Monday 26 November 2018

Majengo ya Shule ya Tumaini Kuongeza Ufaulu



Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe akikata utepe wa boksi lililohifadhi funguo zote za madarasa 24 za shule ya Msingi Tumaini ya Bukoba, ambapo jana aliikabidhi kwa rasmi kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli. Shule hiyo imejengwana Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).


Na Mwandishi Wetu, Bukoba

UBORA wa majengo ya shule mpya ya Msingi ya Tumaini Bukoba yenye miundombinu ya kisasa pamoja na maji na umeme, yataongeza ufaulu wa wanafunzi wa darasa la Saba, imeelezwa.

Kauli hiyo, imetolewa jana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe Isack Kamwelwe alipokuwa akiikabidhi shule hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, John Pombe Magufuli.

Mhe. Kamwelwe amesema majengo hayo ya kisasa yaliyojengwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ni kielelezo cha kuwafanya wanafunzi wasome kwa bidii kutokana na kuwa na miundombinu rafiki.


1.        Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe akinyanyua juu funguo za moja ya madarasa 24 ya Shule ya Msingi Tumaini ya Bukoba, kabla ya kuikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli.

“Hii shule inamajengo mazuri sana natamani nirudi katika umri wa mtoto ili nisome hapa, maana madarasa mazuri, nasikia pia kuna umeme na maji ya kutosha, basi ninaimani kubwa ubora huu utakuwa chachu ya kuongeza juhudi katika masomo na mtafaulu zaidi,” amesema.

Pia amewapongeza TAA kwa kuhakikisha wanawajali wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kujenga madarasa matatu kwa ajili ya kufundishiwa na chumba kimoja kinachotumika na walemavu hao kupumzika nyakati za mchana.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela amesema Mamlaka ilijenga shule hii mpya kwa sababu shule ya zamani ilikuwa imejengwa eneo hatarishi ikiwa na mita chache kutoka kwenye barabara ya kutua na kuruka kwa ndege na pia kelele na mingurumo ya ndege sio salama kwa wanafunzi na walimu wao.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe jana akimkabidhi funguo za Shule ya Msingi Tumaini ya Bukoba kwa  Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli. Kulia Mwenye tai nyekundu ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).  (Picha kwa hisani ya TAA)
Bw. Mayongela amesema ujenzi wa shule hiyo imejumuisha jumla ya madarasa 24 kati ya hayo matatu ni ya watoto wenye uhitaji maalum, jengo la utawala, chumba cha kupumzikia watoto wenye uhitaji maalumu, uzio na vyoo.

“Kiusalama ilikuwa lazima shule ya Tumaini iondoke pale kiwanjani na kutafutiwa sehemu nyingine, kwani wakati ndege inatua inakuwa na makelele na kutua kwake inakuwa karibu na paa la shule inaleta shida,” amesema Bw. Mayongela.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya TAA, Mhandisi Prof. Ninatubu Lema amewataka watoto wasome kwa bidii ili waweze kufika Chuo Kikuu kusomea uhandisi ambao wanahitajika kwa wingi.

“Mimi ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, natamani sana baada ya miaka 15 nije kuwafundisha uhandisi kule Chuo Kikuu, taifa linauhitaji sana wa Wahandisi, hivyo msome kwa bidii maana hata shule hii mliyokabidhiwa ni nzuri na inawavutia kusoma, nawapongeza na wazazi waliowaleta shule kusoma,” amesema Prof. Lema.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti ameishukuru serikali kwa kuwezesha ujenzi wa shule hii, ambayo imejengwa kwa kuhudumia wanafunzi wazima na wenye mahitaji maalum, ambapo kwa mkoa mzima hii ndio ya kipekee.

“Tunakuomba ufikishe salaam zetu za shukrani kwa Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa shule hii, ambayo itainua kiwango cha elimu cha mkoa wetu, mwaka huu darasa la Saba tumeshika nafasi ya Tano Kitaifa, ninaimani mwakani (2019) tutakuwa juu zaidi,” amesema.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi.Augustina Daniel amesema ufaulu umeongezeka mara dufu na wazazi wamekuwa na mwamko wa kuandikisha wanafunzi wengi wa darasa la kwanza.

“Tumekuwa tukipata idadi kubwa ya wanafunzi wanaokuja kujiunga na darasa la kwanza, ambapo mwaka 2018 tumeandikisha 246 wa darasa la kwanza,  na  hata ufaulu wa darasa la saba umeongezeka tumefaulisha kwa asilimia 97.7,” amesema Bi. Daniel.

Shule hiyo yenye wanafunzi 1232 kati ya hao 45 ni wenye uhitaji maalum, na imejengwa na Kampuni ya Ujenzi ya CMG Construction Co Ltd.


No comments:

Post a Comment