Na mwandishi Wetu
Timu ya soka ya Kiwanja cha Ndege cha
Iringa kilichopo eneo la Nduli imewafunga CRDB benki kwa magoli 2-0 katika
mchezo wa mashindano ya watumishi wa umma na binafsi yanayofanyika kwenye
uwanja wa Lugalo.
Mashindano hayo ya kwanza na ya kuvutia
yameanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi.Amina Masenza ili kuwajengea afya na
kujenga uhusiano mzuri kati ya umma na binafsi, ambapo magoli ya Kiwanja cha
ndege yalifungwa na Mwika Nyangi na Daniel Mtweve.
Timu 23 zinashiriki kwenye mashindano
hayo na zimegawanywa katika makundi manne ambapo timu ya Kiwanja cha ndege cha
Iringa inaongoza katika kundi lake la C wakijikusanyia pointi sita (6) baada ya
kushinda mechi mbili ilizocheza.
Timu nyingine zinazounda kundi C ni
pamoja na Benki ya Posta, Iringa DC, Tanesco na IDY DC, wakati kundi ‘A’ linaundwa na RAS, TANROADS, IRUWASA, TRA,
Magereza, DIRA timu za kundi ‘B’ ni Veta, Manispaa, Polisi, Kiumaki na Sido na
zinazounda kundi ‘D’ ni Zimamoto na vyuo vya RUCU, Mkwawa, Iringa, na Kleruu.
Hata hivyo bingwa wa mashindano hayo
yanayofanyika asubuhi na jioni katika viwanja vya Chuo cha Mkwawa, Kleruu,
Lugalo na Kichangani atazawadiwa sh. 350,000, wakati mshindi wa pili atapata
250,000 na watatu sh.200,000 pia kutakua na zawadi nyingine mbalimbali.
No comments:
Post a Comment