Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Multchoice-Tanzania Januari 4 inatarajia
kuingia mkataba mnono na Riadha Tanzania (RT) kwa ajili ya kuisaidia timu ya
taifa ya mchezo huo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam
jana, RT na Multchoice- Tanzania kupitia king’amuzi chake cha DStv watakutana
jijini Dar es Salaam na kusaini mkataba wa miaka mitatu wa mamilioni ya fedha.
Whlhelm Gidabuday |
Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday alikiri jana kwa
njia ya simu kutoka Arusha kuwa, Januari 4 watakutana na DStv na kuingia
mkataba mnono kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo ya taifa ya mchezo huo.
Pamoja na kutokuwa wazi ni kiasi gani cha fedha
kitakachotolewa na DStv, Gidabuday alisema ni mkataba mnono, ambao utaiwezesha
timu yao kujiandaa vizuri kwa mashindano mbalimbali.
Alisema mbali na kambi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola,
mkataba huo utasaidia pia maandalizi ya timu yao kwa ajili ya mashindano ya dunia
ya riadha mwaka 2019 na Michezo ya Olimpiki 2020 Tokyo, Japan.
Alisema mkataba huo utasaidia kuiwezesha Tanzania kupata
medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia ya riadha pamoja na Olimpiki,
medali ambazo bado hatujawahi kuzipata.
“Mkataba huo utatusaidia kuwaandaa wanariadha wetu
kutuletea medali za kwanza za dhahabu kutoka katika mashindano ya dunia na
Michezo ya Olimpiki, ambayo hatujawahi kuzipata, “alisema Gida.
Alisema kuwa mkataba huo wa miaka mitatu utakuwa ni wa
thamani kubwa, ambapo taarifa zingine zilidokeza kuwa ni wa zaidi ya sh milioni
700.
Gidabuday aliendelea kusisitiza kuwa RT wanauwezo wa
kuleta medali ya dhahabu kutoka katika Michezo ya Jumuiya ya Madola bila ya
kuwepo kwa nyota wa Tanzania, Alphonce Simbu.
Hivi karibuni Gidabuday alikaririwa na gazeti hili
akisisitiza kuwa, mwanariadha huyo hatakwenda Gold Coast, Australia katika
Michezo ya Madola, kwani anahitaji mapumziko baada ya kushiriki mashindano
mengi.
Alphonce Simbu |
Hatahivyo, licha ya kusema anahitaji mapuziko, lakini
inadaiwa kuwa mwanariadha huyo atashiriki London Marathon, mbio ambazo
zitafanyika Aprili mwaka huu sambamba na Michezo ya Jumuiya ya Madola.
Awali, kambi ya timu ya taifa ya riadha kwa ajili ya
Michezo ya Jumuiya ya Madola, ilipangwa kuanza Novemba mwaka jana Lushoto, Tanga
lakini hadi sasa bado haijaanza ikisubiri fedha hizo.
Taarifa zingine zinasema kuwa kambi hiyo sasa haitakuwa
Lushoto na badala yake huenda ikapigwa West Kilimanjaro, ambako ilikaa timu ya
taifa iliyoshiriki Olimpiki ya Rio na kumfanya Simbu kumaliza watano.
Simbu Januari mwaka jana alimaliza wa kwanza katika
Mumbai Marathon kabla ya kuibuka na medali ya shaba katika mashindano ya dunia
ya riadha London, Uingereza Agosti mwaka jana.
No comments:
Post a Comment