Na Mwandishi Wetu
AZAM FC imefanikiwa kutetea Kombe la Mapinduzi kwa mara nyingine
tena baada ya kuibuka na ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya URA ya Uganda kufuatia
kumaliza suluhu katika dakika 90 za mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa
Amaan, Zanzibar.
Shujaa wa mchezo huo na mchezaji aliyeibeba Azam hadi
kuendelea kulibeba taji hilo ni kipa Mghana, Razack Abalora aliyezuia penalti
mbili mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali
Mohamed Shein aliyekuwa mgeni rasmi katika kipute hicho.
Abalora aliye katika msimu wake wa kwanza Azam FC tangu
asajiliwe kutoka West African Football Academy (WAFA FC) ya Ghana, alipangu
penalti ya kwanza ya URA iliyopigwa na Parrick Mbowa na kuiweka timu yake
katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa kabla ya kufanya hivyo tena penalti ya
mwisho ya Brian Majwega.
Waliofunga penalti za Azam ni nahodha Himid Mao, Yakubu
Mohammed, Enock Atta Agyei na Aggrey Morris wakati Bruce Kangwa alimpelekea
mikononi mpira kipa wa URA, Alionzi Nafian na penalti za URA zimefungwa na
Charles Ssempa, Shafiq Kagimu na Jimmy Kulaba.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa mkongwe visiwani
hapa, Mfaume Nassor aliyesaidiwa na Mbaraka Haule na Dalila Jaffar, dakika 90
zilikuwa ngumu timu zote zikishambuliana kwa zamu na ziwaendee makipa wa timu
zote, Abalora na Alionzi Nafian kwa kuokoa vizuri.
Ushindi huu unamaanisha Azam FC wanatwaa Kombe la Mapinduzi
kwa mara ya nne ya rekodi, baada ya awali kulibeba pia katika miaka ya 2012,
2013 na 2017 wakiipiku Simba SC ya Dar es Salaam iliyotwaa mara tatu 2008, 2011
na 2015.
Yanga ndiye bingwa
wa kwanza wa Kombe la Mapinduzi mwaka 2007 wakati timu nyingine zilizotwaa taji
hilo ni Miembeni mwaka 2009, Mtibwa Sugar mwaka 2010 na KCCA ya Uganda mwaka
2014.
Jumla ya timu 11 zilishiriki michuano ya mwaka huu, ambazo
ni URA, Jamhuri, Mwenge, Azam na Simba zilizokuwa Kundi A na Zimamoto,
Mlandege, Yanga, JKU, Taifa Jan’gombe na Singida United zilizokuwa Kundi B.
Kikosi cha Azam FC
kilikuwa; Razack Abalora, Himid Mao, Bruce Kangwa,
Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Abdallah Kheri/Joseph Mahundi (dk59), Stephan
Kingue, Frank Domayo/Iddi Kipagwile (dk58), Salmin Hoza, Bernard Arthur/Shaaban
Iddi (dk58) na Yahya Zayed/Enock Atta-Agyei (dk64).
URA;Alionzi Nafian, Enock Kibumba, Brian Majwega, Allan
Munaaba, Patrick Mbowa, Julius Mutyaba, Nicholas Kagaba, Kalama Deboss/Charles
Ssempa (dk66), Moses Sseruyide/Peter Lwasa (dk81), Hudu Mulikyi na Shafiq
Kagimu/Jimmy Kulaba (dk82).
No comments:
Post a Comment