Thursday 22 November 2018

BMT yaitaka RT kutumia vizuri mashindano ya wanawake

Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa, BMT, Alex Nkenyenge akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kuhusu mashindano ya taifa ya riadha ya wanawake. Kulia ni Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Misaada ya Kimaendeleo la Japan Tanzania, Jica, Toshio Nagase. Kushoto ni Katibu Msaidizi wa RT, Ombeni Zavalla.

Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), limelitaka Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kutumia mashindano ya taifa ya riadha ya wanawake kuchagua timu ya wanariadha watakaoenda kushiriki mashindano ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki 2020 itakayofanyika Tokyo, Japan.

Mashindano hayo ya pili ya taifa ya wanawake, ambayo yanajulikana kama JICA Ladies First, yatafanyika kwenye Uwanja Taifa Jijini Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia Jumamosi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu wa BMT Alex Nkenyenge alisema, jumla ya wanariadha 155 wanatarajia kujitokeza kushiriki katika mashindano hayo.

Nkenyenge alisema kuwa mashindano hayo ni muhimu kwa sababu yatawasaidia RT kugundua vipaji vya riadha, ambavyo watavitumia katika mashindano mbalimbali ya kufuzu kwa michezo ya Olimpiki.

"Hii ni nafasi muhimu  kwa RT kuchagua wanariadha wenye viwango kwasababu mwakani kuna mashindano ya kufuzu kushiriki michezo ya Olimpiki," alisema Nkenyenge.

Alisema kutokana na hilo, Kamati ya RT iwe makini kwenye mashindano hayo ili kupata wanariadha watakaofanya vizuri na kufikia viwango, ambavyo vitawasaidia kwenda kushinda katika mashindano mbalimbali ya kufuzu kwa Olimpiki yanayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha (IAA).

Alisema mpaka sasa mikoa yote imethibitisha kushiriki katika mashindano hayo ambayo mwaka jana ilishirikisha wanariadha wanawake 123 kutoka mikoa 26 ya Bara na Visiwani.

Naye Mwakilishi Mkuu wa JICA, Toshio Nagase alisema mashindano haya ni muhimu kwa Tanzania hususani wanariadha wakike kwa sababu yanatoa nafasi ya wao kwenda Japan kushiriki mbio mbalimbali nchini humo.

Mbali na hilo alisema ushiriki wa mashindano hayo, unawasaidia  wanariadha kuinua vipaji vyao kutokana na kwenda nje ya nchi katika.mashindano ya kirafiki ambayo ni moja ya mazoezi ya kujiandaa na michuano mbalimbali ya kimataifa, yakiwemo yale ya kufuzu Olimpiki ya 2020.

"Nimefurahia kuona mwitikio wa mikoa ni mkubwa, tutaendelea kushirikiana ili kuinua vipaji vya wanariadha wa Tanzania," alisema Nagase.

Kwa upande wa Katibu msaidizi wa RT, Omben Zavalla alisema wanakila sababu ya kuwashukuru JICA kwa sababu wamefanya jambo kubwa kwa RT pamoja na maendeleo ya riadha kwa ujumla.

"Huu ni ushirikiano mzuri sana kwasababu unasaidia kuibua vipaji vya wanariadha mbalimbali kutoka mikoani," alisema Zavalla.

Alisema wanariadha waliochaguliwa kuwakilisha mikoa yao washindani kwa bidii ili kuonesha uwezo wao.

Mashindano hayo yanatarajia kuanza kesho huku wanariadha 155 wanatarajia kushiriki,ambapo kutakuwa na mbio za mita 100,200, 400, 800, 1,500 na meta 10,000 sambamba na kurusha mkuki.

Jica ndio wadhamini wa mashindano hayo, ambayo yaliadhishwa baada ya mwanariadha wa zamani kwa kushirikiana na RT kuiomba Jica idhamini ili Tanzania iwe na wanariadha wengi katika Olimpiki ya 2020.


No comments:

Post a Comment