Wednesday, 11 March 2015

Mkutano wa marekebisho ya Katiba RT wanuka ukata


Wanariadha wakichuana katika mbio jijini Dar es Salaam hii karibuni. Mbele kulia ni fabian Joseph.

Na Mwandishi Wetu
MAANDALIZI ya Mkutano Maalum wa marekebisho ya Katiba ya Riadha Tanzania (RT) utakaofanyika Jumamosi mjini Morogoro, yanasuasua kutokana na ukata unaliandama shirikisho hilo.

Uongozi RT ulikuwa unahitaji kiasi cha kama Sh. Milioni 21 kwa gharama za kuendeshea mkutano huo ikiwemo posho za wajumbe, malazi, chakula na shughuli zingine za kiofisi, lakini hadi sasa mkononi wana kiasi cha Milioni 10.

Kamati ya Utendaji ya RT imekutana leo jijini Dar es Salaam na kujadili kwa kina, ambapo tegemeo lao kubwa lilikuwa kwa mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Dioniz Malinzi angegharamia mkutano huo kama alivyofanya ule wa mwanzo Novemba 30, 2013.

Habari za uhakika zilizotufikia zinasema kuwa Malinzi ametoa kiasi cha Sh. Milioni 10, hivyo uongozi wa RT unatakiwa kusaka Milioni 11 zilzobaki ili kufanikisha mkutano huo.

Mjumbe mmoja wa Kamati ya Utendaji ya RT alisema kuwa kwa sasa wanahaha kusaka fedha na hawana uhakika kama watazipata fedha hizo ili kufanikisha mkutano huo.

Alisema uongozi wa RT unajisachi na unafuatilia madeni yake ili angalau kupata hizo fedha, ambapo Sh. Milioni 3 watazipata kwa waandaaji wa Kili Marathoni za ada ya kuandaa mashindano hayo.

Naye Katibu Mkuu wa RT Suleiman Nyambui alisema kuwa ni kweli bado wanasaka fedha lakini alimuhakikishia mwanahabari wetu kuwa mkutano huo iwe mvua au jua, lazima hufanyike kwani wanaendelea kujipanga.

Alisema ni kweli hawana fedha za kutosha lakini wanapiga kiume kuhakikisha mkutano huo unafanyika hata kwa kujibanabana, kwani hakuna kurudi nyuma.

Aliwataka wajumbe wa mikoa kujua hali halisi ya ukata inayoikabili RT, hiyo wasiwe wakali watakapokosa posho, lakini malazi,chakula na mambo mengine watapatiwa.

Katika mkutano uliopita wajumbe walikuwa wakali sana wakidai posho zao pamoja na stahiki zingine za mkutano mkuu.

Aidha, Nyambui amekjuwa akipambana usiku na mchana kuhakikisha katiba mpya inamtambua mjumbe wa mmoja wa mkoa tu ndiye atakuwa akipiga kura na ndiye atakayegharamiwa na RT katika mikutano badala ya watatu kama iliyosasa.

Nyambui alisema kuwa nchi nyingi pamoja na Shirikisho la Kimataifa la Vyama ya Riadha (IAAF) zinamgharamia mjumbe mmoja tu katika vikao vyake, na anashangaa Tanzania kuendelea kungangania taratibu za mwaka `47, ambazo zimepitwa na wakati.

No comments:

Post a Comment