Tuesday, 2 January 2018

Simba Waanza Kwa Sare Kombe la Mapinduzi

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MABINGWA wa kihistoria wa Kombe la Mapinduzi, Simba leo walianza vibaya mashindano hayo baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mwenge kwenye Uwanja wa Amaan hapa.

Simba waliandika bao la kwanza kupitia kwa Jamal Mwambeleko kufuatia mpira wa krosi wa Mohamed Hussein katika dakika ya pili tangu kuanza kwa mchezo huo.

Kipa wa Mwenge nusura auzawadie Simba bao la pili kutokana na uzembe wake.

Moses Kitandu muda alishindwa kuifunga Simba bao baada ya shuti lake kupaa juu katika dakika ya 17.

Katika dakika ya 28, Mwenge walipata bao la kusawazisha lililofungwa na Humudu Abrahaman Ali baada ya kupiga shuti katikati ya mabeki wa Simba na mpira kujaa wavuni.

Simba iliianza kipindi cha pili kwa kuwaingiza John Bocco, Shiza Kichuya na Nicholous Gyan waliochukua nafasi za Jamal Mwambeleko, Juma Luizi na Moses Kitandu.

Mwenge walizinduka na kulishambulia lango la Simba kwa nguvu katika dakika ya 70 na kufanikiwa kupata kona mbili.

Bocco nusura aipatie Simba bao katika dakika ya 80 lakini akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga alizubaa na mabeki wa Mwenge waliokoa.


Kikosi Simba kilikuwa; Emmanuel Mseja, Paul Bukaba, Mohamed Hussein, Yusuf Mlipili, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Ally Shomari, Said Ndemla, Juma Luizio, Moses Kitandu na Jamal Mwambeleko.

No comments:

Post a Comment