Friday 16 November 2018

Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi wajifunza mengi TB3




1.        Wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar leo wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutembelea jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere kwa ajili ya kujifunza.

Na Mwandishi Wetu

WAJUMBE wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar imekiri kujifunza mambo makubwa katika ujenzi wa jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3), imeelezwa.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambayo ilikuwa na ziara kwenye jengo hilo na Mhe. Mohammed Said (Mwakilishi wa Mpendae), amesema ujenzi wa jengo hilo ni fundisho tosha kutokana na kwenda kwa kasi tangu ujenzi wake uanze Juni  2013, tofauti na ujenzi wa jengo la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Amani Abeid Karume umechukua takribani miaka 10 tangu mwaka 2009 lakini hadi sasa lina asilimia 39 pekee.

1.        Mhandisi Barton Komba wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), (aliyesimama mbele), leo akitoa maelezo ya maendeleo ya mradi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere kwa Wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar walipofanya ziara ya mafunzo.

Mhe. Said amesema TB3 ni jengo la kisasa kutokana na miundombinu yake ambayo mingi inaendeshwa kwa mifumo maalum, ikiwemo sehemu ya mizigo, ambayo inaendeshwa kupitia hatua tano.

“Katika ziara hii tumefarijika sana kwani tumejifunza mengi wenzetu walivyoweza kuufikisha mradi huu, kwa kweli tumechukua yote na tutakwenda kuishauri serikali namna bora ya kuendeleza ujenzi wa majengo na viwanja vya ndege kwa ujumla,” amesema Mhe. Said.

Hali kadhalika, Mhe Said amesema mbali na kutembelea jengo hilo, pia wamepata maelezo mazuri ya kiutendaji katika uendeshaji, ukusanyaji na mgawanyo wa mapato kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na wataishauri serikali namna bora ya kudhibiti mapato.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Lawrence Thobias, ameishukuru kamati hiyo kwa kuichagua TAA kuwa sehemu yake ya mafunzo, kwa kuwa imezoeleka wengi wanaotaka kujifunza lazima waende nje ya nchi.

1.        Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mohammed Said (aliyesimama katikati) pamoja na wajumbe wakimsikiliza Mhandisi Barton Komba wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) (aliyenyoosha mikono), akiwaelezea ujenzi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere leo walipofanya ziara ya mafunzo. 

Bw. Thobias amesema TAA ikiwa ni moja ya taasisi za serikali chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, imekuwa ikijiendesha kwa kufuata sheria na taratibu za ukusanyaji wa mapato za serikali.

Akiwasilisha maendeleo ya mradi wa jengo la tatu la abiria, mmoja wa wasimamizi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Burton Komba amesema hadi kufikia Oktoba 31, 2018 umefikia asilimia 85.53 na unatarajiwa kukamilika Mei 2019.

Mhandisi Komba amesema ujenzi wa jengo hilo ambalo litahudumia abiria milioni sita kwa mwaka, umehusisha eneo la maegesho ya ndege lenye mita za  mraba 227,000 lenye uwezo wa kuegesha ndege 19 za Daraja C kwa wakati mmoja zikiwa kwenye madaraja na eneo lisilokuwa na madaraja.

“Pia eneo hili linaweza kuegesha ndege za daraja E 11 mfano wa hii Dreamliner ya ATCL Boeing 787 na Boeing 777, ni eneo kubwa,” amesema.

Pia amesema kumejengwa maegesho ya magari mchanganyiko yasiyopungua 2075 kwa wakati mmoja; barabara za kuingia na kutoka eneo la jengo; uzio wa usalama, mifumo ya maji taka nay a mvua; ujenzi wa matanki ya kuhifadhia maji yenye ujazo wa lita milioni 2.26; kituo kikubwa cha umeme (33Kv); usimikaji wa jenereta saba zenye uwezo wa KvA 2000 kila moja; ujenzi wa mifumo ya kujaza mafuta kwenye ndege na kusimika mifumo ya mawasiliano na usalama.

No comments:

Post a Comment