Friday, 25 August 2017

Kiwanja cha JNIA Terminal 3 kufungwa mitambo ya kisasa kubaini waliomeza dawa za kulevya

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Salim Msangi akizungumza na Kamati ya  Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar waliotembekea mradi wa ujenzi wa Terminal 3 jijini Dar es Salaam leo.

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege (TAA) imesema itafunga mitambo ya kubaini watu waliomeza dawa za kulevya katika jengo la abiria namba tatu (Terminal III) kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Hatua hiyo ni katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya na kuhakikisha hakuna dawa zinazopitishwa kupitia uwanja huo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Salim Msangi (kushoto) akielezea jambo wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar 
 Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Salim Msangi wakati akijibu maswali mbalimbali ya wajumbe wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar waliotembekea mradi wa ujenzi wa jengo hilo leo.

Msangi alisema, mbali na mtambo huo kufungwa katika kiwanja huo ili kuhakikisha hakuna dawa zinazopitishwa lakini pia taasisi nyingine mbalimbali ikiwemo za madini zitakuwa na nafasi katika uwanja huo ili kuhakikisha hakuna madini yanayotoroshwa kwenda nje ya nchi.

"Ni jengo la aina yake kwa kweli, kwa sababu tunataka Airport ya Dar es Salaam iwe ni kiunganishi cha kwenda sehemu nyingine lakini pia kwa kuwa tunafufua shirika letu la ndege iwe ni sehemu ambapo safari zinaanzia hapa na kwenda kuchukua watu katika nchi mbalimbali na kuwaleta hapa," alisema.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wakitembelea Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) Terminal 3 leo jijini Dar es Salaam

Msangi alisema, hatua hiyo itasaidia kuongeza fedha za kigeni na mapato kwani ndege zilizonunuliwa na serikali zitaweza kwenda katika nchi mbalimbali na hivyo kuleta watalii nchini.
Aidha, alisema sambamba na mradi huo pia wana mpango wa kujenga hoteli ya kisasa karibu na uwanja huo ili kuwarahisishia abiria na wageni ambao wanapenda kukaa karibu na uwanja wa ndege.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar, Mohamed Ahmed Salim alisema, kupitia ziara hiyo wamejifunza mambo mengi ambayo wataenda kuangalia namna ya kuyaweka katika mradi wa ujenzi wa jengo la abiria namba mbili (Terminal II) katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar.
Alisema mradi huo awali ulikwama kutokana na changamoto mbalimbali lakini kwa sasa wameshafikia muafaka na kwamba ujenzi utaanza muda wowote kuanzia sasa na utachukua miezi 18.

"Kwa mwaka jana uwanja ule umehudumia wageni miliomni moja, tulikuwa tunalenga kujenga jengo litakalohudumia abiria milioni moja nukta mbili lakini kwa kuangalia idadi ya watalii inavyoongeza na dira ya maendeleo tukasema ni bora jengo la kuhudumia abiria milioni moja nukta sita," alisema Salum.
Alisema hatua hiyo ilisababisha kuchelewa kuanza kwa ujenzi kwa kuwa walikuwa kwenye majadiliano ya wafadhili wa mradi huo ambao ni China kupitia Benki ya Exim China.

Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hamza Hassan Juma alipongeza maendeleo ya ujenzi huo pia kupongeza hatua ya serikali kujenga awamu ya pili kwa kutumia fedha za ndani.


"Hii ni nzuri sana, kwasababu inaonesha kuna mambo tunaweza sisi wenyewe, bila kutegemea misaada. Pia tumejifunza mengi tukirudi Zanzibar tutaishauri serikali," alisema Juma.
 


Wednesday, 23 August 2017

Yanga wasaka kufuta uteja wa kufungwa na Simba

Na Mwandishi Wetu

TIMU za Yanga na Simba leo zinashuka kwenye Uwana wa Taifa kucheza mchezo a Ngao ya Jamii ikiwa ni uzinduzi rasmi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2017/18 utakaoanza wikiendi ijayo.

Hii ni mechi ya tatu kwa kocha wa Yanga, Mzambia George Lwandamina kukutana na watani zake za jadi Simba, huku kocha huyo akifungwa mara mbili na watani hao tangu alioanza kuifundisha Yanga.

Huo utakuwa mchezo wa tatu kwa Mzambia, George Lwandamina tangu achukue nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm Desemba mwaka jana na mechi mbili zilizopita zote alipoteza. 

