Sunday, 28 January 2018

Real Madrid Yaitisha PSG kwa Ushindi wa Mabao 4-1

PARIS, Ufaransa
KLABU ya Real Madrid imechimba mkwara kwa Paris St Germain baada ya kutoa kipigo cha mabao 4-1 dhidi ya Valencia katika mchezo wa La Liga.

Real Madrid itaikaribisha PSG Februari 14 katika mchezo wa kwanza wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya utakaofanyika kwenye Uwanja wa Santiago Bernabéu.

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha siku 280, kocha wa Real Madrid alipanga safu kali ya ushambuliaji iliyowajumuisha kwa pamoja Gareth Bale, Karim Benzema na Cristiano Ronaldo.

Safu hiyo ya ushambuliaji ilianza katika mchezo huo wakati timu hiyo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kutolewa katika mashindano ya Kombe la Mfalme dhidi ya timu ndogo ya Leganes.

Valencia iko katika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga.
Huku Real ikiwa pointi 16 nyuma ya vinara wa La Liga, Barcelona ambayo iko nje ya Kombe la Mfalme, sasa kazi imebaki katika Ligi ya Mabingwa hatua ya 16 bora.

Nacho alisema kuwa timu yao (Real) haina cha kuhofia kutoka kwa vinara hao wa Ligue 1, ambao watawakaribisha katika mchezo wa kwanza.

"Wamekuwa na mwaka mzuri, lakini sisi Real Madrid hatuhofii timu yoyote na tunawea kuifunga timu yoyote ile itakayochea dhidi yetu,”alisema Nacho.

"Mbele yetu kuna changamoto kubwa na tuko vizuri kushinda taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.”

Penalti mbili za Cristiano Ronaldo ziliipatia Real Madrid faida kabla ya mapumziko na bao la Santi Mina liliirejesha Valencia katika njia kabla ya mabao ya Marcelo na Toni Kroos.

"Unatakiwa kujua jinsi gani ya kupambana katika mchezo kama huu,”aliongeza Nacho.
"Pointi hizi tatu ni muhimu sana kwetu na zaidi ni na kikubwa ni upande wa saikolojia.”


Kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane amekuwa katika kiti moto licha ya timu yake msimu uliopita kutwaa taji la La Liga na kutetea lile la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

No comments:

Post a Comment