Na Mwandishi Wetu
WAKATI Simba ikishuka dimbani leo kucheza na Singida
United, mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi ameomba radhi wachezaji wenzake,
viongozi na benchi la ufundi baada ya kukosekana kwenye kikosi hicho kwa muda
mrefu bila sababu za msingi.
Akizungumza jana Kocha wa Simba, Masoud Djuma alisema
amemsamehe Emmanuel Okwi, kwani aliomba radhi kwake, kwa uongozi na wachezaji
wenzake na juzi alianza rasmi mazoezi na timu.
“Unajua binadamu hakuna aliyekamilika cha lazima ni
muunganiko wa pamoja, tukianza kunyoosheana vidole nguvu inapungua cha lazima
ni kurudisha nidhamu kwenye timu. Hakuna mchezaji au mtu yeyote ambaye yuko juu
ya timu, hata rais wa timu hayuko juu ya timu, timu inakuja kwanza halafu mtu
baadaye,” alisema Masoud.
Pia Masoud amemuombea radhi Emanuel Okwi kwa
mashabiki, akiwataka kuungana ili timu ifanye vizuri katika mchezo wa leo dhidi
ya Singida United na michezo ijayo.
Simba ambayo ilikuwa imeweka kambi mkoani Morogoro, ilirejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa
leo dhidi Singida United utakaochezwa kwenye wa Taifa.
Mchezo huo unachezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es
Salaam baada ya serikali kuruhusu kutumika kwa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara
na zile za kimataifa zilizo chini ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).
Okwi amekuwa na tabia ya kuchelewa kurudi kundini
mara anaporuhusiwa kwenda kwao Uganda kutatua matatizo ya kifamilia au
anapoitwa katika timu yao ya taifa, The Cranes, ambapo amekuwa akilalamikia na
uongozi pamoja na benchi la ufundi kwa kuvuruga ratiba ya mazoezi.
No comments:
Post a Comment