Na Mwandishi Wetu
MABAO mawili yaliyofungwa na Said Ndemla na John Bocco
‘Adebayor’ dhidi ya Kagera Sugar, leo yameirudisha Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, na kuishusha
nafasi ya pili Azam iliyokuwa imekaa nafasi hiyo kwa muda baada ya ushindi wa
mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons jana.
Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 32, katika
michezo 14 na wanatarajiwa kumaliza mzunguko wa kwanza wikiendi inayokuja kwa
kukabiliana na Majimaji Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, timu zote mbili
zilishambuliana kwa zamu na kupoteza nafasi kadhaa walizozipata, huku wachezaji
wawili wa Kagera Sugar, Juma Nyosso na Mohamed Fakhi wakioneshwa kadi za njano
kutokana na kucheza rafu mbaya kwa wachezaji wa Simba.
Kipindi cha pili Simba waliingia kwa kasi na kufanikiwa
kupata bao la kuongoza dakika ya 69, lililofungwa na Ndemla aliyemalizia pasi
murua ya Shiza Kichuya na kupiga shuti, ambalo kipa wa Kagera Sugar, Juma
Kaseja alibaki akiukodolea macho ukitinga nyavuni kwake.
Kagera Sugar walijitahidi kupambana kutafuta bao la
kusawazisha kupitia kwa washambuliaji wake, Atupele Green na Pastory Athanas,
lakini safu ya ulinzi ya Simba ilikuwa makini kuondosha hatari zote langoni
mwao.
Dakika ya 79 Bocco, aliifungia Simba bao la pili na
kuihakikishia timu hiyo ushindi akimalizia krosi nzuri iliyotokana na jitihada
kubwa za beki Shomar Kapombe aliyeingia dakika ya 71 kuchukua nafasi ya
Nicholaus Gyan.
Hiyo ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa Kapombe tangu
aliposajiliwa na Simba, akitokea Azam FC, na kabla ya kupiga krosi hiyo
alifanya kazi kubwa ya kumtambuka beki wa Kagera Sugar Adeyum Mohamed.
Chirstopher Edward wa Kagera ambaye aliigia kipindi cha
pili kuchukua nafasi ya Athanas mara kadhaa alimjaribu kipa Aishi Manula wa
Simba, lakini lengo lake lilishindikana kutokana na kipa huyo kuwa imara kwa
kudaka mashuti yote ya wapinzani wao.
Mshambuliaji Emmanuel Okwi ambaye katika mchezo uliopita
dhidi ya Singida United alifunga mabao mawili akitokea benchi, jana hakuweza
kufurukutwa baada ya kuwekwa chini ya ulinzi mkali na Juma Nyosso ingawa dakika za mwishoni mwa mchezo huo
alikaribia kufunga bao, lakini Kaseja alifanya kazi nzuri kwa kuuwahi mpira.
Wakati huo huo; timu ya Singida United nayo ililazimishwa
sare kwa kutoka sare ya kufungana 1-1 na Majimaji FC katika mchezo uliopigwa
Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
No comments:
Post a Comment