Friday 1 February 2019

Kijazi kubariki Bonanza la Shimiwi Dodoma kesho

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WATUMISHI zaidi ya 1,000 kutoka Wizara na Idara za Serikali leo watashiriki kwenye Bonanza la Michezo litakaloongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Utumishi wa Umma ambaye pia ni Mlezi wa Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), litakalofanyika Jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa SHIMIWI, Daniel Mwalusamba amesema bonanza hilo litatanguliwa na mbio fupi fupi (jogging) zitakazoanzia kwenye uwanja wa Jamhuri hadi maeneo ya Bunge na kurudi kiwanja cha Jamhuri, ambapo mbali na Katibu Mkuu Kiongozi, pia watashiriki Watendaji Wakuu wa kutoka taasisi mbalimbali za Umma.

Mwalusamba amesema baada ya mbio hizo wachezaji wote walioshiriki ;watafanya mazoezi ya viungo na baadaye kushiriki kwenye michezo ya netiboli, soka na kuvuta Kamba.
Wajumbe wa klabu mbalimbali za Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa wakimsikiliza Mwenyekiti, Daniel Mwalusamba alipoendesha kikao leo kwenye ukumbi wa mikutano Hazina Dodoma.
“Hili bonanza ni moja ya njia ya kuwaweka watumishi wa umma katika afya njema na kuepuka magonjwa nyemelezi, ambapo mtumishi ataweza kufanya kazi kwa weledi na bidi kwa kuwa wanakuwa na afya nzuri,” amesema Mwalusamba.

Pia amesema bonanza hilo litaendelea kesho (Jumapili) kwa michezo mbalimbali.
Akizungumzia uwepo wa mashindano ya michezo ya SHIMIWI, ambayo imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara kutokana na sababu mbalimbali, Mwalusamba amesema mashindano hayo yapo na hayajafutwa na yatafanyika kulingana na taratibu.

“Hii michezo haijafutwa lakini kumekuwa na mabadiliko ya kiutaratibu, ambapo sasa serikali yetu ipo katika harakati za ujenzi wa viwanda na sisi ni watu muhimu wa kuimiza hilo, hivyo michezo itaendelea kama ilivyopangwa,” amesema Mwalusamba.
Hatahivyo, amehimiza Watumishi wa Umma kuhakikisha wanatekeleza agizo la Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan la watumishi wafanye mazoezi kila Jumamosi ya Pili ya kila mwezi, ili waweze kujiweka vyema katika afya.

Klabu mbalimbali zimekuwa zikiendesha michezo mbalimbali kwa kushirikisha klabu kwa kushirikiana.

No comments:

Post a Comment