Na Mwandishi Wetu
TIMU ya taifa ya ndondi ya Uganda imewasili jijini Dar es Salaam
tayari kwa mashindano ya ndondi yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa
kuanzia kesho Jumanne, imeelezwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Ndondi Mkoa wa Temeke (Teaba), ambao ndio
waandaaji wa mashindano hayo ya kimataifa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
BFT, Said Omary `Gogopoa’ alisema kuwa
timu hiyo iliwasili usiku wa kuamkia jana ikiwa na mabondia 10 na viongozi
wawili.
Hatahivyo, alisema kuwa pamoja na mashindano hayo kupangwa kuanza kesho Jumanne na Uganda wameshawasili na Kenya wakiwa njia kuja, bado waandaaji hawajapa hata thumni kwa ajili ya mashindano hayo.
Aliwaomba watu wenye mapenzi mema akiwemo mwenyekiti wa IPP Reginald Mengi kusaidia kuokoa mashindano hayo kwani ni aibu tayari wageni wameshafika.
Alisema kuwa mbali na Uganda, timu zingine za nje zitakazoshiriki
mashindano hayo ni Kenya baada ya Zambia ambayo nayo ilithibitisha kushiriki,
kushindwa kuja nchini kwa sababu mbalimbali.
Gogopoa alisema kuwa, timu
ya taifa ya Kenya nayo itashiriki mashindano hayo kwani ilitarajia kuwasili
wakati wowote jijini Dar es Salaam.
Awali, mbali na Uganda, Zambia na Kenya, nchi zingine
zilizotarajia kushiriki ni pamoja na Ethiopia, Sudan na Djibout, ambazo
hazitashiriki kwa sababu mbalimbali.
Alisema kuwa Teaba bado haijapata fedha kwa ajili ya mashindano
hayo ambayo awali ilihitaji bajeti ya sh. Milioni 27 kama mikoa 17 na nchi tano
zingeshiriki katika mashindano hayo yaliyopangwa kufikia tamati Machi 28 mwaka
huu.
Alisema kuwa kwa sasa wanahitaji kama kiasi cha sh. Milioni 10 tu
kwa ajili ya kufanikisha mashindano hayo, ambayo Shirikisho la Ndondi Tanzania
(BFT) nao watayatumia kwa ajili ya kupata timu ya taifa itakayojiandaa kwa
ajili ya mashindano ya Mataifa ya Afrika yatakayofanyika Brazzaville, Kongo
Septemba mwaka huu.
BFT hivi karibuni iliteua mabondia 37 ambao ingewachuja katika
mashindano maalum , ambayo hatahivyo walishindwa kuyaandaa kwa sababu ya ukata,
na baadae wangepata wachezaji 15 watakaoingia kambini kujiandaa na michezo hiyo
ya Afrika, na hivyo imewabidi kutumia mashindano hayo yaliyoandaliwa na Temeke.
No comments:
Post a Comment