Sunday, 24 April 2016

Wakenya watamba London Marathon 2016 baada ya kushika nafasi za kwanza kwa wanawake na wanaume



LONDON, Uingereza

WAKENYA leo wametamba katika mbio za London Marathon baada ya kushika nafasi ya kwanza kwa upande wa wanawake na wanaume.

Kwa upande wa mademu, Jemima Sumgong ameshinda mbio hizo licha ya kudondoka wakati akishindana katika shindano hilo.

Mwanariadha huyo (31) alianguka na kugonga kichwa chini baada ya kusukumwa na mwanariadha wa Ethiopia Aselefech Mergia wakati wakiwa wanakaribia katika sehemu ya maji.

Lakini licha ya dhahama hiyo bado mwanadada huyo alisimama na kuendelea kukimbia akiwa pamoja na kundi hilo la wanariadha wenzake.

Alionesha umakini mkubwa na kuwastaajabisha watu baada ya kuwashinda wanariadha hao na kisha kuchukua taji lake hilo la kwanza kwa kutumia muda wa saa 2 dakika 22 na sekunde 58.

Pia mwanariadha Tigist Tufa wa Ethiopia ambaye alikuwa bingwa wa mwaka 2015 aliibuka wa pili katika shindano hilo akiwa nyuma ya mshindi kwa sekunde tano tu.

Katika michuano hiyo bado Wakenya walionekana kutamba zaidi kwa kuwa hata mshindi wa tatu alitokea Kenya ambaye ni Florence Kiplagat.

Wakati huo huo, mwanariadha Eliud Kipchoge alishinda shindano la upande wa wanaume katika mbio hizo.

Mshindi huyo ameonekana kuweka rekodi ya aina yake kwa kuwa licha ya kuwa na umri mkubwa, lakini bado aliibuka mshindi.

Alitumia muda wa saa 2 dakika 3 na sekunde 5 kumaliza na kuibuka na ushindi huo ambapo akionekana akiwa amechoka.

Papa Wemba afariki jukwaani akitumbuiza Abidjan, Ivory Coast



Na Mwandishi Wetu
GWIJI wa muziki wa Kikongo, Papa Wemba (pichani) anayejulikana kwa majina mengi yakiwemo King of Rhumba Rock, amefariki dunia baada ya kuanguka jukwaani wakati akitumbuiza jijini Abidjan, Ivory Coast.

Papa Wemba ni mmoja wa wanamuziki waliochangia kukua kwa muziki wa Afrika na pia wanamuziki wengi wakubwa wamepita mikononi mwake.

Mpaka mauti yanamkuta alikuwa na umri wa miaka 66, video ya tukio inaonyesha alianguka ghafla wakati wacheza shoo wake wakiwa mbele ya jukwaa na waliendelea kucheza kwa hatua kadhaa kabla ya kusitisha na kwenda kumuangalia akiwa chini.

Inaelezwa kuwa tukio la kuanguka lilitokea mara baada ya Papa Wemba kuimba wimbo wake wa tatu jukwaani hapo.

Kituo cha redio cha Okapi cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kilitangaza juu ya kifo hicho, lakini hakikusema sababu haswa zilizoondoa roho ya mkongwe huyo.
 
Marehemu ambaye jjina lake halisi ni Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba alikuwa kitumbuiza kwenye Tamasha la Urban Music Festival

Papa Wemba
Kuzaliwa: Juni 14, 1949
Kufariki: Aprili 24, 2016
Aina ya muziki aliokuwa akiimba: Soukous, Rhumba.

Friday, 22 April 2016

Tasuba walivyokabidhiwa vifaa vya muziki vyenye thamani ya sh. mil 80 na Kituo cha Utamaduni na Maendeleo cha Denmark (CKU)

Kundi la Matarumbeta la Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (Tasuba) nalo lilitumbuiza siku hiyo muhimu.
Wageni kutoka mataifa mbalimbali nao walikuwepo kushuhudia makabidhiano hayo ya vyombo vya muziki Tasuba.

Wanafunzi wakiimba kabla ya makabidhiano hayo ya vyombo.


Maigizo nayo yalikuwepo katika hafla hiyo.

Sarakasi ilikuwa balaa na kuwaacha watu hoi kwa mibinuko na mikunjo.

Akina dada nao hawakuwa nyuma katika sarakasi za kichina china.






