Friday 14 December 2018

Wanariadha Arusha Watamba Riadha ya Wazi


Viongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kabla ya kuanza kwa mbio za kilometa 10 za mashindano ya wazi ya taifa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha leo.
Na Mwandishi Wetu, Arusha
MASHINDANO ya wazi ya taifa ya riadha ya Ngorongoro ‘Ngorongoro National Open Athletics Championships’ yamefanyika leo jijini Arusha na kushuhudiwa na watazamaji kibao waliofika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid huku wanariadha wa Arusha wakitamba.

Tofauti na mashindano hayo yanapofanyikia jijini Dar es Salaam, leo uwanja huo ulikuwa na watazamaji kibao walioshuhudia wanariadha  wao, wengi wakitokea Arusha wakitamba katika mbio na michezo mbalimbali.
 
Mashindano hayo yalidhaminiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa mara ya kwanza katika mashindano ya taifa yalishirikisha mbio za barabarani za kilometa 10 badala ya zile za uwanjani za meta 10,000, ambazo  jana hazikuwepo.
 
Katika mbio za kilometa 10, Jackson Mwakombe alimaliza wa kwanza kwa kutumia dakika 32:00.22, baada ya kuongoza kwa muda mrefu mbio hizo akiwaacha wenzake mbali.
Wanariadha wakichuana katika mbio za meta 5,000 za mashindano ya wazi ya taifa jijini Arusha leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
 Arusha pia ilitwaa medali ya dhahabu katika kilometa 10 kwa wanawake wakati Neema Kisuda alipomaliza wa kwanza kwa kutumia dakika 40:01.04 akifuatiwa na wanariadha wengine wa Arusha, ambao ni Gloria Makula na Sarah Hiti waliomaliza katika nafasi ya pili na tatu kwa dakika 40:27.98 na 41:26.91.

Benjamin Michael alimaliza wa kwanza kwa kutumia sekunde 10:99, huku Laurent Masatu na Bakari Barnabasi wote wa Arusha wakimaliza katika nafsi ya pili na tatu kwa kutumia sekunde 11:10 na 11:18.
Mwanariadha kipita mbele ya bango la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, ambao ni wadhamini wa mbio za wazi za taifa zilizofanyika leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Katika mbio za meta 800, Mariam Salim, Grace Jackson na Shamin Ramadhani wote wa Arusha walimaliza kwa dakika 2:18.09, 2:20.72 na 2:21.87 na kushika nafasi ya kwanza, ya pili na tatu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Kwa upande wa meta 5,000 wanawake, Arusha ilishika nafasi mbili za kwanza pale, Natalia Elisante na Angelina Daniel walimaliza wa kwanza kwa kutumia dakika 16:54.52 na 17:18.80 huku Angelina John wa Singida akimaliza wa tatu kwa kutumia dakika 18:10.68.
Ni hatari lakini salama! Mwanariadha Jackson Makombe akipita eneo la Njiro huku magari nayo yakipita wakati wa mbio za kilometa 10 za mashindano ya wazi ya taifa jijini Arusha leo. Makombe alishinda mbio hizo kwa dakika 32:00.22.
Katika mbio za meta 800 kwa wanaume, mwanariadha wa Manyara Gabriel Geay alitamba baada ya kumaliza wa kwanza kwa kutumia dakika 1:50.75 huku akifuatiwa na Faraja Damas na Simon Francis wote wa Arusha waliotumia muda wa dakika 1:52.28 na 1:52.68.

Washindi wa kwanza katika kila mchezo wa mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, waliondoka na Sh 150,000 kila mmoja wakati wale walioshika nafasi za pili kila mmoja alipata 100,000 na watatu Sh 50,000.
Watoto nao walichuana katika mbio za meta 100 wakati wa mashindano hayo ya wazi ya taifa leo Sheikh Amri Abeid.
 Washindi wa kwanza wa michezo yote kuanzia ile ya kilometa 10, meta 5,000,  meta 100, meta 800, kuruka chini, meta 400, meta 1500, meta 200 na wale wa kupokezana vijiti, wote kesho watatembelea hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, ikiwa ni ofa kutoka kwa wadhamini wa mashindano hayo.
Wanariadha wakike wakichuana katika mbio za meta 5,000.

Mwanariadha akiruka chini wakati wa mashindano ya wazi ya taifa ya riadha leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

No comments:

Post a Comment