Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Azam imeanza vizuri kutetea ubingwa wa Kombe la
Mapinduzi baada ya kuinyuka Mwenge mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika usiku wa kuamkia leo kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Kwa ushindi huo, Azam FC imekaa kileleni mwa Kundi A
ikiwa na pointi tatu sawa na Mwenge, ambayo ilipata ushindi kwenye mchezo wa
kwanza dhidi ya Jamhuri, zote zikiwa ni timu kutoka Pemba.
Kwa mujibu wa televisheni ya Azam ilionesha mchezo huo
`live’, benchi la ufundi la Azam FC liliutumia mchezo huo wa kwanza kuwapa
nafasi wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kucheza kwenye mchezo uliopita wa
ligi dhidi ya Stand United pamoja na wale waliocheza dakika chache.
Mshambuliaji chipukizi wa timu hiyo, Paul Peter, ndiye
aliyeibuka shujaa baada ya kufunga mabao yote mawili la kwanza akitupia dakika
ya 41 baada ya kazi nzuri iliyofanywa na mshambuliaji Bernard Arthur, aliyepiga
shuti lililopanguliwa na kipa kabla ya mfungaji kuuwahi mpira na kumalizia.
Peter aliyechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo,
alifunga bao la pili dakika ya 62 akimalizia pia kwa shuti baada ya kukutana na
mpira uliotemwa na kipa kufuatia shuti lililopigwa na Idd Kipagwile.
Baada ya mchezo huo, Azam FC itashuka tena dimbani kesho
kuvaana na Jamhuri ya Pemba, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Amaan.
No comments:
Post a Comment