Na Mwandishi Wetu
YANGA na Azam FC zimeangukiwa kwa timu za daraja la pili
katika hatua ya 32 ya Mashindano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC), ambayo
yanatarajiwa kuchezwa Januari 31 na Februari Mosi mwaka huu.
Katika droo hiyo iliyozechezwa jana mubashara kwenye
Kituo cha Televisheni cha Azam, Yanga watasafiri kwenda Mbeya kucheza na Ihefu
FC kwenye Uwanja wa Sokoine na Azam FC itamenyana na Shupavu FC ya Morogoro
katika Uwanja wa Jamhuri.
Green Warriors iliyowatoa mabingwa watetezi, Simba
itacheza nyumbani dhidi ya Singida United katika Uwanja wa Azam Complex,
Chamazi.
KMC ya Dar es Salaam itakuwa mwenyeji wa Toto African ya
Mwanza wakati Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi utahodhi mechi mbili mfululizo za
wenyeji, Kariakoo United dhidi ya Mbao FC ya Mwanza na Majimaji Rangers dhidi
ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Majimaji FC wataikaribisha Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa
Majimaji Songea, Njombe Mji FC wataikaribisha Rhino Rangers ya Tabora katika
Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe.
Kiluvya United ya Pwani wataikaribisha JKT Oljoro ya
Arusha katika Uwanja wa Mabatini, Pwani na Ndanda FC ya Mtwara watakuwa wenyeji
wa Biashara United ya Mara katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Pamba ya Mwanza wataikaribisha Stand United Shinyanga
katika Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Polisi Tanzania watakuwa wenyeji wa
Friends Rangers ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi mkoani
Kilimanjaro.
JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Polisi Dar es Salaam na
Mwadui FC ya Shinyanga wataikaribisha Dodoma FC ya Dodoma katika Uwanja wa
Mwadui Complex, Shinyanga.
Tanzania Prisons wataikaribisha Burkina Faso ya Morogoro,
Uwanja wa Sokoine Mbeya wakati Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Buseresere FC
ya Geita katika Uwanja wa Kaitaba,
Bukoba, Kagera.
Droo hii imeshirikisha timu 32 ambapo timu nne ni za
mabingwa wa mikoa, timu tatu za Ligi
Daraja la Pili, timu 12 za Ligi Daraja la Kwanza na 13 za Ligi Kuu.
No comments:
Post a Comment