Thursday 7 June 2018

Makocha Simba Sport Club Wabwaga Manyanga


Na Mwandishi Wetu, Nakuru
WAKATI Simba imetinga fainali ya mashindano ya SportsPesa Super Cup, swali ni je wameachana na makocha wao baada ya leo kuwa katika jukwaani wakishuhudia timu yao ikishinda kwa penalti 5-4 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Afraha mjini Nakuru.

Kocha Mkuu, Pierre Lechantre na kocha wa viungo wa timu hiyo kutoka Morocco, jana walishuhudia pambano hilo kutokea jukwaani na taarifa zilidai kuwa tayari wameachana na timu hiyo baada ya kumaliza mkataba wao.

Hatahivyo, taarifa zingine zilidai kuwa, Mfaransa Lechantre ametofautiana na uongozi wa Simba na hivyo hawako tayari kumuongezea mkataba mwingine, licha ya kuipatia mafanikio timu hiyo hadi kuipatia ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara iliyoukosa kwa karibu miaka mitano.

Hatahivyo, hakuna kiongozi wa Simba aliyekuwa tayari kulizungumzia hilo, lakini walisema wangekuwa na kikao jana usiku na taarifa kamili wangezitoa baadae.

Timu hiyo jana ilikuwa chini ya kocha msaidizi Mburundi Masoud Djuma, ambaye ndiye akapewa mikoba hiyo.

Wakati huohuo, Singida United ya Tanzania jana ilitolewa katika mashindano ya SportPesa Super Cup baada ya kulambwa mabao 2-0 na mabingwa wa Kenya katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Afraha mjini hapa.

Kwa kipigo hicho, Singida United wanaungana na mabingwa wazamani wa Tanzania Bara, Yanga na JKU ya Zanzibar kuyaaga mashindano hayo baada ya kutolewa katika nusu fainali, Yanga na JKU wenyewe walitolewa katika robo fainali.

Mabao yote ya Gor Mahia yalifungwa na Meddy Kagere katika kila kipindi na kuifanya timu hiyo kujihakikishia nafasi ya kucheza dhidi ya Simba katika fainali itakayopigwa Jumapili kwenye uwanja huo.

No comments:

Post a Comment