Tuesday 18 December 2018

Ndege Mpya Mbili za ATCL Kuwasili Jumapili


Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela akimkaribisha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwele.

Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imesema ndege mpya mbili za ATCL zinatarajiwa kutua Jumapili zikitokea nchini Canada tayari kwa kuanza kufanya kazi ya kusafirisha abiria.

Aidha, aliwaondoa watu hofu kuwa kusimamishwa kwa huduma za ndege ya Fastjet hakutawaathiri kwa vile wamejipanga kusafirisha abiria usiku na mchana ili kuhakikisha hawapati shida ya usafiri.

Akizungumza na waandishi wa habari,  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele alisema ndege hizo zitatua kama ratiba haitabadilika, kwani wameshapeleka rubani na wahudumu wa ndege kwenda nchini humo kwa ajili ya kurudi nazo.

“Mtengenezaji alituahidi mpaka Desemba 23, mwaka huu zitakuwa ziko tayari kurudi kuja kuanza kazi,  tayari tumepeleka wahudumu wa kuja nazo,”alisema.

Waziri huyo aliwatoa hofu Watanzania kuwa  hakuna atakayepata shida ya usfiri wa ndege kwani wamejipanga kwa viwanja vyenye taa kusafiri mpaka usiku na vile visivyokuwa na taa kama Songwe wataongeza ndege kutokana na uhitahiji ili watu wasikose usafiri kwenda na kutoka maeneo yote.

Aliwataka wahudumu wote wa ndege  na wale wa Mamlaka ya Usafiri wa  nchi Kavu na Majini (Sumatra) waliokwenda likizo kurudi haraka kusimamia huduma hizo hasa kipindi hiki cha sikukuu na kuhakikisha nauli haziongezwi upande wa mabasi yaendayo mikoani.

Alizungumzia kuhusu Fastjet kupewa notsi ya siku 28 kwa ndege hiyo kusitisha huduma baada ya kushindwa kulipa madeni yake na kutokidhi huduma za abiria na kwamba hawataruhusiwa kuruka popote hadi kuyalipa ikiwemo huduma, mishahara wanazodaiwa.

Pia Waziri Kamwele aliwataka viongozi na wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuhakikisha wanafanyia kazi malalamiko ya abiria wanayoyatoa juu ya mapungufu katika viwanja vya ndege vikiwemo vipoza hewa katika eneo la pili la kuwasili na kuondokea abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Juliuys Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Alisema abiria wamekuwa wakilalamika kuhusu joto lililopo Terminal Two, lakini wahusika hawajachukua hatua yoyote ya kurekebisha na wameendelea kufanya kazi kimazoa tu wakati hiki ni kipindi cha ushindani.

Pia alisema mtandao nao haufanyika  kazi vizuri, hivyo aliwataka TAA kuchukua hatua haraka kurekebisha matatizo hayo, sivyo kuanzia mwakani atachukua hatua kali.

Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela aliomba muda ili kufanyia kazi mapungufu hayo na kusema atachukua hatua za kiutawala kuhakikisha mambo yanakuwa sawa haraka iwezekanavyo.

Mayongela pia aliwataka waandishi wa habari kuwa makini kwa kuandika au kutangaza habari kutoka katika vyanzo vya uhakika au rasmi na sio kupokea taarifa upande mmoja tu, tena kutoka katika mitandao.

Waziri alitoa muda hadi Januari mwakani kufanyia kazi changamoto hizo na ikiwa watashindwa basi wajiondoe wenyewe huku akisisitiza kuwa, sehemu ya tatu ya abiria ya Kiwanja cha Ndeger cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), kinatarajia kuanza kutumika Mei mwakani.

No comments:

Post a Comment