Wednesday, 8 June 2016

Stephen Keshi afariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wa moyo



Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan (kushoto) akimpa tuzo Stephen Keshi baada ya kuiwezesha Super Eagles kutwaa taji la Afcon 2013 .

ABUJA, Nigeria

KOCHA wazamani wa timu ya taifa ya Nigeria ya Super Eagles, Stephen Keshi, mwenye umri wa miaka 54, amefariki duniani.

Nahodha huyo wazamani wa timu ya taifa ya Nigeria, ni mmoja wa watu wawili waliowahi kutwaa taji hilo akiwa mchezaji na kocha.

Pia aliiongoza Togo na Mali, na wakati akicheza aliwahi kuichezea klabu ya Ubelgiji ya Anderlecht.

Alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo, viliripoti vyombo vya habari vya hapa.

Akiwa mchezaji, Keshi alikuwa sehemu ya wachezaji wa Super Eagles waliotwaa taji la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 1994 na nusura watinge robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka huo huo.

Aliifundisha timu ya taifa kwa miaka mitatu, akiiongoza kutwaa taji la Afcon 2013 Afrika Kusini na kucheza hatua ya 16 bora katika fainali za Kombe la Dunia Brazil 2014.

Mkataba wake auliongezwa baada ya Kombe la Dunia lakini baadae alikuwa akipewa kibarua kila timu hiyo ilipokuwa na mechi baada ya kushindwa kutinga fainali ya Mataifa ya Afrika mwaka 2015.

Baadae alitimuliwa kama kocha wa muda, lakini aliitwa tena baada ya rais wa nchi hiyo Goodluck Jonathan kuingilia. Alitimuliwa kwa mara ya mwisho Julai mwaka jana.

Keshi, aliyeshinda taji la Mataifa ya Afrika akiwa mchezaji na kocha, alifariki dunia katika jiji la Benin City kwa kile kinachodaiwa ni matatizo ya moyo.

Monday, 6 June 2016

Air Zimbabwe yazindua tena safari za kuja Tanzania lengo likiwa ni kuimarisha ushirikiano zaidi



Ndege ya air Zimbabwe ikitua kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya miaka saba tangu ilipotua mara ya mwisho kwenye uwanaja huo.
Na Mwandishi Wetu
USHIRIKIANO wa Tanzania na Zimbabwe katika utalii utaongezeka zaidi baada ya ndege ya Air Zimbabwe kurejesha tena safari za kuja nchini baada ya kuacha kuja kwa takribani miaka saba sasa.

Kwa mara ya mwisho ndege ya nchi hiyo ilikuja nchini mwaka 2009 huku ile ya Tanzania, Air Tanzania ilitua katika ardhi ya Zimbabwe kwa mara ya mwisho mwaka 2004, ikiwa ni miaka 12 sasa.
 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Faustine Kamuzora aliyemuwakilisha waziri wa wizara hiyo, Profesa Makame Mbarawa aliipongeza Air Zimbabwe kwa kuanza tena safari zake huku ikiinua sekta ya utalii.

Alisema ndege hiyo itasaidia wanaotaka kutembelea vivutio vya utalii kama Maporomoko ya Victoria, Mlima Kilimanjaro, Ngorongoro na Zimbawe sasa wataweza kusafiri moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili.
 
Ndege hiyo itakuwa inakuja nchini mara mbili kwa wiki, Jumanne na Jumamosi.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Kimataifa wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA),Waziri wa Uchukuzi, Maendeleo ya Miundombinu wa Zimbabwe, Dr Jorum Gumbo alisema kuanza tena safari za ndege hiyo kutasaidia sana kukuza utalii na kuinua uchumi wan chi hiyo.

Kikundi cha Utamaduni cha Jeshi la Kujenga taifa (JKT) kikicheza ngoma wakati wa kuikaribisha ndege ya Air Zimbabwe kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Alisema watalii wanaokuja Tanzania na Zanzibar sasa watakuwa na nafasi ya kwenda moja kwa moja Zimbabwe kwa kutumia ndege, tofauti na huko nyuma iliwabidi kupitia nchi zingine, kitu ambacho ni gharama kubwa.

