Monday 11 July 2016

Caf yaipiga faini yanga ya milioni 10 kwa wachezaji wake kumzonga mwamuzi walipocheza na timu ya Angola



Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Yanga imesema kuwa inatafakari adhabu ya dola 5,000 (sawa n ash milioni 10) waliyopigwa na Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) baada ya wachezaji wake kuchelewesha muda.

Caf juzi ilitangaza kuiadhibu Yanga baada ya baadhi ya wachezaji wake kumzonga mwamuzi na kusababisha kuchelewesha mchezo wake timu hiyo ilipocheza na GD Sagrada Esperanca uliofanyika Angola Mei 18, 2016.

Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit anakiri wachezaji wao kumzonga mwamuzi lakini kwa sasa wanatafakari kabla ya kutoa tamko kamili.

Mchezo huo ulikuwa ni wa hatua ya kutafuta nafasi ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika.

Uamuzi wa mchezo huo Na. 100 ulifanywa na Kamati ya Nidhamu ya CAF inayoundwa Mwenyekiti Raymond Hack Raia wa Afrika Kusini na wajumbe Mustapha Samugabo (Burundi) na Gbenga Elegbeleye (Nigeria). Pia alikuwako Amina Kassem kutoka Sekretarieti ya CAF ambaye ni Mtawala katika Kitengo cha Nidhamu.

Katika mkutano huo uliofanyika Cairo, Misri Makao Mkuu ya CAF, Julai 3, 2016, kamati ilipitia taarifa zote za mchezo na kufikia uamuzi wa kuipiga faini Yanga.

Taarifa za mchezo zinasema, wachezaji wa timu hiyo walionesha utovu wa nidhamu kwa kumzonga mwamuzi na kumsukuma mara baada ya kutoa adhabu ya penalti kwa wapinzani. 

Kwa tukio hilo, mchezo huo ulisimama kwa dakika sita. Polisi waliingia uwanjani kudhibiti hali hiyo.

Kwa kosa hilo, Wachezaji wa Yanga walivunja Ibara ya 82 inayozungumza utaratibu wa mawasiliano. Kwamba chama chochote cha mpira wa miguu, klabu, ofisa au mtu yoyote wakiwamo wachezaji, lazima waheshimu utaratibu za kuvumilia, uadiliufu na uanamichezo.

Kwa mujibu wa Kamati hiyo ya Nidhamu ya CAF, Yanga ilistahili kutozwa faini ya dola 10.000 za Marekani kwa makosa ambayo si uungwana kwenye soka yaliyoonyeshwa na wachezaji wake.

Lakini kwa kuwa Yanga haikuonyesha utovu wa nidhamu katika mchezo mingine ya kimataifa iliyofuata dhidi ya MOB ya Algeria na TP Mazembe ya DRC, imepunguziwa adhabu na sasa wametakiwa kulipa dola 5,000 za Marekani kama faini.
Faini hiyo haina budi kulipwa mara moja. Na imetakiwa kuendelea kuwa na nidhamu, vinginevyo adhabu hiyo itawarudia.

No comments:

Post a Comment