PARIS, Ufaransa
MWAMUZI wa kati Tony Chapron ambaye anadaiwa kumpiga teke
mchezaji wa Nantes nchini Ufaransa kabla ya kumtoa nje kwa kadi nyekundu wakati
timu hiyo ilipocheza dhidi ya Paris St-Germain (PSG), amesimamishwa kazi.
Chama cha Soka cha Ufaransa kimetangaza kwamba mwamuzi
huyo amesimamishwa kazi kwa muda usiojulikana "hadi uamuzi mwingine utakapotolewa."
Beki Diego Carlos alimgonga mwamuzi Tony Chapron kwa
bahati mbaya katika kisigino wakati wakikimbilia ulipo mpira dakika za mwisho
mwisho kabla mchezo huo wa Ligue 1 ya Ufaransa haujamalizika.
Chapron alimpiga teke mchezaji huyo na kisha akampa kadi
ya pili ya njano kwa sababu ya kulalamika.
Katika mchezo huo, PSG walishinda mechi hiyo kwa bao 1-0.
Nantes wanataka kadi hiyo ibatilishwe kwani
isipobatilishwa atakosa mechi moja.
Chama cha Soka cha Ufaransa kimesema kuwa chama cha
waamuzi kimeamua "kumuondoa Tony Chapron ambaye alikuwa ameteuliwa
kusimamia mechi ya Ligue 1 Jumatano kati ya Angers na Troyes, hadi wakati
mwingine".
Wameongeza: "Chapron karibuni ataitwa katika Kamati
ya Nidhamu ya LFP [Ambao ni Wasimamizi wa Ligi Ufaransa].
"Mwamuzi huyo baada ya kuangalia kwa kina video ya
tukio hilo, alikiri kuwa aliangushwa kwa bahati mbaya na halikuwa kusudio la
mchezaji huyo.”
Mwenyekiti wa Nantes Waldemar Kita alisema Chapron anafaa
kupigwa marufuku kwa miezi sita kwa sababu ya uamuzi huo wenye utata.
Ameongeza kuwa: "Sitaki kukubali kuwa mwamuzi huyo alikusudia kufanya hivyo."
No comments:
Post a Comment