Na Mwandishi Wetu, Morogoro
TIMU ya Simba imewasili mjini Morogoro kuweka kambi ya
kujiandaa na mchezo wake ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Singida
United utakaofanyika Januari 18, kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Simba imeweka kambi katika Chuo cha Biblia, Bigwa mjini
Morogoro na jana jioni ilitazamiwa kuanza mazoezi kabambe kujiandaa na mchezo
huo unaotarajiwa kuwa wa ushindani mkali kutokana na timu zote kuwa kwenye mbio
za ubingwa.
Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi aliyekuwa kwao kwa
sababu ya mapumziko maalum aliyopewa kupata ahueni ya maumivu yake amepona na inaelezwa
kuwa amesharejea.
Kipa namba moja, Aishi Manula aliyepewa ruhusa ya kwenda kufunga
ndoa, kipa namba mbili Said Nduda aliyekuwa majeruhi, wote wako kambini
Morogoro.
Na baada ya timu kufanya vibaya kwenye michuano ya Kombe
la Mapinduzi Visiwani Zanzibar, viongozi wanatarajiwa kukutana na wachezaji ili
kuwarudishia morali iliyopotea kabla ya mchezo na Singida.
Simba inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 26, sawa na Azam
FC, wakiizidi kwa pointi tatu Singida United na tano mabingwa watetezi, Yanga
SC.
Ligi Kuu iliendelea jana baada ya mapumziko ya wiki mbili
kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo ilifikia kilele usiku na Azam FC
kutwaa taji baada ya kuifunga kwa penalti 4-3 URA ya Uganda kwenye Uwanja wa
Amaan.
Lipuli jana iliikaribisha Mtibwa Sugar na kupokea kichapo
cha bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa, huku Stand
United ikiichapa Ruvu Shooting kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga huku Ndanda
wakitoa sare ya kufungana bao 1-1 na Mbao kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona,
Mtwara.
Jumapili, mahasimu wa Jiji la Mbeya, Tanzania Prisons na
Mbeya City zitakutana kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na kesho Janauri 15,
Njombe Mji wataikaribisha Kagera Sugar FC Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe na
Jumatano, Yanga SC watakuwa wenyeji wa Mwadui FC Uwanja wa Uhuru mjini Dar Es
Salaam.
Mzunguko wa 13 utahitimishwa kwa michezo miwili Januri
18, Simba wakiikaribisha Singida United kwenye Uwanja wa Uhuru na Maji Maji
wakiwa wenyeji wa Azam FC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea.
No comments:
Post a Comment