Januari 10, mwaka huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar Yanga ilifungwa kwa penalti 4-2 na Simba baada ya sare ya 0-0 katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi.

Februari 26, mwaka huu, Simba ikatoka nyuma na kushinda 2-1 kwa mabao ya Mrundi Laudit Mavugo dakika ya 66 na Shiza Kichuya dakika ya 81, baada ya Simon Msuva kuanza kuifungia Yanga kwa penalti dakika ya tano.

Na mechi zote Lwandamina amefungwa na Simba ikiwa chini ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog akisaidiwa na Mganda, Jackson Mayanja ambao wote leo watakuwepo kwenye benchi la Simba,

Katika benchi la Yanga kuna mabadiliko kidogo, kocha msaidizi wa msimu uliopita, Juma Mwambusi hayupo na nafasi yake imechukuliwa na beki na nahodha wa zamani wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa.

Kwenye benchi la Simba, ameondoka kocha wa makipa Mkenya, Iddi Salim na nafasi yake kuchukuliwa na golikipa wa zamani wa timu hiyo, Muharami Mohammed Shilton.

Kiungo Haruna Niyonzima leo ataibukia kwa mahasimu Simba, baada ya miaka sita ya kucheza Yanga tangu alipojiunga nayo mwaka 2012 akitokea APR ya Rwanda. Yanga pia haitakuwa mchezaji wake mahiri na aliyekuwa tegemeo katika safu ya ushambuliaji, Simon Msuva aliyehamia Difaa Hassan El- Jadida ya Ligi Kuu ya Morocco.

Mshambuliaji Ibrahim Hajib naye leo ataibukia kwa watani, Yanga baada ya kuibukia timu ya vijana ya Simba na kupandishwa kikosi cha kwanza cha timu hiyo alikopatia umaarufu. Simba pia haitakuwa na beki wake, Abdi  Banda aliyehamia Baroka FC ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Timu zote zilikuwa kambini upande wa pili wa Muungano wa Tanzania kwa wiki nzima Yanga walikuwa kisiwani Pemba na Simba walikuwa Unguja na kabla ya mchezo wa leo, kila timu imecheza mechi sita za kujipima na kila moja ilipoteza mchezo mmoja.

Simba ilifungwa 1-0 na Orlando Pirates, kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Bidvest Wits nchini Afrika Kusini, ikashinda 1-0 na Rayon Sport ya Rwanda, 1-0 na Mtibwa Sugar, 0-0 na Mlandege na kumalizia kwa ushindi wa 5-0 dhidi ya Gulioni FC, wakati Yanga ilishinda 5-0 na Moro Kids, 3-2 na Singida United, ikafungwa 1-0 na Ruvu Shooting, ikashinda 2-0 na Mlandege, 1-0 na Chipukizi na 1-0 na Jamhuri.   

Mara ya mwisho Yanga kuifunga Simba ilikuwa ni Februari 20, mwaka 2016 ushindi wa 2-0 uliotokana na mabao ya mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma dakika ya 39 na Amissi Tambwe dakika ya 72, ambao kwa pamoja leo wanatarajiwa kuiongoza tena timu hiyo.

REKODI YA SIMBA NA YANGA NJE YA LIGI KUU:

NANI MTANI JEMBE:

DESEMBA 13, 2014

Simba SC 2-0 Yanga

WAFUNGAJI:

SIMBA SC: Awadh Juma na Elias Maguri

NANI MTANI JEMBE:

DESEMBA 23, 2013

Simba SC 3-1 Yanga

WAFUNGAJI:

SIMBA SC: Amisi Tambwe dk 14 na 44penalti na Awadh Juma dk,

YANGA SC: Emmanuel Okwi dk87 

KLABU BINGWA AFRIKA MASHARIKI NA KATI:

JULAI 10, 2011

Yanga 1-0 Simba, Fainali

MFUNGAJI : Kenneth Asamoah dk 108

JANUARI 1975

Yanga Vs Simba; Fainali, 2-0

WAFUNGAJI: Gibson Sembuli na Sunday Manara

JANUARI 1992

Simba Vs Yanga; Fainali

1-1, Simba ilishinda kwa penalti 5-4

JULAI 27, 2008

Simba Vs Yanga; Mshindi wa Tatu

(Yanga haikutokea uwanjani, Simba ikapewa ushindi wa chee)

KOMBE LA HEDEX:

JUNI 30, 1996

Yanga Vs Simba 2-0

CCM Kirumba, Mwanza

WAFUNGAJI: Bakari Malima na Edibily Lunyamila

KOMBE LA HEDEX:

JULAI 13, 1996

Simba Vs Yanga 1-1, Taifa, Dsm

WAFUNGAJI:

SIMBA: Hussein Amaan Marsha kwa penalti

YANGA: Bakari Juma Malima

KOMBE LA TUSKER:

FEBRUARI 10, 2001

Yanga Vs Simba (fainali) 0-0

(Simba ilishinda kwa penalti 5-4, Uwanja wa Taifa)

MACHI 31, 2002.

