Thursday, 24 September 2015

Mtu aliyegoma kuacha kuvuta sigara ndani ya ndege apigwa faini na kufunguliwa mashtaka





BRISBANE, Australia
MTU mmoja ambaye aligoma kuacha kuvuta sigara katika ndege kutoka Sydney kwenda Sunshine Coast alijikuta matatani na kupigwa faini ya dola za Marekani 850 ikiwa ni mara 10 ya gharama ya njia moja ya tiketi.

Polisi walisema kuwa mfanyakazi wa ndege alimuomba mtu huyo mwenye umri wa miaka 37 kuacha kuvuta sigara wakati wa safari hiyo ya ndege ambayo ingechukua dakika 90 jana, lakini alipuuza na kuendelea kupuliza moshi hewani.
 
Wakati ndege hiyo ilipotua katika uwanja wa ndege wa Sunshine Coast majira ya saa 12:30 jioni, polisi waliingia ndani ya ndege hiyo na kumkamata mtu huyo.

Mtu huyo kutoka Caboolture (Kaskazini ya Brisbane, Australia),kilometa 55 kusini mwa pwani ya Sunshine na kufunguliwa mashtaka na anatakiwa kufika mahakamani Oktoba 12, polisi ilisema.

Mapema mwaka huu, abiria aliyepanda ndege hiyo ya Jetstar kutoka Gold Coast kwenda Sydney aliwasha sigara katika chumba cha kupumzikia, na kulazimisha ndege kubadili mwelekeo na kwenda Newcastle ambako ilitua kwa dharura.

Kuvuta sigara kumepigwa marufuku ndani ya ndege za Australia na atakayepuuza amri hiyo anapigwa faini ya dola za Marekani850.

Mamia ya Mahujaji wauawa Makka kwa kukanyagana



Na Mwandishi Wetu
WATU 717 ambao walikuwa wanashiriki ibada ya Hijja nchini Saudi Arabia wamefariki kutokana na kukanyagana karibu na mji mtakatifu wa Makka, maofisa wa Saudi wamesema.

Watu wengine 863 wamejeruhi katika tukio hilo lililotokea Mina, ambako mahujaji milioni mbili walikuwa wakishiriki katika shughuli ya mwisho ya ibada hiyo kubwa ya Hijja.

Ni ajali kubwa zaidi kuwahi kutokea katika miaka 25 ya Hijja.

Maandalizi ya ibada hiyo ambayo ni nguzo ya tano ya dini ya Kiislamu yaligubikwa na fadhaa baada ya winchi kuanguka katika Msikiti Mkuu wa Makka mwezi huu na kuua watu 109.

Mahujaji walikuwa wakisafiri kwenda Mina, bonde kubwa kiasi cha kilometa tano kutoka Makka, wakati wa mahujaji kurusha mawe katika nguzo saba zinazoitwa Jamarat ambazo zinawakilisha shetani.

Nguzo hizo zimesimama katika maeneo matatu, ambako Shetani inaaminika alijaribu kumrubuni Nabii Abraham.

Watu walikuwa wakielekea kwenda kumrushia mawe shetani wakati wengine walikuwa wakirudi upande mwingine. Kisha ikaanza kuwa vurugu na ghafla watu wakaanza kuanguka.

Kulikuwa na watu kutoka Nigeria, Niger, Chad na Senegal miongoni mwa mataifa mengine. Watu walikuwa wakikanyagana ili kwenda sehemu salama na hivyo ndivyo vifo vilivyotokea.

Watu walikuwa wakitaja jina la Mwenyezi Mungu wakati wengine wakilia wakiwamo watoto wadogo na wachanga. 

Wengine walianguka wakiomba msaada, lakini hakukuwapo na yeyote wa kufanya hivyo. Kila mmoja alionekana kuwa na lake.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Makka, viongozi wa Tanzania akiwamo Mufti Shekhe Mkuu wa Tanzania, Abubakari Zubery, walieleza wakati tukienda mitamboni kwamba hakukuwa na taarifa ya kuwapo kwa mwathirika ambaye ni Mtanzania, na taarifa rasmi zinatarajiwa kutolewa leo.

Katika hatua nyingine, Serikali imesisitiza amani, upendo na mshikamano katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, huku ikionya kuwa itakabiliana na wote watakaofanya vitendo vitakavyoashiria kutaka kuvunja amani ya nchi wakati huu wa kampeni, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.


Saturday, 19 September 2015

tsunami ya Yanga kuiangukia JKT Ruvu leo Uwanja wa Taifa



Na Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga, leo wanashuka tena kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kucheza na JKT Ruvu.

Yanga inashuka dimbani ikiwa inaongoza katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kushinda mechi zake mbili na kujikusanyia pointi zote sita huku ikifunga mabao matano.

Katika mchezo wa kwanza, Yanga ilishinda Wagosi wa Kaya Coastal Union kwa mabao 2-0 kabla ya kuibuka na ushindi mwingine wa mabao 3-0 dhidi ya Prisons ya Mbeya.

Timu hiyo itacheza mechi nne mfululizo kwenye uwanja wake wa nyumbani kwani baada ya mchezo wa leo, itashuka tena dimbani kumenyana na watani zao wa jadi Simba Septemba 26 kabla ya kuanza kutoka wakati itakapocheza na Mtibwa Sugar Septemba 30 kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Yanga inahitaji ushindi katika mchezo huo ili iweze kuzidi kukalia kiti hicho na kufanya biashara mapema kabla ya kuhesabu mapato jioni.

