Wednesday 6 June 2018

Simba, Singida ni Shida Nusu Fainali SportPesa

Wachezaji wa Simba wakijifua kwa ajili ya nusu fainali ya SportPesa jijini Nakuru hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu, Nakuru
SIMBA na Singida United zimepania kufuzu fainali ya Mashindano ya SportPesa Super Cup yanayofanyika katika Uwanja wa Afraha mjini hapa kwa kuzifunga timu za Kenya ambazo wanakutana nazo kwenye nusu fainali leo.

Timu zote zimefuzu nusu fainali kwa  penalti kwenye michezo yao ya robo fainali ambapo, Simba iliifunga Kariobang, ambao waliwafungisha virago Yanga wakati Singida United ikaifunga AFC Leopard.

Simba itakuwa ya kwanza kutupa karata yake kwa kucheza na Kakamega Homeboys saa 7:00 mchana na Singida itawakabili mabingwa wa Kenya na mashindano ya SportPesa Super Cup, Gor Mahia saa 9:15 alasiri.

Wakizungumzia kwa nyakati tofauti, Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, alisema mchezo wa leo  hautakuwa kama mchezo wa kwanza, kwani hawakucheza vizuri na kuahidi timu yake itabadilika kwenye mchezo huo na kufanya 'surprise'.

"Natarajia leo tutacheza vizuri kila mtu aliona namna, ambavyo tulicheza kwa kiwango kibovu, hivyo mchezo utakuwa na mabadiliko kwenye kikosi chetu ," alisema Djuma.

Naye nahodha wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala' alisema "penalti sio nzuri ni kama bahati nasibu, mchezo uliopita tuliingia tukiwa na nia ya kushinda katika dakika 90, lakini sasa tunarejea tukiwa tumesahihisha makosa yetu na kuja na mbinu mpya," alisema.

Kwa upande wa kocha wa Singida United, Hemeda Morocco, ambaye anakutana na Gor Mahia alisema itakuwa ni mechi tofauti na jinsi walivyocheza na AFC Leopards, hivyo watabadilika ili waweze kushinda mapema japo hawapewi nafasi ya kufika fainali, lakini hawana hofu.

"Mchezo huo utakuwa tofauti na wa juzi, kwani nimepata kuwafahamu wachezaji kidogo sasa baada ya mazoezi ya siku mbili tutacheza soka la tofauti na na mchezo wa juzi, tunaiheshimu Gor lakini tuko tayari kupambana," alisema Morocco.

Pia alisema  hawataki kufika kwenye penalti kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa juzi hivyo wamejipanga kumaliza kazi ndani ya dakika 90.

Naye kocha msaidizi wa Gor Mahia, Ottieno alisema: "Utakuwa mchezo mgumu kwani nimewaona Singida United wanavyocheza ila tumejiandaa kutetea ubingwa wetu, ukitaka kushinda lazima ufunge mabao tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi,"

Simba na Singida endapo zitashinda zitakutana kwenye hatua ya fainali itakayochezwa Jumapili mjini hapa.

Mwaka jana mashindano hayo yalifanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo Gor Mahia iliifunga AFC Leopards na kupata nafasi ya kucheza dhidi ya Everton kwenye uwanja huo.

Bingwa wa mwaka huu, ambali na kuondoka na Kombe, fedha taslimu, itapata fursa ya kwenda England kucheza na Everton kwenye Uwanja wa Godson Park.

No comments:

Post a Comment