Simba Vs Yanga 4-1

WAFUNGAJI:

SIMBA: Mark Sirengo dk. 3 na 76, Madaraka Selemani dk. 32 na Emanuel Gabriel dk. 83.

YANGA: Sekilojo Chambua dk 16.

(Mechi hii ya fainali iliyohudhuriwa na rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, chupuchupu ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka kufunga bao ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa. Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za maji na mashabiki wa Yanga. Mwamuzi wa mchezo huo, Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza mchezo. Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia mchezo huo. Baada ya hapo, alifungiwa na Chama cha Soka Tanzania, FAT).

JULAI 2, 2005

CCM Kirumba, Mwanza. Fainali

Simba Vs Yanga, 2-0

WAFUNGAJI: Emmanuel Gabriel dk. 60, Mussa Hassan Mgosi dk. 72

AGOSTI 15, 2006

Simba Vs Yanga; Nusu Fainali, 1-1

WAFUNGAJI:

SIMBA: Emanuel Gabriel dk. 69

YANGA: Credo Mwaipopo 90

(Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti 7-6)

DESEMBA 24, 2009

Yanga Vs Simba; Nusu Fainali, 2-1

WAFUNGAJI:

YANGA: Jerry Tegete dk 67, Shamte Ally dk 120

SIMBA: Hillary Echesa dk 78 (penalti)

(Uwanja wa mpya wa Taifa)

KOMBE LA MAPINDUZI:

Januari 10, 2017; Nusu Fainali

Simba 0-0 Yanga

Simba ilishinda kwa penalti 4-2

JANUARI 12, 2011

Simba Vs Yanga; Fainali 2-0

WAFUNGAJI: Mussa Mgosi dk 33, Shijja Mkinna dk 71

(Uwanja wa Amaan, Zanzibar)

KOMBE LA AICC:

JUNI 1989

Yanga Vs Simba SC 1-0

MFUNGAJI: Joseph Machella

APRILI 20, 2003,

CCM Kirumba, Mwanza

Yanga Vs Simba 3-0

WAFUNGAJI:

Kudra Omary dk. 30, Heri Morris dk 32 na Salum Athumani dk. 47

KOMBE LA CCM

JANUARI 19, 2003

Simba Vs Yanga 1-1, Dsm

WAFUNGAJI:

SIMBA: Jumanne Tondolo dk. 10

YANGA: Mwinyi Rajabu dk. 20

NGAO YA JAMII:

FEBRUARI 17, 2001

Yangs Vs Simba 2-1, Dsm

WAFUNGAJI:

YANGA: Edibilly Lunyamila dk. 47, AllyYussuf 'Tigana' dk 80.

SIMBA: Steven Mapunda 'Garrincha' dk.43

AGOSTI 18, 2010

Yanga vs Simba 0-0

(Yanga ilishinda kwa penalti 3-1)

WAFUNGAJI: Geoffrey Bonny, Stefano Mwasyika na Isaac Boakye kwa upande wa Yanga na Mohamed Banka kwa Simba.

WALIOKOSA: Ernest Boakye kwa Yanga na Emanuel Okwi, Uhuru Suleiman na Juma Nyosso kwa Simba.

AGOSTI 17, 2011

Simba vs Yanga 2-0, Dar

WAFUNGAJI:

Haruna Moshi Boban dk 15 na Felix Sunzu dk 38.

KOMBE LA FAT

NOVEMBA 15, 2000

Yanga Vs Simba 2-1

Sheikh Amri Abeid, Arusha.

WAFUNGAJI:

YANGA: Aziz Hunter 40 na Vincent Tendwa

SIMBA: Ally Yussuf 'Tigana' dk.37

NOVEMBA 12,  2000

MARUDIANO KOMBE LA FAT

Simba Vs Yanga 1-0, Dsm

MFUNGAJI:

SIMBA: Ben Luoga  dk.44       

(Matokeo ya jumla yakawa 2-2 na Yanga ikatolewa kwa mikwaju ya penalti 5-4)


Viwanja vinne vya ndege kuwekewa rada za kisasa

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akisikiliza wataalam alipotembelea jengo la Tower kabla ya kuingia mkataba wa ufungaji wa Rada nne katika viwanja vya ndege nchini. Mwenye tai nyekundu Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Salim Msangi.