Mchezo wa kuigiza uliokuwa unaelezea changamoto wanazopata wanafunzi wa muziki Tasuba kwa ukosefu wa vifaa vya muziki, ambavyo Kituo cha Utamaduni na Maendeleo cha Denmark (CKU) kilitoa vifaa hivyo vyenye thamani ya sh. milioni 80 ili kutatua tatizo hilo.


 

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Leah Kihimbi akiangalia moja ya vifaa vya muziki wakati wa makabidhiano hayo. Kushoto ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tasuba, Michael Kandinde.

Mwalimu wa muziki Andrew Nyakasi akipiga kinanda mumuonesha Kaimu Mkurugenzi wa Sanaa, Leah Kihimbi wakati wa makabidhiano ya vifaa vya muziki Tasuba.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni ya Bagamoyo (Tasuba), Michael Kandinde

Msimamizi wa Programu ya muziki nchini Tanzania wa Kituo cha Utamaduni na Maendeleo cha Denmark (CKU), Mandolin Kihindi wakati wa hafla hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Leah Kihimbi


Thursday, 21 April 2016

Yanga yaanza mbio za kusaka bil 1.36 Kombe la Shirikisho ikianza kwa kucheza na Sagrada Esperanca ya Angola




Na Mwandishi Wetu
SIKU moja baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga imeangukia kwa Sagrada Esperanca ya Angola katika michuano ya kuwania ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Itakutana na Waangola hao katika hatua ya mtoano ambayo mshindi wake ataingia hatua ya makundi ya michuano hiyo inayoshika nafasi ya pili kwa ukubwa katika ngazi za klabu barani Afrika.

Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jana alasiri, Yanga baada ya kufungwa 2-1 na Ahly juzi usiku huko Alexandria na hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 3-2, sasa itakipiga dhidi ya timu hiyo inayomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa la Angola.

Itaanza kwa kuwakaribisha Waangola hao kati ya Mei 6 na 8 jijini Dar es Salaam na marudiano kuwa kati ya  Mei 17 na 18 nchini Angola.

Haijafahamika Angola zitachuana katika mji gani, ingawa Sagrada iliyoanzishwa Desemba 22, mwaka 1976, yaani miaka 39 iliyopita, uwanja wake wa nyumbani upo Dundo, katika Jimbo la Lund Norte ambao una uwezo wa kuingiza mashabiki 3,000 kwa wakati mmoja.

 Kama Yanga vile; timu ya Sagrada Esperanca ya Angola, ambayo itacheza na Yanga.
Endapo itafanikiwa kuwangoa Sagrada inayonolewa na Zoran Mackic, raia wa Serbia, Yanga itakuwa imejihakikishia kusaka mamilioni ya fedha katika michuano hiyo ambayo mshindi wake hutwaa kitita cha dola za Kimarekani 625,000 (sh bilioni 1.36).

Mshindi wa pili hupata dola 432,000 (sh milioni 907) wakati timu zinazoshika nafasi ya pili na ya tatu katika kila kundi hupata dola 239,000 (sh milioni 500) na ya mwisho katika kundi, yaani inayoshika nafasi ya nne, huambulia dola 150,000 (sh milioni 315).

Wakati Yanga ikiangukia kwa Waangola, waliokuwa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe waliovuliwa ubingwa juzi,  watakutana na Waarabu wa Tunisia, Stade Gabesien, huku Esperance pia ya Tunisia iliyoitoa Azam FC ikipangwa kukutana na Mo Bejaiaa ya Algeria.

Michezo mingine ya mtoani itakuwa kati ya Stade Malien (Mali) na FUS Rabat (Morocco), Etoile du Sahel (Tunisia)  na CF Mounana (Gabon), Al-Ahli Tripoli (Libya) na Misr El-Makasa (Misri), Al-Merreikh (Sudan)   na Kawkab Marrakech (Morocco), wakati Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini itacheza na Medeama ya Ghana.

Yanga na timu nyingine zilizotolewa katika Hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika, zimeangukia Kombe la Shirikisho kama Kanuni za CAF zinavyoeleza kuwa, timu ambazo zitatolewa katika Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa zitaangukia Kombe la Shirikisho kukutana na timu nane zilizosonga mbele ambapo zitacheza mechi za mtoano za nyumbani na ugenini kisha zitakazofuzu zitaingia hatua ya makundi.