Yanga imeshafunga mabao matano katika mechi mbili na haijafungwa bao hata moja, hivyo inaonesha jinsi safu yake ya ushambuliaji kama akina Donald Ngoma, Hamisi Msuva, Amiss Tambwe na wengineo ilivyo na uchu wa mabao, hivyo mabeki wa maafande wa JKT Ruvu watakuwa na kibarua kigumu cha kuwazuia wasifunge.

Hata hivyo, kikosi cha JKT Ruvu kinachofundishwa na mchezaji na kocha wa zamani wa Yanga, Fred Minziro hakitakubali kufa kikondoo, kwani kinazihitaji sana pointi hizo tatu ili kurejesha matumaini ya kufanya vizuri.

JKT Ruvu ndio inaburuza mkia baada ya kufungwa mechi zote mbili za mwanzo na kuifanya kuwa na kazi kubwa ya kufanya ili kutoka na pointi zote tatu au moja kwa kutoka sare.

Kocha wa JKT Ruvu, Minziro alikiri kuanza vibaya kwa ligi hiyo lakini alisema leo hawatakubali kufungwa licha ya uimara wa Yanga ambayo ina wachezaji wengi wazuri, wakiwemo wa kutoka nje ya nchi.

Alisema kuwa timu yao ilianza vibaya mechi mbili za mwanzo baada ya wachezaji wake kutokuwepo katika maandalizi ya mwisho baada ya kuwa katika mashindano ya majeshi nchini Uganda kwa takribani siku 11.

Pia alisema timu yake ina majeruhi wawili, lakini alikuwa na imani siku zinavyokwenda timu hiyo itazidi kuimarika na kufanya vizuri katika mechi zao zijazo.

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub alisema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaondoka na pointi zote tatu ili kuzidi kungara katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.

Mechi zingine leo ni Stand United watachea na African Sports katika mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, huku Mgambo Shooting itawakaribisha wana Lizombe Maji Maji ya Songea katika uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Mbeya City wenyewe watakuwa wageni wa ndugu zao wa Tanzania Prisons katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Wakati Mbeya City ni ya nane baada ya kuwa na pointi tatu kutoka katika mechi mbili walizocheza, Tanzania Prisons wenyewe ni wa pili kutoka mkiani wakiwa hawana pointi hata moja baada ya kuchapwa mechi zote mbili za mwanzo.

Mechi hizo zitaendelea tena kesho Jumapili kwa Mwadui ya Shinyanga kuikaribisha Azam FC huku kocha wa wenyeji hao Jamhuri Kihwelu kutamba kuibuka na ushindi.

Mtibwa Sugar watacheza na Ndanda FC katika mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wa Manungu, Turiani wakati Simba baada ya kuanza kwa kucheza mechi mbili ugenini, kesho kwa mara ya kwanza itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa ikicheza na Kagera Sugar.

African Sports wenyewe watakuwa mwenyeji wa Toto Africans ya Mwanza katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Wananchi wa Finland watoa viatu vya mamilioni kwa Riadha Tanzania


Kaimu Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Ombeni Zavalla (kushoto) akimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Liike, Ari Koivu baada ya kukabidhiwa maboksi 15 ya zaidi ya jozi 400 za viatu vilitolewa na wananchi wa Finland kwenye Uwanja wa Taifa wiki hii.

 Na Mwandishi Wetu
RIADHA Tanzania (RT), wiki hii ilipokea jozi za viatu 450 zenye thamani ya sh. 45,000,000 kutoka kwa wananchi wa Finland.

Viatu hivyo vitasaidia katika maandalizi ya wanariadha wa Tanzania kushiriki mashindano mbalimbali yatakayofanyika nje ya nchi.
 
Akikabidhi viatu hivyo, Ari Koivu ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa wa taasisi ya Toiminnanjohtaja alisema kuwa, viatu hivyo pamoja na samani za ofisi vimetolewa na watu wa Finland ili kusaidia maendeleo ya michezo hapa nchini.

Alisema kuwa ameamua kutafuta vifaa hivyo kwa RT kutokana na mapenzi yake kwa Tanzania ili kuendeleza michezo na hasa riadha nchini.

Mbali na RT pia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Sayansi ya Michezo, baadhi ya shule za msingi na sekondari za Mtwara na Lindi nazo zimefaidikana msaada kutoka Finland, ambao ni tofauti na ule waliopewa RT.
 
Alisema kuwa mpango wa maendeleo ya michezo mikoa hiyo ya kusini utafaidika na msaada huo.
 
Kaimu Katibu Mkuu wa RT, Ombeni Zavalla alisema kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka kwani sasa wanajiandaa kuanza mazoezi kwa ajili ya mashindano mbalimbali ikiwemo Michezo ya Olimpiki itakayofanyika Rio, Brazil mwakani.

Alisema kuwa viatu hivyo vitawasaidia sana wanariadha kujiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano mbalimbali, ambapo aliwataka wadau wengi kujitokeza kusaidia mchezo huo.


Ari Koivu (kulia) akimkabidhi jozi ya viatu mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Riadha Tanzania (RT), Rehema Killo `Mbeya wa Mtaa'.
Zacahria Gwandu, mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya RT akipokea jozi yake.



Add caption
Waandishi wa habari nao walipata mgao wa viatu na wengine jezi hivyo kutoka Finland.



Dk. Hamad Ndee (katikati) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa mgao wa chuo hicho.

Add caption