Na Mwandishi Wetu
VINARA wa Soka Ligi Kuu Tanzania Bara Simba leo imezidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, baada ya kuibuka na
ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Kwa ushindi huo, Simba sasa imefikisha pointi 35
baada ya kucheza mechi 15 na kumaliza mzunguko wa kwanza wakiwa pointi tano
zaidi ya Azam FC iliyopo nafasi ya pili. Yanga ambayo juzi iliifunga Azam, ni ya
tatu ikiwa na pointi 28.
Simba ilipata bao la kuongoza lililofungwa na John
Bocco katika dakika ya 17 baada ya kuunganisha wavuni kona na Shiza Kichuya.
Bocco alifunga la pili katika dakika ya 26 akimalizia
kwa kichwa krosi ya Said Ndemla.
Majimaji walinyimwa penalti ya wazi katika dakika ya
19 baada ya Juuko Murshid kumchezea rafu, Geofrey Mlawala lakini mwamuzi
akasema ipigwe adhabu ndogo.
Timu hiyo ya Songea ilizinduka na kujaribu
kutengeneza nafasi mbili baada ya kulifikia lango la Simba, lakini walishindwa
kufunga.
Kilindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya
mabadiliko, ambapo ilimtoa Murshid na kumuingiza James Kotei, na kuongeza kasi
kwa timu hiyo.
Emmanuel Okwi aliiongezea Simba ushindi baada ya
kufunga bao la tatu katika dakika ya 52
baada ya mabeki wa Majimaji kushindwa kuokoa mpira wa kona uliochogwa na
Kichuya.
Okwi alifunga bao la nne likiwa la pili kwake katika
dakika ya 68 akipokea pasi safi ya Bocco, ambaye alifanya kazi ya ziada
kuwatoka mabeki wa Majimaji kabla ya kutoa pasi kwa mfungaji.
Okwi ameendelea naye kuzidi kujichimbia kileleni
katika mbio za kusaka kiatu cha dhahabu baada ya kufikisha mabao 12 hadi sasa.
Vikosi vilikuwa;Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe,
Asante Kwasi, Juuko Murshid/James Kotei, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Emannuel
Okwi, Said Ndemla, John Bocco, Shiza Kichuya/Laudit Mavugo na Jamal Mnyate.
Majimaji: Salehe Malande, Lucas Kikoti, Mpoki Mwakinyuke,
Kenned Kipepe, Paulo Maona, Hassan Hamisi, Peter Mapunda, Yakubu Kibiga,
Geofrey Mlawa/Six Mwasekaga, Maccel Bonaventure na Jafar Mohamed.
Katika mchezo mwingine, Singida United jana
walishinda bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya katika mchezo uliofanyika
kwenye Uwanja wa Namfua, Singida.
No comments:
Post a Comment