Wachezaji wa Dar Swim baada ya kutwaa taji la ubingwa wa mashindano ya waogeleaji chipukizi Hopac Jijini Dar es Salaam. |
Na Mwandishi Wetu
KLABU ya kuogelea ya Dar Swim imetwaa ubingwa wa
Tanzania wa waogeleaji chipukizi wenye umri kati ya miaka 7-14 kwa mara ya pili
mfululizo baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 3,144.
Mashindano hayo yalishirikisha jumla ya timu sita,
yalimalizika Jumamosi jioni kwenye Bwawa la Kuogelea la Shule ya Heaven of Peace Academy (Hopac)
jijini Dar es Salaam.
Haikuwa kazi rahisi kwa Dar Swim Club kutwaa ubingwa
huo kwa mara ya pili mfululizo kutokana na ushindani mkubwa kutoka kwa klabu za
Taliss na Bluefins, ambazo zilionesha upinzani wa hali ya juu.
Taliss ilimaliza katika nafasi ya pili kwa
kujikusanyia pointi 2,966 huku Bluefins ikimaliza ya tatu kwa kupata pointi
2,945 na Champion Rise ikishika nafasi ya nne kwa kupata pointi 329.
Nafasi ya tano ilichukuliwa na timu ya Wahoo ya
Zanzibar kwa kupata pointi 222 na klabu
ya Mwanza International School ikimaliza ya sita kwa kupata pointi 44.
Mashindano hayo yalidhaminiwa na Kituo cha
Televisheni cha ITV, Coca Cola, Print Galore, Label Promotions, Kisima Water,
IST, JNC Events Support & Co limited, Kalu Photography na Knight Support.
Waogeaji wa kike wa klabu ya Dar Swim Club ndio
waliochangia ushindi kwa kiasi kikubwa katika mashindao hayo baada ya kuwa wa
kwanza kwa kujikusanyia pointi 1,706 na kufuatiwa na Taliss waliopata pointi
1,480 na Bluefins kwa kupata pointi
1,000.
Wahoo walishika nafasi ya nne kwa upande wa wasichana
kwa pointi 190 na kufuatiwa na Mwanza (44) na Champions Rise katika nafasi ya
sita kwa kupata pointi 30.
Kwa upande wa wavulana, klabu ya Bluefins ilishika
nafasi ya kwanza kwa kupata pointi 1,755 na kufuatiwa na Taliss (1,321) na Dar
Swim Club (1,243), Champion Rise ( 329) na Wahoo katika nafasi ya tano kwa
kupata pointi 32.
Katibu Mkuu wa DSC, Inviolata Itatiro aliwapongeza
wachezaji na makocha wa klabu hiyo kwa kufanya vyema katika mashindano hayo na
kuendelea kuwa mabingwa.
Inviolata alisema kuwa kujituma kwa wachezaji,
makocha, viongozi na wazazi kumeiletea sifa timu hiyo.
Mashindani hayo yalishirikisha jumla ya waogeleaji
chipukizi 182 walioshindana katika meta 50, 100 na 200 katika staili tano
butterfly, freestyle, breaststroke, backstroke na Individual Medley (IM).
No comments:
Post a Comment