Na Mwandishi Wetu
SIMBA SC kesho Jumapili ina kibarua kigumu pale
itakaposhuka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kukabiliana na
Majimaji FC kwenye mchezo wa kukamilisha raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara
msimu huu.
Mchezo huo utakuwa ndio wa kwanza kwa kocha raia wa
Ufaransa, Pierre Lechantre kuiongoza timu hiyo ambaye hivi karibuni aliingia
mkataba wa kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo akichukua mikoba iliyoachwa wazi na
Mcameroon, Joseph Omog.
Simba inaoongoza kwenye msimamo wa ligi ikiwa na
pointi 32 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 30 huku Yanga ina pointi 28,
itahitaji ushindi kwa udi na uvumba ili kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa
kileleni.
Tangu Simba imtimue kazi Omog mwishoni mwa mwaka
jana, timu hiyo ilikuwa chini ya kocha msaidizi Masoud Djuma ambaye aliiongoza
kwenye mechi mbili za ligi na kupata ushindi mnono, iliichapa Singida United
mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa, kisha Kagera Sugar ikiwa nyumbani kwenye
Uwanja wa Kaitaba mabao 2-0.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kwa Simba kutokana
na ukweli kuwa Majimaji hawataingia kinyonge, kwani nao pointi tatu zina
umuhimu mkubwa baada ya kuwa na pointi 13 kwenye nafasi ya 11 katika msimamo wa
ligi.
Akizungumzia mchezo huo kocha Djuma, alisema kuwa si
yeye wala kocha wake mkuu, Lechantre wote hakuna anayefahamu timu hiyo vizuri,
lakini hilo haliwatishi kwani wameshapata mbinu za kukabiliana nayo.
Alisema kuwa wamekaa na kupanga mikakati yao ambayo
moja wapo ni kuingia kwa kushambulia kwa nguvu mwanzo mwisho ili kuwafanya
wapinzani wao hao wasitumie mchezo wa kupaki basi.
“Kiukweli mimi pamoja na Kocha Mkuu hakuna anayeijua
vizuri Majimaji, lakini hii haiwezi kutufanya tushindwe kupata ushindi kwao,
Simba kwa sasa inajitengenezea nafasi ya kuwa bingwa hivyo tunataka mchezo huu
tushinde ili tuzidi kuwa kwenye nafasi nzuri,” alisema Djuma.
Kwa upande wao, Majimaji yenye maskani yake Songea
mkoani Ruvuma, kupitia kwa mchezaji wao nyota, Jerry Tegete, alisema kuwa
mchezo huo kwao wanautizama kwa jicho la tatu kwani wanahitaji kuondoka na
pointi tatu ambazo zitawafanya wasogee juu kwenye msimamo wa ligi.
Alisema kuwa wanafahamu wazi kuwa wapinzani wao hao
wameonesha kiwango kizuri hivi karibuni pamoja na ujio wa kocha mpya,
utawafanya waingie kwenye mchezo huo kwa kujiamini, lakini hayo yote
hayawatishi na wanachokitaka ni kurudi Songea na ushindi tu.
“Ukiangalia ligi kwa sasa inaelekea mzunguko wa pili
ambao ni wa lala salama, tunahitaji
pointi tatu kwenye mchezio huo ambazo zitatufanya tukae sehemu nzuri wakati
ligi ikiwa inaelekea ukingoni,” alisema Tegete.
No comments:
Post a Comment