Saturday 9 July 2016

Ureno yaivaa Ufaransa katika fainali ya Mataifa ya Ulaya ya euro 2016 kesho Jumapili



PARIS, Ufaransa
BEKI wa kushoto mwenye kipaji, Raphael Guerreiro ni mmoja kati ya wachezaji watatu wa Ureno ambao watakaikabili nchi yao waliyozaliwa, wakati watakapokutana na Ufaransa kwenye fainali ya mataifa ya Ulaya, Euro 2016, kesho Jumapili saa nne usiku kwa saa za hapa Bongo.

Guerreiro na golikipa, Anthony Lopes walizaliwa na kukulia nchini Ufaransa, ambako ni nyumbani kwa Wareno wengi wahamiaji.

Kiungo Adrien Silva aliishi nchini Ufaransa hadi akiwa na umri wa miaka 12, wakati alipohamia nchini Ureno na familia yake.

Nilichagua Ureno. Yalikuwa maamuzi yangu muhimu. Si familia yangu wala marafiki zangu ambao waliweza kuubadilisha uamuzi wangu, amesema Guerreiro mwenye umri wa miaka 22, ambaye mwezi uliopita alikubali uhamisho wa kwenda kwa miamba ya Ujerumani, Borussia Dortmund akitokea Klabu ya Lorient inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa, Ligue 1.

Guerreiro alizaliwa kitongoji cha Le Blanc Mesnil jijini Paris, umbali mfupi kutoka kwenye Uwanja wa Stade de France ambako fainali hiyo inachezwa leo.

Ufaransa inaingia kwenye mchezo huo ikiwa ni nchi ya kwanza kufika mara mbili fainali ya Euro ikiwa nchi mwenyeji wa mashindano, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1984.

Michel Platini bado anashikilia rekodi ya magoli mengi zaidi kwenye msimu mmoja wa michuano ya Euro (magoli 9, Euro 1984) magoli matatu zaidi ya Antoine Griezmann aliyefunga magoli 6 hadi sasa Euro 2016. 

Kwa upande wao Ureno hadi wanamaliza hatua ya makundi walikuwa hawajashinda mchezo hata mchezo mmoja. Ni mfumo tu wa mashindano ya mwaka huu ndiyo uliwapa nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora, kupitia mlango wa nyuma.

Ureno mechi yao katika hatua ya 16 bora ilishuhudia dakika 90 zikiisha kwa sare. Bao la ushindi likapatikana dakika ya 117, dakika tatu kabla ya dakika za nyongeza kumalizika.
Ureno kwenye hatua ya Robo fainali waliitoa Poland kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya bao 1-1 dakika 120. 

Cristiano Ronaldo ameifikia rekodi ya gwiji wa Ufaransa, Michel Platini ya kufunga magoli 9 ya Euro. Ronaldo alifunga goli lake la kwanza kwenye michuano ya Euro mwaka 2004.

Anahitaji goli moja ili kuwa mfungaji bora wa muda wote kwenye michuano ya Euro.

Mara ya mwisho timu kutinga fainali kiujanja ujanja namna hii kama Ureno, ilikuwa Italia kwenye kombe la Dunia 1982 na ikawa bingwa.

No comments:

Post a Comment