Na
Mwandishi Wetu, Kahama
KAMPUNI
ya madini ya ACACIA yenye kumiliki migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyahulu
imekirudisha serikalini Kiwanja cha Ndege cha Kahama kwa ajili ya kuchochea
maendeleo kwa ujumla.
Awali
mwaka 2005 kiwanja hicho kilikabidhiwa kwa makabidhiano maalum kati ya serikali
na iliyokuwa kampuni ya madini ya Barrick walioomba ili kurahisisha shughuli
zao za migodini ikiwemo ya kutumia ndege kusafirisha wafanyakazi wao na vifaa.
Katika
makabidhiano hayo yaliyofanyika jana mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi.
Zainab Telack na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela aliiomba serikali kusaidia
kurefusha barabara ya kutua na kuruka kwa ndege kutoka Km. 1.5 hadi kufikia Km
2, ili kufanikisha utuaji wa ndege kubwa ikiwemo ya Shirika la ndege la
Tanzania (ATCL) aina ya Bombardier Q400.
“Tunashukuru
wenzetu wa ACACIA kwa kurudisha tena serikalini kiwanja hiki, lakini bado
tunaimani tutaendeleza ushirikiano baina yetu, lakini ombi langu kwa serikali
ni kuongeza urefu wa barabara ya kutua na kuruka kwa ndege ili ndege kubwa
zaidi ziweze kutua ninaimani zitachochea shughuli za kilimo, biashara na madini
na uchumi wananchi utaimarika zaidi,” alisema Bw. Mayongela.
Naye
Naibu Waziri, Mhe. Kwandikwa alisema serikali itahakikisha inasaidiana na wadau
mbalimbali ili waweze kurefusha barabara ya kutua na kuruka kwa ndege, ili
kufanikisha utuaji wa ndege kubwa za abiria na mizigo, ambazo zitachochea
maendeleo ya Wilaya ya Kahama na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla.
Hatahivyo,
Mhe. Kwandikwa aliwataka ACACIA kuweka katika mipango yao ya kusaidia ujenzi wa
upanuzi na urefushaji wa Kiwanja cha ndege cha Kahama, ili kiweze kutumika kwa
lengo la kutua kwa ndege kubwa, ambapo itachochea sera ya kukuza viwanda.
“Tunamaeneo
mengi sana hapa Shinyanga, tunawaita wawekezaji waje kuwekeza kwa wingi katika ujenzi
wa viwanda, kilimo, madini na biashara nyingine, sasa usafiri wa uhakika upo
ukizingatia tunaviwanja viwili vya ndege kikiwemo hiki cha Kahama na kile cha
Shinyanga, na malighafi, umeme na maji vipo vya kutosha hivyo waje tu
kuwekeza,” alisisitiza Mhe. Kwandikwa.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa, Bi. Telack alisema sasa mkoa wake utainuka kwa kuwa
umepata fursa ya kuongezewa kiwanja cha pili cha ndege cha Kahama, ambapo sasa
wananchi wataweza kusafirisha mazao ya kilimo na kufanya biashara na mikoa
mingine kutokana na usafiri wa ndege ni wa haraka na uhakika.
“Ninakuomba
Naibu Waziri najua hili lipo kwenye wizara yako, utusaidie kuharakisha
kumalizika kwa kiwanja cha ndege cha Shinyanga, maana hiki hapa tayari kipo ili
na sisi tuweze kupata wawekezaji katika viwanda mfano Wachina wasiende kuwekeza
mkoani Pwani pekee bali waje na huku, tunaimani tutachochea maendeleo sio ya
mkoa wetu tu ila kwa Taifa kwa ujumla,” alisema Bi. Telack.
Kwa
upande wa Meneja wa migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyahulu, Bw. Benedict
Busuzu alisema wanajivunia tukio la kurudisha kiwanja cha ndege cha Kahama kwa
serikali, ili sasa kiweze kutumika na Watanzania wote katika kuchochea ukuaji
wa viwanda.
Hata
hivyo, Bw. Busuzu ameahidi wataendelea kutoa huduma mbalimbali kwenye kiwanja
hicho kama ilivyokuwa awali, na wataendeleza ushirikiano mzuri ulipo kati yao
na TAA.
No comments:
Post a Comment