jr, alisema katika mikakati hiyo, mwaka huu wameingia mkataba na Kamati za Kitaifa za Olimpiki Afrika (ANOCAs), kuusambaza mchezo huo katika mashirikisho 40.
Hadi sasa nchi 14 tayari zimefikiwa na mchezo huo.

Alisema FITEQ itatoa Euro 6,000 (sawa na Sh 15,276,600) kwa mwaka kwa shirikisho la nchi husika kwa ajili ya uendeshaji, sambamba na kuendesha mafunzo kwa makocha na waamuzi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki Tanzania, TOC, Henry Tandau akipeana mkono na Mkuu wa Uhusiano wa Kimataifa FITEQ, Marius Vizer Jr wakati wa makabidhiano ya meza za mchezo huo Kibaha, Pwani jana. Kushoto ni Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi.
Naye Makamu wa Rais Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau, aliishukuru FITEQ na kusema kuwa historia imeandikwa kwa kuutambulisha mchezo huo.

Tandau, alisema wataitumia fursa hiyo kuhamasisha mchezo huo kwa kuundwa chama cha kitaifa, kuusambaza mikoani, kisha mashindano ya ngazi mbalimbali ili baadae uweze kuwa mchezo mkubwa nchini.
Alisema watajitahidi Tanzania ipate kuwa mwenyeji wa kwanza wa Fainali za Afrika za mchezo huo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shule za Filbert Bayi (FBS), Filbert Bayi, mbali na kushukuru alisema watautendea haki msaada huo kwa kuhakikisha unachezwa na kuundwa timu mbalimbali.

Mchezo huo ni mchanganyiko wa Mpira wa Meza na Mpira wa Miguu, ambapo huhesabiwa kwa pointi zifikapo 20 kwa utofauti wa pointi mbili.
Huchezwa kwa mchezaji moja moja au wawili wawili, ukitumia meza iliyopinda, mpira kama wa miguu na viungo vya mwili miguu, kifua, mabega na kichwa, isipoluwa mikono hairuhisiwi.

Mchezaji hatakiwi kutumia kiungo kimoja mara mbili, pia kuugusa mpira zaidi ya mara tatu.
Mkurugenzi wa Shule za Filbert Bayi, Anna Bayi (kulia) akipiga mpira kwa kichwa wakati akicheza mchezo wa Teq Ball Kibaha mkoani Pwani jana. Kulia ni Makamu wa Rais na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau (kulia mbele) na Filbert Bayi. 
Na kabla ya uzinduzi wakufunzi wa mchezo huo kutoka hungary, Gondos Zoltan na Vasas Lea walionesha umahiri mkubwa wa kuucheza mchezo huo kwa kumiliki mpira na kuupiga kwa kutumia kichwa, mabega, miguu, magoti na viungo vingine isipokuwa mikono.
Mchezo huu uliasisiwa mwaka 2013 na umewahi kuchezwa na wanasoka maarufu Duniani kama akina Luis Figo na Ronaldihno Gaucho ambaye pia ndiye Balozi wa mchezo huo.

No comments:

Post a Comment