Sunday, 7 January 2018

Serikali yakerwa na RT kutaka kuondoa jina la Alphonce Simbu katika Michezo ya Madola 2018

Mwanariadha nyota wa Tanzania, Alphonce Simbu.
Na Mwandishi Wetu
SUALA la Riadha Tanzania (RT) kutaka kuengua jina na mwanariadha nyota wa Tanzania, Alphonce Simbu limeingia sura mpya baada ya Serikali kuingilia kati.
Katika siku za hivi karibuni Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday amekuwa akisisitiza kuwa mwanariadha huyo hatakwenda katika Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Gold Coast, Australia Aprili.

Mkurugenzi wa Maendeleo nchini, Dk Yusuph Singo alisema jana kwa njia ya simu kutoka Dodoma kuwa, ameamua kuwaita Simbu, Gidabuday na Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi ili kupata ukweli wa jambo hilo.

Singo akizungumza na gazeti hili kutoka Dodoma alisema kuwa amekuwa akisikia uvumi wa taarifa hizo, lakini anapojaribu kuwaliza RT anaambiwa wamenukuliwa vibaya.
Mkurugenzi wa Michezo nchini, Dk Yusuph Singo.
Hatahivyo, mkurugenzi alisema kuwa anajua kuna kitu kinafichwa, hivyo ameamua kuitisha kikao mara moja kati ya watu hao ili kupata ukweli halisi.

Alisema kikao hicho kinaweza kufanyikia jijini Dar es Salaam au Dodoma kutegemea na nafasi yake (Dk Singo).

Alisema kuwa akimpigia simu Gidabuday anapata jibu tofauti kwani anasema waandishi wamemnukuu vibaya na akipiga kwa wengine anapata jibu tofauti, “hivyo nimeamua kuwaita kupata ukweli kamili.”

Juzi Gidabuday alisema kuwa Kamati ya Ufundi ya RT ilikutana kwadharura jijini Dar es Salaam na kuamu kutoa jina la Simbu katika orodha ya majina ya wanariadha watakaoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola.

Alisema wameamua hivyo ili kumuwezesha mchezaji huyo kupumzika na kujiandaa kwa ajili ya London Marathon zitakazofanyika London, Uingereza Aprili ili kujipatia fedha.

Katibu Mkuu TOC, Filbert Bayi.
Alisema mwanariadha huyo atawakilisha taifa katika mashindano ya dunia ya riadha yatakayofanyika Doha mwakani na yale ya Olimpiki Tokyo, Japan 2020, ili kulipatia taifa medali za dhahabu.

Gidabuday alisema Simbu amekimbia mashindano mengi ya kuliwakilisha taifa, ambayo yana presha kubwa, sasa anahitaji kupumzika na kukimbia mashindano ya mwaliko kama London Marathon.


Hivi karibuni Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi alisema kuwa wao kama waratibu wa michezo hiyo, hawana taarifa na kutolewa kwa jina la Simbu na kuitaka RT kupeleka barua TOC kama kweli wanataka kuliondoa jina hilo.
Katibu RT, Wilhelm Gidabuday.

No comments:

Post a Comment