Wednesday 1 June 2016

Mchakato wa usajili mbio za watoto, Azani Bank Kids Run waendelea kwa kasi kubwa


Wilhelm Gidabuday akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Kulia ni Ofisa Masoko Mwandamizi wa Benki ya Azani,Othman Jibrea

Na Mwandishi Wetu
MCHAKATO wa usajili wa washiriki wa Mbio za Watoto za Azania Bank, Kids Run 2016, umezidi kushika kasi, huku zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya kufanyika kwake kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, mmoja wa waratibu wa mbio hizo, Wilhelm Gidabuday, alisema kufikia leo mchana, mchakato wa usajili ulikuwa ukiendelea vema, ambako wazazi na walezi wamejitokeza kwa wingi kuandikisha watoto wao.

Gidabuday alisema kuwa, matarajio ni kusajili watoto zaidi ya 2,000 walio na umri chini ya miaka 16, ambao watashiriki Azania Bank Kids Run 2016.
Fomu ya kujisajili kwa ajili ya kushiriki mbio hizo.
Mbio hizo zimegawanywa katika makundi matano, ambayo ni ya kimeta tano, km 2, km 1, mita 100 na mita 50.

Alibainisha kuwa, fomu za ushiriki zinapatikana katika Matawi ya Azania Bank popote jijini Dar es Salaam, pamoja na Ofisi za Ridha Tanzania (RT), pamoja na Ofisi za BMT zilizoko Samora Avenue katikati ya jiji.

Aliwataka wazazi na walezi ambao hawajachukua fomu za ushiriki wa watoto wao, kuchangamkia mchakato huo kwa kufika katika vituo husika na kununua fomu hizo kwa sh. 
 2,000 tu, ili kuwawezesha watoto kushiriki na kushinda zawadi nono.

Naye, Ofisa Masoko Mwandamizi wa Azania Bank inayodhamini mashindano hayo, Othman Jibrea, alisisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kusajili watoto wao katika Azania Bank Kids Run, ili kufikia lengo lao la kuibua vipaji vipya vya riadha.
 
Jibrea alibainsiha kuwa, Azania Bank imejitosa kudhamini mbio hizo kutokana na mlengo wake wa kuibua vipaji vichanga katika riadha, hivyo ili kufikia lengo, wazazui na walezi hawana budi kujitokeza kwa wingi kusajili watoto wao.

Alizitaja zawadi za mbio za Kilometa tano kuwa ni Sh. 200,000 kwa mshindi wa kwanza, Sh. 150,000 kwa mshindi wa pili na Sh. 100,000 kwa mshindi wa tatu, wote wakitarajiwa pia kupata medali, begi lenye vifaa vya shule na sare za michezo (track suit).

Jibrea alibainisha kuwa, mshindi wa kwanza wa mbio za kilomita 2 atajinyakulia Sh. 100,000, mshindi wa pili Sh. 75,000 na mshindi wa tatu Sh. 50,000, pamoja na medali, begi lenye vifaa vya shule na sare za michezo.

Katika mbio za kilomita 1, Jibrea alitaja zawadi za washindi kuwa ni Sh. 75,000 kwa mshindi wa kwanza, 50,000 kwa mshindi wa pili na Sh. 40,000 kwa wa tatu, ambao watapata zawadi ya ziada ya medali, begi lenye vifaa vya shule na sare za michezo.

"Pia, washindi wa nne hadi wa 10 wa mbio hizo, watapata kifuta jasho cha Sh. 15,000, begi lenye vifaa vya shule na sare za michezo. Nia ni kuwafanya watoto watakaoshiriki kutotoka bure mwishoni mwa mashindano," alisema Jibrea.

Pia, washindi wote watafunguliwa akaunti katika benki hiyo ya Azani, ambayo inadhamini mashindano hayo ya kwanza kufanyika nchini.

No comments:

Post a Comment