MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga leo usiku
wanacheza mchezo wao watatu wa Kundi B wa Kombe la Mapinduzi itakapochuana na Taifa
Jang’ombe kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mchezo huo utakaoanza
majira ya saa 2:15 usiku, unakuja siku moja tu baada ya Yanga kuibuka na
ushindi wa 1-0 dhidi ya JKU jana, bao la dakika ya 90 la beki Hassan Ramadhani
Kessy.
Kwa ushindi huo mwembamba, Yanga SC inafikisha pointi
sita baada ya mechi mbili, ikiwemo ya kwanza waliyoshinda 2-1 dhidi ya Mlandege
juzi na ikishinda leo itakuwa imejihakikishia kwenda Nusu Fainali hata kabla ya
mechi zake mbili za mwisho dhidi ya Zimamoto FC Januari 7 na Singida United
Januari 8.
Mechi ya kwanza leo itakuwa ni kati ya Mlandege na
Singida United Saa 8:30, kabla ya URA kumenyana na Azam FC Saa 10:30 jioni.
Baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi Jamhuri ya Pemba
kwenye mchezo wa Kundi A jana usiku, Simba itarejea Uwanja wa Amaan kesho
kumenyana na Azam FC Saa 2:15 usiku.
Ushindi wa jana uliotokana na mabao ya mabao ya
washambuliaji, Nahodha John Raphael Bocco, chipukizi Moses Kitandu na beki
Mghana, Asante Kwasi uliifanya Simba ifikishe pointi nne baada ya sare ya 1-1
na Mwenge SC katika mchezo wa kwanza.
Na baada ya mechi ya kesho dhidi ya Azam FC, Simba
watarejea Uwanja wa Amaan Januari 8 kumenyana na URA ya Uganda Saa 10:30 jioni
kukamilisha mechi zake za Kundi A.
No comments:
Post a Comment