Friday 16 August 2019

Mabalozi Tanzania Nje Wamwagia Sifa Terminal 3

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Julius Ndyamukama akitoa maelezo kwa mabalozi wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi wakati walipotembelea Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam leo. Kulia kwa Ndyamukama ni Mtendaji Mkuu wa Tanroad, Patrick Mfugale. 

Na Mwandishi Wetu
MABALOZI 42 wanaowakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani wamelimwagia sifa Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA).

Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Wilbroad Slaa akizungumza kwa niaba ya wenzake baada ya kutembelea jengo hilo jana, alisema jengo hilo ni kioo cha nchi  na ndipo wageni wengi wa nje ya nchi ndio wanafikia, ni kivutio kizuri.

 “Hapa (JNIA) ni kioo cha nchi. Tukiharibu mambo kwa kutoweka kaunta nzuri, tunaharibu taswira ya nchi. Hii ndiyo Dubai (Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) yetu. Lazima izingatie viwango vya kimataifa, “alisema Slaa huku akisisitiza kutoogopa kujifunza kutoka nje.

Komba akiwaonesha mabalozi wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi walipotembelea Jengo la Tatu la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Alaa alitakiwa kutoa shukrani kwa niaba ya wenzake na Mkuu wa Msafara huo wa mabalozi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ramadhan Mwinyi.
Dk. Slaa aliishukuru serikali kwa kuwapa mabalozi hao fursa ya kutembelea jengo hilo kujionea kazi nzuri ya serikali ya awamu ya tano iliyomalizia ujenzi wa jengo hilo.

Alisema kiwanja cha ndege ni sehemu ya kuingilia nchini na kama kina huduma na vifaa bora, kama ulivyo huo wa JNIA Terminal 3 utashawishi watu wengi kuingia nchini kupitia lango hilo.

Jengo hilo lina uwezo wa kupokea abiria milioni 6 kwa mwaka wakati lile la Terminal 2 lina uwezo wa kuchukua watu milioni 2 tu, hivyo ni hatua kubwa imepigwa kuhakikisha wasafiri wanahudumiwa kwa haraka na kwa muda mfupi, tofauti na huko nyuma.
Awali, akizungumza wakati akiwakaribisha mabalozi hao ambao wako nchini kuhudhuria mkutano wa Sadc Mkurugenzi Mkuu wa Viwanja vya Ndege nchini, Julius Ndyamukama alisema tayari makampuni 29 kati ya 41 ya usafi yanaendelea na huduma mengi yao yakiwa ni ya wazawa.

Mabalozi hao walitembezwa kuanzia sehemu ya mwanzo ya ukaguzi, sehemu ya uhamiaji, kuondokea abiria, daraja la kuingilia ndani ya ndege, sehemu ya kufikia abiria na sehemu ya mizigo kabla ya kutoka nje ya kiwanja hicho.
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dk Asha Rose Migilo alimwambia mwandishi wetu kuwa kutokana na kazi nzuri wanayofanya mabalozi nje ya nchi, watu wengi wakiwemo watalii wanataka kutembelea Tanzania, hivyo kiwanja hicho kinaendana na wakati.
Alisema uwezo wake wa kuchukuwa watu wengi kwa wakati mmoja, huduma kiwanja hicho kina hadhi ya hali ya juu na itasaidia sana kupokea watu hao na kuwapokea bila tatizo.

No comments:

Post a Comment