Baadhi ya wafanyakazi wa Ubalozi wa Zimbabwe wakishuhudia ndege ya nchi yao ilipozindua safari zake za kuja Tanzania juzi kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.
Balozi wa Zimbabwe nchini Tanzania, Edzai Absalom Chimonyo alisema kumekuwa ndege hiyo itasaidia sana kusafirish watalii, wafanyabiashara na watu wa kawaida kusafiri kati ya nchi hizo mbili kwa shughuli mbalimbali.

Alisema Wazimbabwe wamekuwa wakitumia sana bandari ya Dar es Salaam, ambapo mbali na shughuli zingine, pia wamekuwa wakiingiza magari zaidi ya 300 kwa mwezi kupitia bandari hiyo.

Waziri wa Uchukuzi, Maendeleo ya Miundombinu wa Zimbabwe, Dr Jorum Gumbo (kushoto) akisalimiana na balozi wa Zimbabwe nchini Tanzania,Edzai Absalom Chimonyo.Wa pili kulia ni
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Faustine Kamuzora.
"Karibu magari 300 yamekuwa yakichukuliwa kutoka bandari ya Dar es Salaam na kupelekwa Zimbabwe kila mwezi, “alisema akionesha umuhimu wa Air Zimbabwe kurejesha tena safari zake nchini Tanzania.
 

Friday, 3 June 2016

Kaimu Mkurugenzi wa kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ahimiza usafi





Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Laurent Mwigune (mwenye suti) akishiriki zoezi la kufanya usafi jana maeneo mtaa wa Kigilagila Relini, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la usafi kuelekea Siku ya Mazingira Duniani, Juni 5, 20916.
Na Mwandishi Wetu
KAIMU Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha amehimiza usafi maeneo yanayozunguka kiwanja hicho, ili kuepusha kuzaliana kwa ndege wanyama wa aina mbalimbali.

Rwegasha aliyasema hayo wakati akimwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Mhandisi George Sambali jana wakati wa kufanya usafi wa mazingira ulioongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu,Bw. Laurent Mwigune kwa wafanyakazi wa TAA kushirikiana na wakazi wa mtaa wa Kigilagila Relini ikiwa ni muendelezo kuelekea kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, Juni 5, 2016.

Alisema uchafu unachangia ongezeko la ndege wanyama ambao ni hatari kwa ndege za abiria.

Ndugu zangu tusiruhusu mazingira yetu yakawa machafu, kwani ni hatari kubwa kwa sisi kiwanja cha ndege, kwani ndege mnyama akiingia kwenye injini ya ndege ya abiria atasababisha hasara kubwa.

Wafanyakazi Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) katika picha ya pamoja na
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu,

Laurent Mwigune(watatu kutoka kushoto waliochuchumaa), mara baada ya kumaliza kufanya usafi eneo la Kigilagila jijini Dar es Salaam jana.
Hivyo tujitahidi kufanya mazingira yetu yawe safi ili ndege kama kunguru na wengine wasizaliane hapo kwani wanaweza kuleta madhara, alisema Rwegasha.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo iliyotolewa Kitaifa na Mhe January Makamba , Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ni Tuhifadhi Vyanzo vya Maji kwa Uhai wa Taifa letu.

Alimtaka Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigilagila Relini na Vituka kuhakikisha dampo lisilo rasmi lililoanzishwa karibu na ukuta wa JNIA linaondolewa haraka, na waweke ulinzi kuzuia utupaji wa taka eneo hilo.

Aidha, alisema TAA imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na majirani zake wanaozunguka JNIA, ili kuweka mazingira hayo katika hali ya usalama na usafi, lakini bado wapo wakazi wachache wanaosababisha uhusiano huo kulegalega kwa kufanya vitendo vya kutupa taka hovyo.

Alifafanua zaidi kuwa TAA inaendelea na zoezi la kufyeka vichaka vilivyozunguka JNIA, ili kuzuia uhalifu wa watu wabaya kutumia mwanya huo kuruka uzio na kuingia ndani ya kiwanja hicho.

Sisi hatutanii tena tunaagiza hili dampo liondoke na tutaweka mabango ya kuzuia utupaji wa taka hapa, na Wenyekiti tunaomba mhakikishe mnawakamata wale wote watakaokiuka agizo hilo na tutawachukulia hatua za kisheria, alisema Rwegasha.