Na Cosmas Mlekani, Zanzibar
TIMU ya shule ya Filbert Bayi jana ilitamba katika mbio za nyika
za shule za msingi na sekondari za Zanzibar baada ya kushika nafasi ya kwanza
hadi ya tatu katika umbali wa kilometa nne na sita.
Mbio hizo za kila mwaka, mwaka huu zilishirikisha shule zaidi ya
30 za Unguja na shule ya Filbert Bayi ambayo ni pekee kutoka Tanzania bara
iliyoshiriki.
Mwaka jana pia shule za Filbert Bayi za msingi na sekndari ndizo
zilishinda katika mbio hizo ambazi husimamiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Amali kwa kushirikiana na Idara ya Michezo na Utamaduni.
Katika mbio za kilometa kwa wasichana wa shule za msingi, Teresia
Joseph, Evodia Martin na Tumaini wote wa shule ya Filbert Bayi walishika nafasi
ya kwanza hadi ya tatu kwa kutumia dakika 17:41:45, 17:1:40 na 17:55:10.
Wanariadha wakijiandaa kwa ajili ya mbio za nyika Zanzibar Jumamosi. |
Mshindi wa nne wa mbio hizo alikuwa Nasra Khamis wa shule ya
msingi Ndijani ya Zanzibar aliyetumia dakika 18:10:96.
Katika mbio za kilometa sita kwa wasichana; Dorcus Boniface wa
shule ya Filbert Bayi aliibuka wa kwanza kwa kutumia dakika 27:17:12 huku
Regina Deogras na Betrima Matiku nao wa Filbert Bayi walishika nafasi ya pili
na tatu.
Katika mbio za kilometa sita wanaume; Hussein Said Hassa wa shule
ya Ndijani alimaliza wa kwanza kwa kutumia dakika 24:03:94 huku Othman Yussuf
Abdallah naye wa Ndijani alimaliza wa pili kwa kutumia dakika 24:40:18 na
Aboubakar Ame Jecha alimaliza watatu kwa kutumia dakika 24:44:60.
Wasichana wa shule za msingi waianza mbio za nyika za kilometa nne Zanzibar Jumamosi. |
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna aliyekuwa
mgeni rasmi katika mbio hizo aliisifu shule ya Filbert Bayi kwa ushindi
ilioupata na kuzitaka shule zingine kuiga mfano wake.
Alisema, Bayi ambaye aliwahi kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za
mita 1500 ni mfano wa kuigwa kwa wanafunzi wake kuwa mahiri katika mchezo huo
wa riadha hapa nchini.
Naye Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Said Ali
Mbarouk alisema kuwa, michezo hiyo lazima iendelezwe ili kuinua vipaji vya
wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Mashindano hayo pia ni muendelezo wa jitihada na mapendekezo
kutoka kwa Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein akiwa ni miongoni mwa
wakimbiaji wazuri wa mbio kama hizo akiwa mwanafunzi miaka ya nyuma.
No comments:
Post a Comment