Na Mwandishi Wetu
STANBIC Tanzania imezindua akaunti mpya ijulikanayo kama
HATUA, ambayo ni kwa ajili ya watoto, ambayo ina lengo la kuwasaidia wazazi
kuwawekea akiba watoto wao huku wakiwajengea utamaduni wa kujiwekea akiba.
Kwa kuanzishwa kwa aina hii mpya ya akaunti, Stanbic Bank
inaendelea kuwapatia wateja wake huduma mpya na bora za kibenki kila siku
kuendana na mahitaji ya wateja na hali halisi ya soko.
Mtoto akifanya muamala katika mashine ya ATM ya Stanbic Bank wakati wa uzinduzi wa akaunti ya HATUA juzi. |
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa akaunti hiyo
uliofanyika katika Makao Makuu ya benki hiyo Kinondoni jijini Dar es Salaam
mwishoni mwa wiki, mkuu wa mauzo wa benki hiyo, Shangwe Kisanji amesema kuwa
benki hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuwapatia wateja wake huduma mpya
kila mara na nyakati zote huduma hizo huendana na mahitaji ya wateja na
mahitaji ya jumla ya soko la huduma za kibenki hapa nchini.
“Wakati wote tumekuwa tukiangalia njia mbalimbali za
kuwahudumia vyema wateja wetu katika kutunza fedha zao, ikiwemo kuwawekea watoto akiba kwa manufaa yao
ya baadae na pia kuwajengea utamaduni wa kujiwekea akiba wawapo wakubwa,
utamaduni ambao ni muhimu sana kwa uchumi na maisha yao”.
Ameeleza kuwa akaunti hiyo ya HATUA ni muendelezo mzuri
wa kuwatoa watoto kwenye utamaduni wa kujiwekea akiba kwenye vibubu na badala
yake kuanza utamaduni wa kujiwekea akiba kwa njia rasmi zaidi.
Amesema akaunti hiyo haina makato ya huduma na kiwango
cha chini cha amana ni sh 20,000 tu.
Amebainisha kuwa akaunti hiyo haina masharti magumu ya
kuiendesha na inaruhusu kutolewa kwa
fedha mara moja kwa robo ya mwaka ili kusaidia katika majukumu yanayowahusu
watoto kama vile ada za shule, sare na kadhalika. Amesema pia akaunti hiyo
hujipatia riba kulingana na amana iliyopo.
No comments:
Post a Comment