Na Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga
jana walipunguzwa kasi baada ya kulazimishwa suluhu na Mwadui ya Shinyanga
katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kwa sare hiyo, Yanga imeendelea kupiga kwata katika
nafasi ya tano ya msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 22, moja nyuma ya
Singida United iliyopo katika nafasi ya nne.
Simba na Azam FC ambazo zinashika nafasi ya kwanza na
pili kila moja ikiwa na pointi 26, leo zina nafasi ya kuzidi kuikimbia Yanga
endapo zitashinda mechi zao.
Simba wanacheza dhidi ya Singida jijini Dar es Salaam
wakati Azam FC watatoana jasho dhidi ya Majimaji ya Songea mjini humo.
Katika mchezo huo wa jana, Yanga nusura ipate bao
katika dakika ya 23, pale Emmanuel Martin baada ya kuingia ndani ya 18, lakini
kabla hajaleta madhara, mabeki wa Mwadui walifanikiwa kumdhibiti.
Dakika ya 32, Amis Tambwe alipata nafasi nzuri ya
kufunga, lakini alipiga mpira pembeni kabla Paul Nonga hajashindwa kufunga
katika dakika ya 33 baada yakupiga shuti lilodakwa na kipa wa Yanga, Youthe
Rostand.
Mashabiki wa Yanga hawakufurahishwa na matokeo hayo,
ambapo baadhi yao walipiga kelele kuwa hawamtaki kocha msaidizi wa timu hiyo,
Shadrack Nsajigwa.
Nsajigwa amekuwa akikaa katika benchi la timu hiyo
baada ya kocha mkuu, George Lwandamina wa Zambia kwenda kwao kwa ajili ya msiba
wa mtoto wake.
Hatahivyo, Lwandamina amesharejea nchini na jana
alikuwepo jukwaani kwenye Uwanja wa Uhuru wakati Yanga ikicheza na Mwadui.
Vikosi vilikuwa Yanga:Youthe Rostand, Hassan Kessy,
Mwinyi Haji, Andrew Vicent, Kelvin Yondan, Said Juma, JUma Mahadhi, Pius
Buswita, Amis Tambwe, Ibrahim Ajibu na Emmanuel Martin.
Mwadui: Anord Massawe, Jackson Salvatory, David
Luhende, Joram Mgeveke, Idd Mfaume, Awadhi Juma, Jean Girukwishako, Abdallah
Omary, Paul Nonga, Evangestus Bernard na Awese Awese.
No comments:
Post a Comment