Friday 3 June 2016

Ushindi Taifa Stars ni lazima kesho ili kuizuia Misri kufuzu kwa fainali za Afcon Gabon 2017 na kurejesha matumaini ya kufikia rekodi ya mwaka 1980


Wachezaji, viongozi na benchi la ufundi la timu ya taifa ya Tanzania, Taifa wakiwa katika picha ya pamoja.

NA Mwandishi Wetu
TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo inaikaribisha Misri katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Gabon mwakani, katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ni wa Kundi G, huku Nigeria ambayo nayo iko katika kundi hilo ikiwa tayari imeiaga michuano hiyo na Chad ilijitoa mapema na kufanya zibaki timu tatu katika kundi hilo badala ya nne.

Katika mchezo wa leo, Taifa Stars inahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kucheza fainali za Afcon mwakani.

Tanzania inashika mkia katika Kundi G, baada ya kucheza mechi mbili, ikifungwa moja ugenini na Misri 3-0 na kutoa suluhu na Nigeria nyumbani.

Misri inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi  saba baada ya kucheza mechi tatu sawa na Nigeria yenye pointi mbili.

Zote, Misri na Nigeria zimebakiza mchezo mmoja mmoja, wakati Tanzania ina faida ya mechi mbili kwanza  hiyo ya kesho dhidi ya Misri na baadaye Septemba watacheza dhidi ya Nigeria, ambayo tayari imeshatolewa.

Iwapo Tanzania itashinda mechi zote mbili za mwisho watamaliza na pointi saba sawa na Misri, hivyo timu ya kufuzu kutoka Kundi G, itapatikana kwa uwiano wa mabao.

Misri wanahitaji sare tu katika mchezo huo wa kesho ili kujihakikishia nafasi ya kutinga fainali hizo za Afcon, huku Stars ikiombea Misri wafungwe kesho ili kurejesha matumaini hayo ya Taifa Stars kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali tangu walipofanya hivyo kwa mara ya mwisho mwaka 1980 nchini Nigeria.

Ukiangalia katika msimamo wa kundi G, Misri inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi saba, ikifuatiwa na Nigeria ambao wana pointi mbili huku Taifa Stars ikiwa na moja. 

Lakini Stars ina faida ya kuweza kuzifikia pointi za Misri kutokana na kubakisha michezo miwili, tofauti na wenzake ambao wamebakisha mechi moja moja. 

Kocha wa timu ya Taifa, Boniface Mkwasa akizugnumzia mchezo huo alisema Mchezo utakuwa mgumu, hii ni naweza kusema ni fainali, sisi tunahitaji matokeo mazuri zaidi, tunahitaji kushinda magoli si chini ya manne ili tufufue matumiani ya kufuzu, lakini ukiangalia wenzetu Misri wanataka sare ili iwavushe.

Kikosi kamili cha Mkwasa kitakachoivaa Misri ni makipa; Deogratius Munishi Dida (Yanga SC), Aishi Manula (Azam FC), Beno Kakolanya (Prisons FC). Mabeki; Aggrey Morris (Azam FC), Erasto Nyoni (Azam FC), David Mwantika (Azam FC), Juma Abdul (Yanga SC), Mwinyi Hajji Mngwali (Yanga SC), Mohamed Hussein Tshabalala (Simba SC) na Andrew Vicent (Mtibwa Sugar).

No comments:

Post a Comment