Na Mwandishi Wetu
SIMBA leo imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania
Bara baada ya kuifunga Ndanda FC mabao 2-0
katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Alikuwa ni mshambuliaji John Bocco aliyepeleka kilio kwa
Ndanda FC iliyokuwa inacheza mbele ya mashabiki wake baada ya kufunga mabao
yote mawili katika kipindi cha pili baada ya dakika 45 kumalizika kwa suluhu.
Bao la kwanza alilifungwa dakika ya 52 kwa kichwa
akiunganisha mpira wa kona iliyopigwa na Shiza Kichuya na bao la pili
alilifunga katika dakika ya 56 akitumia makosa ya mabeki wa Ndanda na kipa wao,
Jeremiah Kisubi kuzembea kuokoa mpira mrefu ulioingizwa kwenye eneo la hatari.
Ndanda walijitahidi kupeleka mashambulizi kwenye eneo la
Simba, wakiongozwa na mkongwe Mrisho Ngassa, lakini umaliziaji mbovu
ukawakosesha kupata bao la kufuta machozi.
Kwa ushindi huo, Simba inafikisha pointi 26 baada ya
kucheza mechi 12, sawa na Azam FC walio nafasi ya pili kwa kuzidiwa wastani wa
mabao.
Azam FC juzi waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya
Stand United kwenye Uwanja wao wa Chamazi Mbagala jijini Dar es Salaam.
Yanga wenye pointi
21 ambao leo wanashuka dimbani wataendelea kushika nafasi ya tatu endapo
watashinda dhidi ya Mbao FC kama watatoa sare au kupoteza na Singida United
wakishinda dhidi ya Njombe Mji FC, basi watashuka hadi nafasi ya nne.
Katika Uwanja wa Samora Iringa jana, Tanzania Prisons
waliifunga Lipuli FC bao 1-0 lililofungwa na Salum Kimenya na Mtibwa Sugar
iliifunga Majimaji mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Manundu
Turiani, Morogoro.
Kikosi cha Ndanda FC kilikuwa, Jeremiah Kisubi, William
Lucian, Abdallah Suleiman/Ayoub Masoud dakika 51, Ibrahim Job, Hamad Waziri,
Hemed Khoja/Omar Mponda dakika 61, Jacob Massawe, Majid Khamis, John Tibar/Alex
Sethi dakika 72, Jabir Aziz na Mrisho Ngassa.
Kikosi cha Simba ni Aishi Manula, Paul Bukaba, Shiza
Kichuya, Juuko Murshid, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, John Bocco, James
Kotei/Yussuf Mlipili dakika 72, Juma Luizio/Moses Kitandu dakika 54, Muzamil
Yassin na Mohamed Ibrahim ‘Mo’/Said Ndemla dakika 38.
No comments:
Post a Comment