Friday, 3 June 2016

Kaimu Mkurugenzi wa kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ahimiza usafi

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Laurent Mwigune (mwenye suti) akishiriki zoezi la kufanya usafi jana maeneo mtaa wa Kigilagila Relini, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la usafi kuelekea Siku ya Mazingira Duniani, Juni 5, 20916.
Na Mwandishi Wetu
KAIMU Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha amehimiza usafi maeneo yanayozunguka kiwanja hicho, ili kuepusha kuzaliana kwa ndege wanyama wa aina mbalimbali.

Rwegasha aliyasema hayo wakati akimwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Mhandisi George Sambali jana wakati wa kufanya usafi wa mazingira ulioongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu,Bw. Laurent Mwigune kwa wafanyakazi wa TAA kushirikiana na wakazi wa mtaa wa Kigilagila Relini ikiwa ni muendelezo kuelekea kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, Juni 5, 2016.

Alisema uchafu unachangia ongezeko la ndege wanyama ambao ni hatari kwa ndege za abiria.

Ndugu zangu tusiruhusu mazingira yetu yakawa machafu, kwani ni hatari kubwa kwa sisi kiwanja cha ndege, kwani ndege mnyama akiingia kwenye injini ya ndege ya abiria atasababisha hasara kubwa.

Wafanyakazi Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) katika picha ya pamoja na
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu,

Laurent Mwigune(watatu kutoka kushoto waliochuchumaa), mara baada ya kumaliza kufanya usafi eneo la Kigilagila jijini Dar es Salaam jana.
Hivyo tujitahidi kufanya mazingira yetu yawe safi ili ndege kama kunguru na wengine wasizaliane hapo kwani wanaweza kuleta madhara, alisema Rwegasha.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo iliyotolewa Kitaifa na Mhe January Makamba , Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ni Tuhifadhi Vyanzo vya Maji kwa Uhai wa Taifa letu.

Alimtaka Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigilagila Relini na Vituka kuhakikisha dampo lisilo rasmi lililoanzishwa karibu na ukuta wa JNIA linaondolewa haraka, na waweke ulinzi kuzuia utupaji wa taka eneo hilo.

Aidha, alisema TAA imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na majirani zake wanaozunguka JNIA, ili kuweka mazingira hayo katika hali ya usalama na usafi, lakini bado wapo wakazi wachache wanaosababisha uhusiano huo kulegalega kwa kufanya vitendo vya kutupa taka hovyo.

Alifafanua zaidi kuwa TAA inaendelea na zoezi la kufyeka vichaka vilivyozunguka JNIA, ili kuzuia uhalifu wa watu wabaya kutumia mwanya huo kuruka uzio na kuingia ndani ya kiwanja hicho.

Sisi hatutanii tena tunaagiza hili dampo liondoke na tutaweka mabango ya kuzuia utupaji wa taka hapa, na Wenyekiti tunaomba mhakikishe mnawakamata wale wote watakaokiuka agizo hilo na tutawachukulia hatua za kisheria, alisema Rwegasha.

No comments:

Post a Comment