Na Mwandishi Wetu
YANGA imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam
FC ugenini katika mchezo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara uliochezwa leo kwenye
Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Hatahivyo, ushindi huo wa Yanga umeendelea kuibakiza
timu hiyo katika nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Azam baada ya kujikusanyia
pointi 28.
Washindi walishuka dimbani huku wakicheza bila ya
wachezaji wake karibu saba, ambao ni majeruhi, lakini walicheza kandanda safi.
Aidha, mchezaji wa Azam FC Abubakari Salum ‘Sure Boy’
alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumsukuma kwa makusudi, Hassan Kessy mbele
ya mwamuzi wa kati Israel Nkongo.
Azam ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika
ya tatu baada ya kuanza kwa mchezo huo likifungwa na Shaban Chilunda, huku
Obrey Chirwa akisawazisha dakika ya 30 na la ushindi likifungwa na Gadiel
Michael.
Ushindi huo umeendelea kuibakiza Yanga katika nafasi ya tatu kwenye msimamo
ikifikisha jumla ya pointi 28, nyuma ya Azam yenye pointi 30 na Simba 32.
Azam FC ilianza mpira kwa kasi na kufanikiwa kupata
bao hilo la uongozi baada ya Chilunda kutengenezewa pasi na Bruce Kangawa.
Baada ya Azam kuongoza bao hilo walianza kupunguza
kasi na kuwapa nafasi wapinzani wao kusawazisha kupitia kwa Chirwa aliyepata
pasi ya Ibrahim Ajibu ambapo alimzunguka kipa Razaki Abalora na kufunga.
Azam baada ya kusawazishiwa walirudi tena kwenye kasi
na kufanya mashambulizi mengi lakini hayakuzaa matunda, na kutoa nafasi zaidi
kwa Yanga kujiamini ambapo Gadiel alipiga shuti kali nje ya 18 na kuifungia
Yanga bao la pili.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Azam ilikuwa
ikiongoza kwa mashambulizi lakini Yanga ilikuwa mbele kwa mabao 2-1.
Kipindi cha pili Azam iliendeleza kasi ya mashabulizi
bila mafanikio kwani tayari Yanga
iliweka ukuta na kupata wakati mgumu wa kufunga. Hadi mpira unakwisha matokeo
hayo
Kocha wa Azam alijaribu kufanya mabadiliko kadhaa
lakini hayakuzaa matunda. Dakika 36 alimtoa Bernard Arthur na kumuingiza Salmin
Hoza, pia, kipindi cha pili dakika 55 na 65 alimtoa Stephen Kingue na Shaban
Chilunda na kuingia Mbaraka Yusufu na Paul Peter.
Kwa upande wa Yanga dakika ya 66 iliwatoa Emmanuel
Martin na kuingia Geofrey Mwashiuya, pia, dakika 68 alimtoa Ibrahim Ajibu na
kuingia Juma Mahadhi.
Azam FC.Razack Abalora, Himid Mao, Bruce Kangwa,
Agrey Morris, Yakubu Mohamed, Stephan Kingue, Salum Abubakari, Joseph Mahundi,
Bernard Arthur, Shaban Chilunda na Enock Atta.
Kikosi cha Yanga. Youthe Rostand, Kelvin Yondani,
Gadiel Michael, Hassan Kessy, Raphael Daud, Andrew Vicent, Said Juma, Papy
Kabamba Tshishimbi, Obrey Chirwa, Ibrahim Ajibu na Emmanuel Martin.
Mechi nyingine zilizochezwa ni Mwadui dhidi ya Njombe
waliopata sare ya mabao 2-2 na Mbeya City dhidi ya Mtibwa sare ya bila
kufungana 0-0. Na Kagera Sugar na Lipuli pia zikitoka sare ya 0-0.
No comments:
Post a Comment