Na Mwandishi Wetu
KIKOSI cha Simba leo kitakuwa na mtihani mgumu wa kuamua
ama kucheza nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi au kurudi Dar es
Salaam kujiandaa na mechi za Ligi Kuu wakati itakapocheza na URA ya Uganda
katika mchezo wa mwisho wa makundi.
Simba yenye pointi nne katika nafasi ya tatu, inalazimika
kushinda mchezo wa leo ili kufikisha pointi saba, ambazo tayari URA wanazo
lakini wastani mzuri wa idadi ya mabao ya kufunga unawabeba vinara hao wa Ligi
Kuu ya Tanzania Bara.
Katika kundi hilo mabingwa watetezi Azam FC, tayari
wameshafuzu kwa kufikisha pointi tisa baada ya kuifunga Simba bao 1-0 juzi,
hivyo inasubiri mmoja wapo kati ya URA au Simba kuungana nayo katika hatua
hiyo.
Mchezo huo wa leo ambao umepangwa kuanza saa 10: 30
jioni, unatarajiwa kuwa na ushindani mkali, kwani URA siyo timu ya kubeza
kwenye michuano hii ilishawahi kutwaa kombe hilo miaka miwili iliyopita kwa kuwafunga Simba kwenye mchezo wa fainali.
URA ndiyo timu pekee ambayo imewafunga mabinghwa
watetezui Azam FC katika hatua ya makundi na wanaingia kwenye mchezo huo
wakihitaji sare tu ili kupata pointi moja, ambayo itawafikisha pointi nane,
ambazo haziwezi kufikiwa na Simba.
Kocha wa Simba Mrundi Masoud Djuma alisema kuwa anatambua
kibarua walichokuwa nacho katika mchezo huo, lakini ameahidi kutumia mbinu
mbadala tofauti na walizotumia kwenye mechi tatu zilizopita ili kupata ushindi
utakaowapeleka nusu fainali.
“Nimchezo mgumu ambao unatulazimisha tucheze kwa
kujitolea zaidi ili kupata matokeo, tumejipanga kufanya hivyo kwasababu tunajua
matokeo kinyume na ushindi tutakuwa tumeaga mashindano, “alisema Djuma.
Kocha huyo alisema amewaona wapinzani wao katika mechi
mbili walizocheza dhidi ya Mwenge na Azam ni timu ambayo inafungika hasa kama
watacheza mpira wa kasi na kuwashambulia mfululizo bila kuchoka.
Katika mfumo huo wachezaji Shiza Kichuya na Nicholaus
Gyan watalazimika kufanya kazi kubwa ya kukimbia na kupiga krosi kwenye eneo la
hatari ili kuwatengenezea nafasi washambuliaji wa kati John Bocco na Moses
Kitandu.
Kwaupande wake Kocha Mkuu wa URA, Nkata Paul alisema
maandalizi yao kuelekea mchezo huo yamekamilika na wanachosubiri ni kuonesha
kile walichodhamiria kukifanya katika mashindano hayo.
Nkata alisema ameiona Simba ni timu nzuri na wanacheza
kwa nidhamu kubwa hasa kwenye eneo lao la ulinzi, lakini atahakikisha
anakipanga vyema kikosi chake ili kupata ushindi kama walivyo fanya kwa Azam
Alhamisi iliyopita.
Safu ya ulinzi ya Simba ambayo inalindwa na mabeki wa
tatu kutokana na mfumo wa 3-5-2 inabidi kuwa imara kuwachunga washambuliaji wa
URA hasa Moses Sseruyide, Ssempa Charles, Kagaba Nicholas na Bokota Labama,
ambao wameonesha makali mechi zilizopita.
Baada ya mchezo huo majira ya saa 2:15 usiku, Yanga
watashuka dimbani kucheza na Singida United katika mchezo wa Kundi B zikimilisha
hatua ya makundi baada ya zote kufuzu kwa nusu fainali.
No comments:
Post a Comment