Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga wameanza vizuri michuano
ya Kombe la Mapinduzi baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mlandege ya Unguja
katika mchezo wa Kundi B uliofanyika kwenye Uwanja wa Amaan hapa.
Mkali wa Yanga alikuwa kiungo aliyetumika kama
mshambuliaji, Juma Mahadhi aliyefunga mabao yote mawili katika kipindi cha
kwanza.
Mahadhi aliye katika msimu wake wa pili Yanga tangu
asajiliwe kutoka Coastal Union ya Tanga, alifunga bao la kwanza dakika ya sita
tu ya mchezo akimalizia pasi ya kiungo Pius Buswita na pili akimalizia krosi ya
beki Mwinyi Hajji Mngwali dakika ya 36.
Katika mchezo huo, Yanga ilipata pigo kipindi cha kwanza
baada ya beki wake, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kuumia na kushindwa kuendelea na
mchezo akikimbizwa hospitali, nafasi yake ikichukuliwa na mkongwe Nadir Haroub
‘Cannavaro.’
Kipindi cha pili pamoja na Yanga kuingia na mkakati wa
kuongeza mabao, walijikuta wakifungwa wao dakika ya pili tu tangu kuanza kwa kipindi
hicho mfungaji akiwa Omar Makame katika dakika ya 48.
Beki wa Yanga, Andrew Vincent Chikupe ‘Dante’ alitolewa
kwa kadi nyekundu dakika ya 88 pamoja na mshambuliaji wa Mlandege, Omar Makame
baada ya kugombana.
No comments:
Post a Comment