Thursday, 17 August 2017

JKT yawapongeza wanariadha wake walioshiriki mashindano ya dunia London na kurudi na medali

Wanariadha wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walioshiriki mashindano ya dunia ya riadha kutoka kushoto ni Alphonce Simbu, Magdalena shauri, Emmanuel Giniki na Stehano Huche wakati wa hafla ya kuwapongeza iliyofanyika Makao Makuu ya JKT Mlalakua leo.
Na Mwandishi Wetu
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limesema kuwa baada ya mwanariadha Alphonce Simbu kurejea na medali kutoka katika mashindano ya 16 ya riadha ya dunia London, Uingereza, wakati umefika kwa wadau kuangalia na michezo mingine ili kulitangaza taifa zaidi.

Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Michael Isamuhyo aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya kumpongeza mwanariadha Simbu aliyetwaa medali ya shaba katika mashindano hayo ya dunia kwa upande wa marathoni na wenzake.
Mkuu wa JKT, Meja Jenerali, Michael Isamuhyo akipokea saluti kutoka kwa Serviceman, Alphonce Simbu.
Tanzania katika mashindano hayo ilipeleka wanariadha nane, wanne akiwemo Simbu ni waajiriwa wa JKT. Wengine ni Magdalena Shauri, Stephano Huche na Emmanuel Giniki, ambao nao walikuwemo katika hafla hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi hilo Mlalakua jijini Dar es Salaam.
Isamuhyo alisema kuwa wakati umefika kuangalia na michezo mingine kama ngumi, mpira wa wavu, kuogelea, netiboli na mingine ili nayo iweze kufanya vizuri na kusaidia kuitangaza nchi nje ya mipaka yake.
Hatahivyo, mkuu huyo alisisitiza kuwa Desemba jeshi lake litaongeza wanariadha ili kuhakikisha wanakuwa wengi na kuongeza changamoto katika kambi ya timu hiyo.

Alisema kuwa ana matumaini makubwa kuwa wanariadha hao pamoja na wengine wa Tanzania watafanya vizuri katika mashindano makubwa yajayo.
Aliongeza kuwa wadau wote washirikiane na kuondoa migongano isiyo ya lazima na JKT wako tayari kuwatoa wanariadha hao wakati wowote ili mradi watumike vizuri kwa ajili ya maslahi ya kitaiffa na sio binafsi.
Mkuu wa JKT, Meja Generali, Michael Isamuhyo akisalimiana na mwakilishi wa MultichoiceTanzania, Johnson Mshana huku Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja akishuhudia leo Mlalakua jijini Dar es Salaam.
Johnson Mshana akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Multichoice-Tanzania, Maharage Chande alisema kuwa watakaa na Simbu ili kujadili mkataba mpya baada ya ule wa awali mwaka mmoja kumalizika baadae mwezi huu.

DStv iliingia mkataba wa mwaka mmoja, ambapo kila mwezi alikuwa akipewa sh milioni 1 kwa ajili ya kujikimu na mkataba mpya unatarajiwa kuwa mnono zaidi ya huo.

Simbu naye aliishukuru JKT, Multichoice-Tanzania, BMT, Riadha Tanzania (RT) kwa mshirikiano na mshikamano waliouonesha hadi kufanikisha ushindi huo wa Tanzania katika mashindanohayo makubwa, ambao alitaka mshikamano huo kuongezeka.
Naye Katibu wa BMT, Mohamed Kiganja alisema kuwa bila majeshi hakuna mafanikio yoyote katika michezo, kwani majeshi yamekuwa na nidhamu kubwa ya kuwalea wachezaji na kuhakikisha wanafanya vizuri.

Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday alisema kuwa analishukuru jeshi kwa kuwalea wanariadha hao na kutaka kuwachukua na wanariadha wengine ili kuleta changamoto katika timu yao ya riadha.

 





 









Service Girl, Magdalena Shauri akimrekebisha kofia Serviceman Alphonce Simbu wakati wa hafla ya kuwapongeza wanariadha hao na wenzao walioshiriki mashindano ya dunia ya riadha London, Uingereza.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Michael Isamuhyo akisalimiana na mwandishi wa The Citizen, Majuto Omary. Katikati ni Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja.